Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Oran Manase Njeza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbeya Vijijini

Primary Question

MHE. ORAN M. NJEZA Aliuliza:- Ili kuboresha kilimo na ujasiriamali inahitajika elimu kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kuwa na vyanzo vya uhakika vya mtaji. (a) Je, Benki ya Kilimo ina mtaji kiasi gani? (b) Je, Benki ya Kilimo ina mkakati gani wa kuwafikia wakulima wadogo wa Wilaya ya Mbeya?

Supplementary Question 1

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, na inavyoonesha Benki ya Kilimo bado ina mahitaji ya mtaji mkubwa hasa ukizingatia kuwa kilimo kwa nchi yetu ndiyo tunakitegemea kwa kiasi kikubwa kwenye uchumi. Sasa ukiangalia katika jibu kwa Mkoa wa Mbeya ambayo imeoneshwa kuwa zimepelekwa shilingi milioni 700 lakini na hizi Wilaya alizozitaja Mheshimiwa Waziri siyo za Mkoa wa Mbeya ni za Mkoa wa Songwe. Kwa hiyo kwa jibu hilo inaelekea kabisa Mkoa wa Mbeya haujanufaika na mikopo ya Benki ya Kilimo.

Sasa swali langu; je, ni kwa kiasi gani Serikali imeweza kufanya tathmini ya mahitaji halisi ya mtaji wa Benki ya Kilimo? Na je, mtaji huo utapelekwa Benki ya Kilimo ukiondolea mbali hiyo mikopo ya ADB utapelekwa lini huo mtaji kwa Benki ya Kilimo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kiasi kikubwa ukiwapa wakulima mikopo risk kubwa iko kwenye bei kwa sababu bei za mazao hazieleweki, kuna risk sana kwenye bei. Sasa kwa kiasi gani Benki ya Kilimo kwa kutumia instruments za kibenki na vilevile kwa kusaidiana na taasisi zingine kama commodity exchange (TMX) zimeweza kutengeneza utaratibu wa kuondoa hiyo risk, wa ku-manage hiyo risk ambayo inatokana na changamoto za bei za mazao yetu? Ahsante.

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza lenye (a) na (b), tathmini ya mtaji na utapelekwa lini; tathmini ya mtaji ilishafanyika na kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi tunaangalia njia nyingine za ku-finance benki yetu ya kilimo ili iweze kuwa na uwezo wa kuwakopesha wateja wake ambao ni wakulima wadogo, wa kati pamoja na wakubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu Bunge lako tukufu likafahamu kwamba mabenki yote hayakopeshi kupitia mtaji, yanakopesha kupitia njia nyingine, co-financing agreement, ndiyo maana Serikali ilitafuta mkopo wa bei nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika na ikaipatia Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania. Kwa hiyo, hilo naomba Waheshimiwa Wabunge tulifahamu; hakuna benki yoyote inayokopesha kupitia mtaji wake, inakopesha kupitia amana na njia nyingine za utafutaji wa fedha ili iweze kuwahudumia wateja wake. Serikali ipo tayari kabisa kuiwezesha benki yetu kupitia mipango mingine ili ipate fedha za kutosha za kuwahudumia wakulima wetu ambao ndio lengo kubwa la uanzishwaji wa benki hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la risk ya masoko; TMX ambalo ni Soko la Bidhaa Tanzania, limeanza kazi vizuri mwaka huu na tayari tumeona baadhi ya mazao kwa mfano ufuta ambao umetafutiwa soko zuri na Soko letu la Bidhaa Tanzania wameweza kutafuta masoko na sasa tunaendelea kutafuta masoko mengine kupitia Soko la Bidhaa Tanzania kwa ajili ya mazao yaliyobaki ili kuwasaidia wakulima wetu kuondokana na vihatarishi vya ukosefu wa bei au bei isiyoeleweka kwenye masoko yetu.