Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Devotha Methew Minja

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:- Wazee ni hazina ya Taifa lakini wapo wazee wasiojiweza ambao Serikali imewapa hifadhi katika kambi mbalimbali ikiwemo Kambi ya Fungafunga ya Mjini Morogoro. Hata hivyo, kambi hiyo ni chakavu kwa muda mrefu hali inayosababisha wazee kuendelea kuishi katika mazingira magumu:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati kambi hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikiliza majibu ya Serikali na nilitarajia kwa kuwa Serikali hii inakusanya kodi basi ingetilia mkazo katika ujenzi wa nyumba hizi za wazee ambazo nyingi ni chakavu na nyingi zimegeuka kuwa magofu walau wazee hawa nao wajisikie kuwa ni sehemu katika Taifa hili. Swali la kwanza, je, ni upi mkakati thabiti wa Serikali kuhakikisha kuwa nyumba hizi za wazee zinakarabatiwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, Serikali imekuwa ikitoa maagizo kuwa wazee wote watapata huduma za matibabu bure lakini hali ilivyo hivi sasa wazee wengi hawapati matibabu kama inavyopaswa katika hospitali za Serikali na hata katika vituo vya afya. Je, ni lini Serikali italeta sheria hapa Bungeni ambayo itasimamia matibabu na maslahi ya wazee hao? (Makofi)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Devotha Minja kwa maswali yake mazuri na kwa kufuatilia kwa karibu masuala ya wazee hususan katika kambi hii ya Fungafunga pale Morogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi na naomba nitoe maelezo ya awali kwamba Serikali tuna kambi 17 za kuhudumia wazee. Hata hivyo, kwa mujibu wa sera yetu Serikali inachukua wazee pale inapoonekana yule mzee hana watoto wa kumtunza, ndugu na watu katika jamii ambao wanaweza wakamtunza. Mpaka sasa hivi tuna wazee takribani 500 ambao tunawahudumia sisi kama Serikali ambapo katika vigezo hivyo vitatu ambavyo nimevisema pale awali wametimiza na ndiyo maana tunawachukua na sisi kama Serikali tunawatunza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukarabati wa hii miundombinu ya vituo vyetu 17 umeshaanza na vituo ambavyo tumeshavifanyia ukarabati ni pamoja na Bukumbi, Mwanzage na Magugu. Aidha, tumejenga tena nyumba mpya pale Kolandoto na tumefanya ukarabati wa bweni pale Kilima. Ndiyo maana nasema tunakwenda awamu kwa awamu kuhakikisha kwamba hizi kambi zote tunaweza kuzifikia na kuzifanyia ukarabati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na matibabu kwa wazee, Serikali ilitoa agizo kwamba wazee wote ambao wamefika umri wa zaidi ya miaka 60 wapate vitambulisho ili waweze kupata matibabu bure. Kumekuwa na changamoto kidogo ya kusuasua katika utekelezaji kwenye baadhi ya Halmashauri kutoa vitambulisho. Nitumie fursa hii kuzikumbusha Halmashauri kuzingatia agizo hili la Serikali la kutoa vitambulisho kwa wazee ambao wamefika miaka 60 na vilevile kutenga madirisha mahsusi kwa ajili ya wazee.

Mheshimiwa Naibu Spika, suluhu ya kudumu ya jambo hili ni hili jambo ambalo tunataka kulifanya kama Serikali kuhakikisha kwamba kila mtu anaingia katika mfumo wa Bima ya Afya ya Wote. Mwezi Septemba tunataka tulete Muswada ambapo utaratibu wa kuwa na bima utawekwa ili kuhakikisha wanapata huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, tunatambua kwamba kuna magonjwa mahsusi ya wazee na sisi wataalam tuna kitu kinaitwa geriatric medicine. Ndani ya Wizara, tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba haya magonjwa ambayo ni mahsusi kwa wazee nayo tunayawekea utaratibu ili wazee waweze kupata matibabu kulingana na magonjwa waliyonayo.