Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Primary Question

MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:- Wilaya ya Momba ni moja kati ya Wilaya mpya zilizoanzishwa hivi karibuni ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi:- Je, kwa nini Serikali imekuwa ikisuasua kutoa fedha ili ziweze kujenga ofisi na nyumba za watumishi katika Makao Makuu ya Wilaya ya Momba eneo la Chitete?

Supplementary Question 1

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini niseme Serikali inaonekana haiko serious katika hizi Halmashauri mpya ambazo tumekuwa tukizianzisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2014/2015 Halmashauri ya Wilaya ya Momba tuliomba shilingi bilioni mbili fedha maalum, maombi maalum, kwa ajili ya kuanzisha ujenzi wa Makao Mkuu yaani kwa maana ya kujenga boma na nyumba za watumishi ili watumishi watoke katika Halmashauri mama ya Mbozi kwenda Momba eneo la Chitete wakaanze kazi maalum. Mwaka 2014/2015 ukiangalia hapa hapa Serikali haijatenga kitu chochote, ni kwa nini Serikali inakuwa haiko serious inapoanzisha Wilaya mpya kwa ajili ya maandalizi ya watu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali (b), Halmashauri ya Momba ipo katika Mkoa mpya wa Songwe ambao na wenyewe umeanzishwa hauna Mkuu wa Mkoa, hauna ofisi, hauna chochote. Ni kwa nini Serikali imekuwa ikianzisha jambo la msingi lakini utekelezaji imekuwa ikishindwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kupata majibu lini Mkoa Mpya wa Songwe utapelekewa Mkuu wa Mkoa na ofisi itakuwepo pamoja na Halmashauri ya Mombo? Ahsante.

Name

Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI WA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Silinde anasema kwamba Serikali haina nia ya dhati. Kikubwa zaidi naomba kwanza Bunge lako hili, tukiri kwamba miongoni mwa mambo ambayo Watanzania wametendewa haki na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni pale ambapo maombi yamepelekwa ya Mikoa, Halmashauri na Wilaya mpya na Serikali ikaamua kutekeleza hili ili mradi suala la kuleta huduma kwa wananchi, naomba tukiri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo ukija kuangalia katika ujenzi wa Ofisi za Wilaya peke yake, takribani Serikali ilitenga ujenzi wake kupitia TBA zaidi ya bilioni 12.9. Katika mchakato huo zaidi ya bilioni 5.6 zimepelekwa na mchakato mwingine unaendelea. Naomba tukiri kwamba rasilimali fedha ndiyo lilikuwa tatizo, lakini Serikali inajitahidi kuhakikisha kwamba, Halmashauri na Wilaya zilizojengwa na Mikoa iweze kufanikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima hususan la Mkoa wa Songwe, Serikali imejipanga itajitahidi kwa kadri iwezekanavyo na ukija kuangalia hivi sasa, tuna Mikoa hii mipya iliyoanzishwa na lengo kubwa ni kukusanya mapato. Mwisho wa siku ni kwamba ofisi hizi na hasa masuala ya kiutawala, ngazi za utawala ziweze kukamilika ilimradi wananchi waweze kupata huduma, lakini Serikali imejidhatiti katika hilo kwa ajili ya kuleta huduma kwa wananchi.

MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE - WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Pengine bila kurudia yale aliyoyasema, nimesimama ili tu niongezee jibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Silinde anasema Mkoa wa Songwe umeanzishwa, mchakato wa Mkoa wa Songwe kuanzishwa haujakamilika kwa sababu hadi sasa hatuja-gazette. Kwa hivyo, huwezi ukaanza kumhudumia mtoto kabla hajazaliwa, unamnunulia nguo za kwenda shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakachofanya kwa sasa baada ya muda tutatoa tamko rasmi la Serikali na tamko la Serikali huwa lipo kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, tukishaipa GN, tutatamka kwamba Rais ameuanzisha huo Mkoa. Naomba uvumilie, lakini napongeza pia, najua una hamu kweli kuanza kuingia katika Mkoa wa Songwe, lakini taarifa hiyo uliyoitoa ni kwamba bado hatujauanzisha rasmi Mkoa wa Songwe, subiri tutatamka wakati wowote Serikali itakapokuwa tayari imemaliza mchakato wake. (Makofi)