Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Amina Saleh Athuman Mollel

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:- Tatizo la kukosekana kwa mafuta yanayosaidia kukinga ngozi dhidi ya mionzi kwa watu wenye Ulemavu wa ngozi hapa nchini limekuwa kubwa na hivyo kuwa chanzo cha magonjwa ya saratani kwa watu hao na kusababisha vifo. Inakadiriwa kuwa asilimia 70 hadi 75 ya vifo vya watu wenye ulemavu wa ngozi vinatokana na saratani. Je, ni lini Serikali itatoa huduma hiyo bure kwa watu wenye ulemavu wa ngozi katika maeneo yote nchini kama inavyotoa dawa za kufubaza virusi kwa watu wenye maambukizi ya UKIMWI?

Supplementary Question 1

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri kutoka kwa Naibu Waziri na vilevile nitambue na kupongeza jitihada za Serikali katika kusaidia makundi maalum hasa watu wenye ulemavu. Pamoja na majibu hayo naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, kweli Serikali imeanza utaratibu huo, lakini usambazaji wa mafuta haya hasa kwa maeneo ya vijijini bado ni tatizo. Albino wengi wanaangamia kutokana na saratani. Napenda tu kufahamu jitihada za Serikali katika kuhakikisha kwamba wanafika vijijini ili kuweza kuwanusuru watoto hawa. Nini mpango mkakati wao kuhakikisha kwamba wanawafikia? Hilo ni swali namba moja.

Swali la pili, albino wengi wanaoishi vijijini, tayari wameshaathirika na ugonjwa wa saratani; na hali za maisha kama tunavyofahamu hasa wa vijijini ni duni sana, kupata shilingi 10,000/= ni shida. Nini mpango mkakati wa Serikali kuwasaidia na kunusuru maisha ya watu wenye albinism hapa nchini?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, utaratibu ambao Serikali tunatumia sasa hivi katika usambazaji wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba ni utaratibu ambao unaitwa pool system. Miaka ya nyuma tulikuwa tunatumia push system. Push system maana yake nini? Ni kwamba sisi Serikali tulikuwa tunanunua dawa, vitendanishi na vifaa tiba tunavipeleka katika vituo vya kutolea huduma ya afya pasipo kuzingatia mahitaji halisi ambayo yako kule. Kwa hiyo, hukuta baadhi ya vifaa, dawa na vitendanishi vinachina kwa sababu uhitaji haukuwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu ambao tunautumia sasa hivi ni wa pool system. Wao kama Vituo vya Afya wanajua mahitaji mbalimbali ya huduma na dawa, vitendanishi na vifaa tiba na wao kuingiza katika mipango yao na kuagiza kutoka MSD. Kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, dawa hizi na mafuta haya kwa ajili ya kundi hili la walemavu wa ngozi tunavyo ndani ya MSD, ni wajibu sasa wa Halmashauri mbalimbali na hospitali za mikoa kuziagiza kulingana na mahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, Mheshimiwa Amina amegusia suala la walemavu wa ngozi kwamba wamekuwa wanaathirika na ugonjwa wa kansa. Hili ni kweli, tunakiri. Ni kwa sababu jua hili ambalo ni mionzi yetu ya jua lina ultraviolet rays ambazo zinaathiri ngozi za wenzetu hawa ambao wana ulemavu wa ngozi kwa kiasi kikubwa kulinganisha na wengine ambao wasiokuwa walemavu wa ngozi na tunaendelea kutoa elimu kuhakikisha kwamba wenzetu ambao wana ulemavu wa ngozi wanajikinga dhidi ya miale ya jua kwa kuvaa kofia na nguo ambazo zinakinga sehemu kubwa ya miili yao, lakini vilevile kutumia mafuta ambayo yanawakinga dhidi ya hii miale ya jua.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, huduma za matibabu ya kansa ni bure ndani ya nchi yetu. Nami nawaomba sana, mtu yoyote ambaye anaona kuna mabadiliko katika ngozi yake, basi aweze kufika katika vituo vya kutolea huduma ya afya aweze kupata huduma kwa haraka.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA IKUPA ALEX): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuongezea kidogo kwenye majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya pamoja na majibu yake mazuri; ni kwamba naomba tu niendelee kutoa msisitizo kwamba Wakurugenzi katika Halmashauri mbalimbali wajitahidi kwamba wanakuwa na idadi kamili ya haya mahitaji kwa maana ya watu wenye mahitaji, watu wenye ualbino. Kwa sababu wasipokuwa na orodha kamili ya mahitaji, inakuwa ni ngumu upatikanaji wa hizi dawa kutoka MSD. Hili limekuwa ni tatizo ambalo katika ziara ambazo nimewahi kuzifanya imeonekana kwamba mahitaji haya hayapatikani kulingana na uhalisia wa watu waliopo. Ahsante.