Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Vedasto Edgar Ngombale Mwiru

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Kilwa Kaskazini

Primary Question

MHE. VEDASTO E. NGOMBALE aliuliza:- Benki ya Dunia imefadhili miradi ya visima kumi (10) katika kila wilaya nchini:- Je, Serikali imefanya tathmini kujua asilimia ya miradi iliyofanikiwa na ambayo haikufanikiwa; na kwa ile ambayo haikufanikiwa, Serikali haioni haja ya kuingiza fedha ili kukamilisha miradi hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa mradi wa Mingumbi – Miteja ambao umekamilika, Kijiji cha Njia Nne ambacho kimepitiwa na mradi huo hakikupata maji: Je, Serikali sasa iko tayari kusambaza maji kwa Kijiji hiki cha Njia Nne ili kuondokana na tatizo la maji ambalo liko pale?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; mwaka 2017, Wakala wa Serikali (DDCA) ilifanya mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kuchimba visima virefu 21, lakini mpaka sasa wamechimba visima vitatu tu katika vijiji 18. Sasa je, DDCA iko tayari kuchimba visima virefu hivyo, au nini sababu zilizowafanya DDCA wasichimbe visima virefu katika Vijiji vya Nampunga, Chumo, Mtondo wa Kimwaga, Nandembo, Kibata, Kinjumbi, Somanga na Marendego?

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anafahamu nia ya Serikali yetu. Zaidi ya shilingi bilioni 4,668 ziliwekezwa pale katika kuhakikisha tunatekeleza Mradi wa Maji wa Mingumbi na Miteja katika jitihada za kutatua tatizo la maji. Nataka nimhakikishie kwamba nia ya Wizara yetu ni kuhakikisha Watanzania wanapata maji safi na salama. Tutafanya extension ili wa Kijiji kile cha Njia Nne nao waweze kupata maji safi na salama katika kuhakikisha tunamtua mwana mama ndoo kichwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala zima la uchimbaji wa visima, tulitenga kiasi cha shilingi milioni 456 katika kuhakikisha zaidi ya vijiji 19, ikiwa Kilwa Kusini na Kilwa Kaskazini vinapata huduma ya maji. Tuliwapa kazi hiyo DDCA, wamefanya kazi, lakini kulikuwa kuna ucheleweshaji mkubwa. Sisi kama viongozi wa Wizara tumeshamwondoa Mkurugenzi yule wa DDCA maana yake kulikuwa na ucheleweshaji. Yote hii ni kuweka mtendaji ambaye ataendana na kasi ya kuhakikisha tunatatua tatizo la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Ngombale, sisi kama Wizara ya Maji tutahakikisha kwamba visima vilivyobaki vinachimbwa kwa wakati na wananchi wake waweze kupata maji safi na salama.

Name

Selemani Said Bungara

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Kilwa Kusini

Primary Question

MHE. VEDASTO E. NGOMBALE aliuliza:- Benki ya Dunia imefadhili miradi ya visima kumi (10) katika kila wilaya nchini:- Je, Serikali imefanya tathmini kujua asilimia ya miradi iliyofanikiwa na ambayo haikufanikiwa; na kwa ile ambayo haikufanikiwa, Serikali haioni haja ya kuingiza fedha ili kukamilisha miradi hiyo?

Supplementary Question 2

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu hayo kuhusu Wilaya ya Kilwa, lakini Wilaya ya Kilwa kwenye Hospitali ya Wilaya kuna uhaba mkubwa wa maji: Je, Serikali inatuambia nini kuhusu jambo hili la Hospitali ya Wilaya kupata maji ya uhakika na salama?

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, sisi kama Serikali na Mheshimiwa Mbunge anatambua, ni miongoni mwa jitihada ambazo tunazifanya katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji katika Jimbo lake la Kilwa Kusini. Yupo katika mpango wa miji 28, lakini kama unavyotambua, suala la hospitali ni suala la dharura sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikubaliane na Mheshimiwa Bungara tukutane baada ya saa saba ili tuwasiliane na wataalam wetu tuangalie ni namna gani tunaweza tukawapatia wananchi wake huduma haraka katika suala zima la maji.

Name

George Malima Lubeleje

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Primary Question

MHE. VEDASTO E. NGOMBALE aliuliza:- Benki ya Dunia imefadhili miradi ya visima kumi (10) katika kila wilaya nchini:- Je, Serikali imefanya tathmini kujua asilimia ya miradi iliyofanikiwa na ambayo haikufanikiwa; na kwa ile ambayo haikufanikiwa, Serikali haioni haja ya kuingiza fedha ili kukamilisha miradi hiyo?

Supplementary Question 3

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja na nyongeza. Kwa kuwa Serikali ilikuwa na mpango wa kuchimba visima vya maji katika Vijiji vya Ng’hambi, Kiegea, Kazania na Chimaligo; na fedha zilitengwa, visima havijachimbwa? Mheshimiwa Waziri unaweza kuwaeleza wananchi wa vijiji hivyo fedha hizo zilikwenda wapi?

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Mbunge. Kiukweli amekuwa mfuatiliaji mkubwa sana katika suala zima la maji. Ukimwona mtu mzima analia, ujue kuna jambo Mpwapwa. Sasa nataka nimhakikishie, kwanza nipo tayari kwenda Mpwapwa, lakini kuzifuatilia hizi fedha katika kuhakikisha zinafanya kazi na wananchi wake waweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Name

Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. VEDASTO E. NGOMBALE aliuliza:- Benki ya Dunia imefadhili miradi ya visima kumi (10) katika kila wilaya nchini:- Je, Serikali imefanya tathmini kujua asilimia ya miradi iliyofanikiwa na ambayo haikufanikiwa; na kwa ile ambayo haikufanikiwa, Serikali haioni haja ya kuingiza fedha ili kukamilisha miradi hiyo?

Supplementary Question 4

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa utekelezaji wa miradi ya maji unategemea na mpango wa fedha, natambua kuna baadhi ya Wakandarasi bado hawajalipwa fedha zao: Je, ni lini sasa Mkandarasi ambaye anatekeleza mradi wa Mji Mdogo wa Ilula katika Jimbo la Kilolo atapatiwa malipo yake ili wananchi wa Ilula waache kupatiwa migao ya maji mara kwa mara?

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwapigania akina mama na Watanzania hususan katika suala zima la maji. Kikubwa, utekelezaji wa miradi ya maji unategemeana na fedha. Kama unavyoona, gari haliwezi kwenda bila mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tulikuwa tunadaiwa takribani zaidi ya shilingi bilioni 88 na Wakandarasi, lakini tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na Wizara ya Fedha, wametupatia fedha zote shilingi bilioni 88 ambazo tulikuwa tunadaiwa na Wakandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, katika mradi wake ule wa Ilula kwa Mheshimiwa Mwamoto, Kilolo pale, tumeshamlipa zaidi ya shilingi bilioni moja. Tunataka zile fedha tulizomlipa sasa awekeze pale katika kuhakikisha anakamilisha mradi na wananchi wa Ilula waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatolesheleza.