Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA Aliuliza: - Je, ni lini Serikali itawalipa wakulima wa tangawizi Mamba Myamba, Wilaya ya Same Mashariki ambao walifungiwa na SIDO mashine zisizo na kiwango cha kuchakata tangawizi?

Supplementary Question 1

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwanza napenda kusema kwamba Serikali imepotosha Bunge lako Tukufu kwa kusema uongo ambao haukubaliki. Je, Waziri anajua kwamba TAMISEMI chini ya Waziri Jafo waliunda Kamati ya Uchunguzi (fraud) mwaka 2018 na Kamati hii ilitoa mapendekezo kuonesha jinsi SIDO ilivyowaibia wakulima pamoja na Halmashauri ambayo haikufanya kazi yake vizuri kuwasahauri wakulima na michango ambayo ilitolewa na Rais wakati huo Kikwete, karibu shilingi milioni 300 haikutumika vizuri na akaomba hatua madhubuti zichukuliwe na SIDO ilipe hela zile za wakulima?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri ana habari kwamba kutokana na kutofanya kazi kwa mitambo ile ndiyo maana sasa hivi PSSF imenunua mitambo mipya na inaifunga kwa kuona kwamba mitambo ile iliyofungwa ilikuwa batili? Inakuwaje Waziri…

NAIBU SPIKA: Umeshauliza maswali mawili tayari.

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kaboyoka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme hakuna uongo ambao umesemwa katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba SIDO baada ya kuingia mkataba ule na kuweza kufunga mtambo ule kulikuwa na changamoto mbalimbali na hasa kwenye upande wa ukaushaji katika mchakato ule. Baada ya kujadiliana na Halmashauri ya Same ikaonekana kwamba wakulima wale walikuwa hawaridhishwi na utendaji wa mitambo ile kwa hiyo SIDO ilishirikiana na mradi wa Market Infrastructure, Value Addition And Rural Finance - MIVARF kuagiza mtambo mpya ambao ulikuwa na gharama ya shilingi milioni 29 na SIDO walichangia katika mtambo huo mpya shilingi milioni 9 na ukafungwa kama nilivyosema tarehe 27/02/2015 na ukaendelea kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na hasara au gharama ambazo zilikuwa zimeingiwa na wakulima wale baada ya kuwa mtambo ule haufanyi kazi vizuri, kama nilivyosema tunaielekeza SIDO waweze kufanya mashauriano na Halmashauri ili waone namna gani ya kuwafidia wakulima wale ambao walipoteza mazao yao kipindi kile ambapo mtambo ule ulikuwa haufanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtambo uliopo sasa hivi unafanya kazi vizuri na yeye atakuwa ni shahidi. Wakulima wale wameridhika na wanaendelea kufanya kazi zao za kuchakata zao la tangawizi.