Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Primary Question

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA (K.n.y MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED) aliuliza:- Kumekuwa na tatizo la kuvuja kwa mitihani ya Taifa hapa nchini hususani ile ya kidato cha nne (CSEE) hali inayoondoa ufanisi hasa ikizingatiwa matokeo yanayotoka yamejaa udanganyifu. Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti tatizo hili?

Supplementary Question 1

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, umekuwa ni utaratibu wakati wa mtihani wa kidato cha nne Serikali inapeleka askari tena askari wenye silaha kwenda kuwasimamia watoto wakati wanafanya mtihani. Kitendo hiki kinawatia uoga wanafunzi kwa sababu hawajazoea kusimamiwa na askari wakati wakifanya mitihani au wakati wanajisomea, hivyo wanapoteza concentration katika mitihani na hii inawapeleka wengine kufeli.
Je, Serikali haina njia mbadala ya kuhakikisha kunakuwa na ulinzi lakini usiotisha kama vile kuweka askari ambao hawana uniform na hawana silaha ili waweze kuwasimamia watoto hawa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, tunaaminishwa kwamba mtihani wa mwisho sio pekee ndiyo unaomfanya mtoto afaulu katika mitihani yake ya kumaliza kidato cha nne, kwamba continuous assessment inachukua asilimia 50 na mitihani ya mwisho inachukua asilimia 50, kama hili ni kweli kuna sababu gani ya kuweka ulinzi mkubwa wakati wa mtihani wa mwisho wakati ule unachangia tu asilimia 50? Je, ulinzi huo pia unawekwa kwenye zile continuous assessment ili kufanya usawa? (Makofi)

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kimsingi tunapoweka ulinzi lengo si kuwatisha watahiniwa bali kuhakikisha kwamba mazingira hayo yanakuwa salama kabisa. Kama ambavyo imeshuhudiwa katika siku za karibuni, hali ya uhatarishi imekuwa ikijitokeza katika aina tofauti tofauti. Kwa kweli siamini kama wanafunzi wa Kitanzania wanaweza wakamuogopa askari kwa sababu ni maisha yao ya siku zote, hawezi akawa hamuoni kabisa askari, karibu kila mahali nchi hii imeimarisha ulinzi na askari kama polisi tuko nao siku zote tena kuna ulinzi jumuishi na shirikishi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa misingi hiyo mimi nadhani kwamba lengo la muhimu lieleweke kwamba ni kuhakikisha kwamba tunaweka mazingira salama kabisa ambayo wanafunzi wale badala ya kuogopa askari kwao ni suala la usalama ili wafanye mitihani yao bila kupata uhatarishi wa aina yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kupimwa kwa kufuata matokeo endelevu (continuous assessment), ni kweli tumekuwa tukifanya hivyo na hiyo haiwezi kuwa ndio sababu ya kusema kwamba kwa sababu marks tunazozitegemea mwishoni ni asilimia 50 tu, basi tusiwawekee mazingira ya usalama. Tutaendelea kufanya hivyo, na kwa sababu umetoa hoja hiyo, tutafanyia kazi kama tukiona kweli mwanafunzi anaogopa sana askari tutajua namna bora zaidi ya kufanya.

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Primary Question

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA (K.n.y MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED) aliuliza:- Kumekuwa na tatizo la kuvuja kwa mitihani ya Taifa hapa nchini hususani ile ya kidato cha nne (CSEE) hali inayoondoa ufanisi hasa ikizingatiwa matokeo yanayotoka yamejaa udanganyifu. Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti tatizo hili?

Supplementary Question 2

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naomba niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, mitihani ya kidato cha nne tunajua inatumika kwa lugha gani lakini kuna mitihani ya darasa la saba ambapo mitihani hii inatungwa maswali ya kuchagua yote. Sasa nilikuwa naomba niiulize Serikali ni lini mtaanza kutunga mitihani ambayo si ya kuchagua, hasa katika masomo ya hesabu ili watoto wetu wapimwe uelewa badala ya kuchagua na wengine wanabahatisha kufaulu kwenda sekondari? Swali langu ni hilo.

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na mtazamo wa wadau tofauti tofauti katika maswali ya kuchagua hasa katika mitihani ya hisabati. Serikali nasi pia tumekuwa tunaliangalia hilo japo katika utafiti uliofanyika ilionesha kwamba kuchagua peke yake hakumwezeshi mtu kufaulu isipokuwa lazima kwanza awe ana msingi wa kujua swali analolifanyia uchaguzi.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kwa siku za nyuma hasa kipindi chetu sisi, ni kwamba hata kama unakuwa na mtihani wa kuchagua ilikuwa bado unakuwa na sehemu ya kufanyia kazi ambayo na yenyewe inakuwa ni sehemu ya kuiangalia. Kwa hiyo, tutaona namna gani tuweze kufanya hivyo ili yule anayekuwa amechagua tuweze pia kupata uthibitisho isiwe tu kwamba swali la mwisho ndio jibu la kuliangalia, lakini ni suala ambalo linafanyiwa kazi. (Makofi)

Name

Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Primary Question

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA (K.n.y MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED) aliuliza:- Kumekuwa na tatizo la kuvuja kwa mitihani ya Taifa hapa nchini hususani ile ya kidato cha nne (CSEE) hali inayoondoa ufanisi hasa ikizingatiwa matokeo yanayotoka yamejaa udanganyifu. Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti tatizo hili?

Supplementary Question 3

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Mheshimiwa Spika, lengo la nne la maendeleo endelevu ya dunia ni elimu bora, sawa, shirikishi kwa wote. Suala la mitihani na udanganyifu ni mchakato mdogo to end product. Sasa Serikali ina weka lini au itaanzisha lini chombo cha kudumu cha kuangalia mchakato mzima wa elimu yaani ubora wa elimu, kuwekeza kwenye miundombinu ya elimu kwa walimu, ukaguzi, vyote yaani quality assurance itaanzishwa lini chombo hiki ili elimu yetu, mitihani iwe ni sehemu ndogo tu kama ilivyo nchi ya Finland ambapo asilimia kumi tu ndiyo ile mitihani lakini mchakato mwingine wote wa kumuandaa mtoto unakuwa umeandaliwa na umesiamamiwa na chombo chenye mamlaka na kinachojitegemea? (Makofi)

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, wizara imeliona hilo. Ni kwamba kwa sasa hivi kwanza tunaiangalia upya Sheria yetu ya Elimu kwa sababu ni ya muda mrefu na kuna mambo mengi yamejitokeza na hiyo tungependa iendane na uhalisia. Vilevile tunataka kuangalia mfumo mzima wa namna ya ukaguzi. Kwa mfano mwanzo tulikuwa na ukaguzi katika sehemu za kanda na kwenye Halmashauri/kwenye Wilaya zetu lakini sasa hivi baada ya kuongeza shule nyingi, inaonesha kwamba sasa kanda peke yake si sehemu sahihi badala yake tungeweza kuangalia mfumo mzima na tukauboresha zaidi. Hii ni kwa sababu sasa shule za Serikali kwa mfano za sekondari zimeshaongezeka sana.
Mheshimiwa Spika, vilevile tunaona kwamba haitoshi tu kuangalia shule ina walimu wangapi, madarasa mangapi na vyoo vingapi, tunataka tuangalie mfumo mzima, na hivyo wizara sasa hivi inaandaa Mfumo wa Uthibiti na Tathmini kwa ujumla (National Schools Assurance Framework) ambayo itawezesha sasa hata kama unafanyika ukaguzi unakuwa tayari una mwongozo unaokwambia ni nini unatakiwa ufuatilie. Vilevile hata kushirikisha kamati za shule pamoja na walimu na wananchi wenyewe kwa ujumla katika kudhibiti ubora wa elimu Tanzania. (Makofi)