Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Primary Question

MHE. JORAM I. HONGOLI (K.n.y. MHE. PROF. NORMAN A. S. KING) aliuliza:- Ili kuboresha utalii katika Hifadhi ya Kitulo, Serikali iliahidi kupeleka wanyama wasio wakali yaani pundamilia 25, lakini mpaka sasa bado wanyama hao hawajapelekwa licha ya Serikali kuahidi kuwa itatekeleza mwezi Mei na Juni mwaka 2018. (a) Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo? (b) Je, ni lini Serikali itaongeza aina ya wanyama kama vile paa na swala?

Supplementary Question 1

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza nianze kuishukuru sana Serikali kwa hatua iliyochukua kuhakikisha kwamba wanapeleka wanyama hawa pundamilia na swala ili kuongeza utalii katika eneo lile la Kitulo. Hata hivyo, nina swali dogo la nyongeza tu kwamba pamoja na hao ambao wanapeleka kwa kuwa wanyama kama twiga huwa wanaweza wakachangamana na wanyama hawa ambao wametajwa pundamilia na swala. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza wanyama wengine nje ya hawa swala ama twiga ili waweze kuvutia watalii kwa kuwa watalii wengi wanapenda kuona twiga katika eneo lile?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ambalo pia niulize Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba barabara angalau inayoenda kwenye ile mbuga za wanyama ile barabara ya Chimala – Matamba inakuwa katika hali nzuri muda wote ili kuweza kuvutia utalii katika eneo lile? Ahsante sana.

Name

Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Profesa Norman Sigalla, amefanya juhudi kubwa kuhamasisha Wizara kupeleka wanyama kwenye hii Hifadhi na lengo kubwa ni kujaribu kufungua Hifadhi hii ili iweze kuvutia Watalii. Pia nimpongeze kwa kweli kwa kusimama imara kuhakikisha kwamba hili zoezi linakamilika mapema.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba twiga, swala na pala wanaweza kuishi katika mazingira ambayo yanafanana, lakini kabla ya kupeleka wanyama kwenye Hifadhi ya Kitulo, Taasisi yetu ya TAWIRI ilifanya utafiti na kujiridhisha kwamba wanyama hawa wanaweza kuishi katika maeneo hayo na kwamba ikolojia zinafanana. Kwa hiyo ili tuweze kupeleka Twiga nitawaagiza watu wa TAWIRI waweze kufanya utafiti na kuona kwamba wanyama hawa wakipelekwa katika Hifadhi ya Kitulo wanaweza kuishi na hawatakuwa na madhara.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali lake la pili, ni kweli kwamba ili watalii waweze kufika maeneo ya utalii na kwenye maeneo ya Hifadhi, taasisi zetu zimekuwa siku zote zikitengeneza miundombinu kuruhusu watalii kuweza kufika maeneo hayo kirahisi. Maeneo ambayo tunayatengeneza ni yale ambayo kimsingi yako chini ya usimamizi wa Wizara yetu. Kwa hiyo nimhakikishie tu kwamba barabara zote ambazo ziko chini ya usimamizi wetu tutazitengeneza kuhakikisha kwamba tunahamasisha utalii katika Hifadhi ya Kitulo.