Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Gimbi Dotto Masaba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. GIMBI D. MASABA aliuliza:- Wakazi wengi wa Mkoa wa Simiyu huendesha maisha yao kwa kutegemea kilimo na ufugaji, ambapo Mkoa huo umepakana na maeneo makubwa na mazuri kwa kazi hizo jirani na Mbuga ya Serengeti:- (a) Je, Serikali itatenga lini maeneo ya kilimo na mifugo kwenye vijiji vinavyopakana na Mbunga ya Serengeti? (b) Je, Serikali itathamini lini mifugo na mazao ya wakulima hawa kama vile inavyothamini wanyamapori wa mbugani kwani huonekana ni halali kwa wanyama pori kuua/kuharibu mazao ya wananchi wakati siyo halali wananchi kuingiza mifugo au kuchimba hata mizizi ndani ya mbuga ya wanyama?

Supplementary Question 1

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Pamoja na majibu ya Waziri katika majibu yake ya msingi amekiri kwamba Serikali inachukua hatua kuhakikisha kwamba wanatatua migogoro inayohusiana na wafugaji na hifadhi.
Sasa swali, Waziri utakuwa tayari kuongozana na mimi kuelekea Mkoani Simiyu kwenda kutatua migogoro inayoendelea katika vijiji vya Nyantugutu, Lumi na Longalombogo kwenda kutatua migogoro hiyo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili wananchi wa Wilaya ya Meatu na Wilaya ya Maswa wengi wao hawana maeneo ya kuchungia mifugo yao. Je, Serikali itakuwa tayari kurudisha Pori la Akiba la Maswa ili wananchi hawa waweze kutumia kama malisho, kwa sababu pori hilo limekosa sifa ya kuwa Hifadhi ya Taifa?

Name

William Tate Olenasha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusu kama nitakuwa tayari kuandamana na yeye ndani ya Bunge hili kwenda kutatua migogoro, nimshauri Mheshimiwa Mbunge kwamba labda baada ya kikao cha leo tukutane nimshauri zaidi namna ya kutatua hili kwa sababu itabidi aongee na watu wa maliasili kwa sababu Wizara yetu hasa haihusiki na migogoro kati ya hifadhi na wananchi lakini nitamshauri namna ya kufanya hivyo na nitamshauri vizuri.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Pori la Akiba la Maswa kutolewa kwa ajili ya wafugaji nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba mimi ni jirani yake, mimi natoka Ngorongoro nafahamu changamoto iliyopo kati ya wafugaji na pori la Maswa.
Mheshimiwa Spika, kuna mkakati ambao unaendelea sasa Serikalini kama ulivyosikia wiki iliyopita Waziri Mkuu alivyozungumza wa kuangalia namna ya kuondoa migogoro hii, vilevile kuangalia namna ya kutafuta ardhi kwa ajili ya wafugaji ikiwa ni pamoja na kutafuta uwezekano wa baadhi ya maeneo ambayo yamepoteza hadhi ya kihifadhi ili wafugaji waweze kugaiwa.
Mheshimwia Spika, hili linaendelea siwezi kusema moja kwa moja sasa kwamba, Pori la Maswa ni moja kati ya haya maeneo lakini kuna mipango ya kujadili suala kama hilo. Nimueleze Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na migogoro hii kuongezeka lakini bado kama Taifa tuna jukumu la kuhifadhi wanyama, tunafahamu kwamba ni rasilimali muhimu, tusipohifadhi baada ya muda inawezekana tusiwe na wanyama pori ambao wanaendelea kuletea nchi yetu fedha za kigeni lakini vilevile sifa. Nashukuru sana.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba nitoe mawazo kuhusu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama mtakuwa mmeangalia takwimu za sensa ya mwaka 2012 mtaona kabisa katika ile Sensa ya Watu na Makazi kwamba eneo la asilimia 10 la surface area ya Tanzania Bara limetengwa kwa ajili ya mifugo, eneo hilo bado halitumiki ipasavyo. Niseme tu kwa sababu muda mwenyewe ni mfupi kwamba Serikali haina mpango wa kuhuisha maeneo ya hifadhi kuwa maeneo ya kuchunga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka pia niseme kwamba wote kabla hatujawa Wabunge hapa baada ya kushinda uchaguzi tuliapa kiapo cha uaminifu cha kuilinda, kuihifadhi na kuitunza Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sehemu ya 27 ya Katiba hiyo inasema; kila mtu anao wajibu wa kulinda maliasili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Name

Andrew John Chenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Primary Question

MHE. GIMBI D. MASABA aliuliza:- Wakazi wengi wa Mkoa wa Simiyu huendesha maisha yao kwa kutegemea kilimo na ufugaji, ambapo Mkoa huo umepakana na maeneo makubwa na mazuri kwa kazi hizo jirani na Mbuga ya Serengeti:- (a) Je, Serikali itatenga lini maeneo ya kilimo na mifugo kwenye vijiji vinavyopakana na Mbunga ya Serengeti? (b) Je, Serikali itathamini lini mifugo na mazao ya wakulima hawa kama vile inavyothamini wanyamapori wa mbugani kwani huonekana ni halali kwa wanyama pori kuua/kuharibu mazao ya wananchi wakati siyo halali wananchi kuingiza mifugo au kuchimba hata mizizi ndani ya mbuga ya wanyama?

Supplementary Question 2

MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali napenda tu nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba katika vile vijiji 73 ambavyo vimeshaandaa Mpango Shirikishi wa Matumizi Bora ya Ardhi, ni vijiji vingapi vipo katika Wilaya ya Bariadi. Ahsante.

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mtemi Andrew Chenge, kama ifuatavyo:-
Kwanza kabisa vijiji vilivyoulizwa kwenye swali la msingi baadhi yake mimi nilishafika akiwa amenipeleka Mheshimiwa Njalu enzi zile nimeenda na helicopter wakati wa kampeni na nikapokea kile kilio cha wananchi wake, nilipanga kwamba nitafika katika eneo hilo baada ya bajeti kwa ajili ya kujionea hali hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukirudi kwenye swali hili alilolisemea Mheshimiwa Mtemi Andrew Chenge linalohitaji idadi ya vijiji, suala hili la migogoro limekuwa endelevu kutokana na kupanuka kwa idadi ya mifugo pamoja na ongezeko la wanadamu na mahitaji ya matumizi ya ardhi, kwa hiyo, kila wakati panapokuwa pamepimwa, panakuwa pana uhitaji zaidi.
Mheshimiwa Spika, hivi tunavyoongea tayari zaidi ya vijiji 23 vilishafanya upimaji huo lakini mahitaji ni makubwa kuliko idadi hiyo ya vijiji na nitawaomba Wabunge wanaotoka maeneo ya wafugaji waungane na viongozi wa wafugaji ambao tumewaomba watuorodheshee mapendekezo ya maeneo yanayoweza kutatua matatizo haya, lakini pia na maeneo ambayo yana migogoro ili Serikali tuweze kupitia mgogoro mmoja baada ya mwingine ili tuweze kupata majibu ya kudumu kwa ajili ya watu wetu wanaogombana katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, jambo hili tumelipanga kati ya Ijumaa na Jumatatu tutakuwa tumeshapata taarifa hiyo na Waheshimiwa Wabunge wote mnaotoka maeneo ya aina hiyo mtatangaziwa ili tuweze kukaa pamoja. Jambo hili linahitaji ushirikiano wa pamoja na uamuzi wa pamoja katika kupata majawabu ya kudumu na kuondokana na tatizo hili.