Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Lolesia Jeremia Maselle Bukwimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Busanda

Primary Question

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA (K.n.y JOSEPHINE T. CHAGULA) aliuliza:- Hospitali ya Mkoa wa Geita haina jenereta la dharura pindi umeme unapokatika na hivyo kusababisha vifo vingi kutokea:- Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka jenereta la dharura katika hospitali hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali ya nyongeza:

Mheshimiwa Spika, kwanza niipongeze sana Serikali kwa kupeleka jenereta tena kwa ajili ya kuendeleza huduma katika hospitali ya Mkoa wa Geita, lakini bado kuna changamoto nyingine pia kwamba hospitali ya Mkoa wa Geita pia ina upungufu mkubwa sana wa watumishi. Je, Serikali inasemaje kuhakikisha kwamba watumishi hawa wanapatikana? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kama ilivyo hospitali ya Mkoa wa Geita pia katika vituo vingi vya kutolea huduma kwenye Mkoa wa Geita hakuna nishati ya umeme na hii inasababisha huduma kutolewa lakini pia kupata changamoto hasa kwa akina mama wajawazito wakati wa kujifungua usiku;

Je, Serikali inasemaje kuhakikisha kwamba vituo vya afya vinapatiwa huduma ya umeme maeneo yote katika Mkoa wa Geita? (Makofi)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ni kweli tunakiri kwamba katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita tuna changamoto ya rasilimali watu, watumishi waliokuwepo pale ni takriban asilimia 50 ya watumishi wote ambao wanahitajika. Serikali imeliona hilo na inaendelea kuongeza watumishi kadri vibali vya ajira vinavyopatikana. Sambamba na hilo, tunaendelea kusomesha wataalam mbalimbali kuhakikisha kwamba zile huduma za kibingwa basi zinapatikana katika Mkoa huu wa Geita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameulizia kuhusu suala la umeme katiak vituo vyetu vya kutolea huduma za afya. Wizara ya Afya tumekuwa tunafanya kazi kwa karibu sana na Wizara ya Nishati kupitia mpango wa REA na moja ya mkakati katika mradi huu ni kuhakikisha kwamba vituo vyote vya kutolea huduma za afya na shule vinapata umeme. Kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ya Afya kushirikiana na Wizara ya Nishati kupitia mradi wa REA itahakikisha kwamba maeneo yote ambayo yanapitiwa na mradi wa REA basi nayo yanapata umeme.