Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

George Malima Lubeleje

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Primary Question

MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaamua kurudisha fedha zilizokusanywa na Halmashauri kupitia vyanzo vyake vya ndani ili ziweze kutekeleza majukumu yake na mikakati iliyopangwa kwa ufanisi?

Supplementary Question 1

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mwaka 1998/1999, mimi nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Katiba ya Sheria na Utawala, Serikali iliamua TRA ijaribu kukusanya kodi ya majengo na walianzia na Halmashauri za Manispaa tatu za Ilala, Temeke na Kinondoni. Baadaye walishindwa, Serikali ikarudisha tena kodi hizo zikusanywe na Manispaa hizo. Sasa ni sababu gani za msingi tena Serikali imeamua kodi ya majengo ikusanywe na TRA na siyo Halmashauri zenyewe? (Makofi)

Name

Dr. Philip Isdor Mpango

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Sababu ya msingi kwa nini Serikali ilifanya maamuzi kwamba sasa kodi hii ianze kukusanywa na Mamlaka ya Mapato, kwanza, niseme Mamlaka ya Mapato kazi yake ni kukusanya mapato yote wala siyo ya kodi peke yake.
Pili, tuliona udhaifu mkubwa katika ukusanyaji wa mapato katika ngazi ile na ndiyo maana lengo la Serikali ni kusema tutumie chombo ambacho kina wataalam waliobobea kwa ajili ya kukusanya mapato haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili la kusema huko nyuma walishindwa kwani ukishindwa maana yake ndiyo basi tena. Mzee wangu Mheshimiwa Lubeleje tumepata uzoefu, tumejifunza kutokana na uzoefu, tumefanya maandalizi ya kutosha na tuna hakika awamu hii tutaikusanya kodi hii ipasavyo. (Makofi)

Name

Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaamua kurudisha fedha zilizokusanywa na Halmashauri kupitia vyanzo vyake vya ndani ili ziweze kutekeleza majukumu yake na mikakati iliyopangwa kwa ufanisi?

Supplementary Question 2

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali ndogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imechukua mfumo wa kodi ya majengo kukusanywa na TRA, lakini kumekuwa na sintofahamu kubwa kwa wananchi wetu kwamba ni majengo yapi hasa ambayo yanatakiwa kulipiwa kodi katika Halmashauri zetu maana hata nyumba za tembe na udongo nazo zinachangiwa kodi. Nini kauli ya Serikali kuhusiana na jambo hili?

Name

George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli mwaka 2015 kupitia Sheria ya Fedha tulifanya marekebisho ya sheria na katika kifungu cha 25(2)(b) tulieleza kwamba chanzo hiki badala ya kuwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa za Mijini kiende hata kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa zilizo Vijijini yaani District Councils. Hata hivyo, tafsiri ya mabadiliko haya haijatafsiriwa vizuri na mamlaka zenyewe kwa sababu mazingara haya yalikuwa ni mahsusi kwa maeneo kama yafuatayo; kwa mfano, Ngurdoto pamoja na establishment yote kubwa ya hoteli, facilities na kumbi za mikutano unaikuta iko vijijini, huwezi ukaacha kukusanya pale property rate au Bagamoyo yako maeneo mengi sana ya hoteli ambazo zipo vijijini, yalikuwa ni maeneo maalum kama hayo.
Mheshimiwa Spika, ili uweze kukusanya chanzo hicho ni lazima itugwe Sheria Ndogo kutoka kwenye Halmashauri husika na sheria hiyo inatungwa Waheshimiwa Wabunge mkiwa wajumbe. Unakuta inatungwa Sheria ya Ndogo ambayo kabisa inakiuka tafsiri nzuri ya sheria iliyotungwa na Bunge.
Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kueleza tu kwamba tafsiri ya kwamba ukusanyaji wa property rate sasa unakwenda mpaka kwenye vijiji kwenye nyumba za tope na udongo si sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, usahihi ni kwamba kwa mazingira maalum ya uwekezaji ambayo uko vijijini lakini unauona ni uwekezaji wa kimjini huko ndiko zinatakiwa kukusanywa. Si kwa nyumba ya mwananchi wa kawaida ambayo haiingizi kipato chochote, hajapangisha mtu yeyote, yeye anaishi tu, hatujafikia hatua hiyo kama nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nichukue nafasi hii kuziagiza Mamlaka zote za Serikali za Mitaa ambazo zinafanya hivyo kukusanya kutoka kwenye nyumba za tope, nyumba za bati au nyumba zozote lakini ambazo haziingizi mapato, si za kibiashara na ziko vijijini, hapana, haitakiwi kukusanya na Serikali ya CCM haijaamua uamuzi huo bado. (Makofi)

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Kwanza nilitaka niongezee tu kwamba kwa mwaka huu ambao tunamalizia, TRA ilikusanya kodi ya majengo kwa Halmashauri 30 tu, Halmashauri nyingine zilitakiwa kuendelea na utaratibu wa kawaida wa kukusanya mapato hayo yanayotokana na kodi ya majengo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nisisitize nchi yetu hii ili tuende ni lazima tuendelee kujenga utaratibu wa wananchi wetu kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa. Nitatoa ufafanuzi mchana kuhusu kodi hii ya majengo na nimwombe sana Mheshimiwa Cecilia Paresso avumilie tu kidogo mpaka ile hotuba itakayowasilisha Bajeti Kuu ya Serikali mchana tutafafanua zaidi kuhusu kodi hii. Ahsante. (Makofi)

Name

Maida Hamad Abdallah

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaamua kurudisha fedha zilizokusanywa na Halmashauri kupitia vyanzo vyake vya ndani ili ziweze kutekeleza majukumu yake na mikakati iliyopangwa kwa ufanisi?

Supplementary Question 3

MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kama alivyokwishasema Mheshimiwa Waziri kwamba mapato ya Halmashauri ndiyo vyanzo vikuu vinavyoendeleza maendeleo katika Halmashauri. Kwa kuwa makusanyo yanayotokana na mapato na kodi ya ardhi na majengo urejeshaji wake kutoka katika mamlaka husika umekuwa ukisuasua huku Halmashauri zikiwa zimejipangia majukumu mbalimbali na hivyo utekelezaji wake kuchelewa. Je, Serikali haioni kwamba mtindo huu unaathiri utekelezaji wa haraka wa vipaumbele ilivyojipangia Halmashauri? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa ndani ya Halmashauri zetu kwa mujibu wa sheria wametakiwa kutekeleza agizo la kuwawezesha wanawake na vijana kwa kutenga asilimia 10 ili ziwaendeleze kiuchumi. Kwa kuwa changamoto hii imekuwa ikiathiri sana agizo hili, je, Serikali sasa ipo tayari kuleta waraka Bungeni wa mapendekezo ya kwamba mapato yanatokana na kodi za ardhi na majengo baada ya makusanyo zibaki kwenye Halmashauri husika? (Makofi)

Name

George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kodi za ardhi na majengo zinakusanywa kwa sehemu, kwa mfano, kodi ya ardhi inakusanywa na kupelekwa Wizara ya Ardhi na baadaye kupelekwa Hazina na hupaswa kurejeshwa kwenye Halmashauri zetu asilimia 30. Urejeshaji huu haujawa mzuri kwa muda sasa, lakini katika bajeti ya mwaka huu tunaokwenda nao katika makusanyo yaliyopelekwa karibu shilingi bilioni 29 angalau kiasi cha shilingi bilioni 4.6 kimerejeshwa, kwa hiyo, utaona tunafanya hivyo.
Hata hivyo, wakati wa hotuba yangu ya bajeti nilisema tunajaribu kuangalia na kupitia sheria hizi ili tuweze ku-harmonize ili fedha ambazo zinakusanywa zirejeshwe kwa utaratibu mzuri zaidi. Kwa hiyo, nachotaka kuahidi tu ni kwamba kwa kodi hizi zote mbili, ya ardhi na majengo, Waziri wa Fedha atakaposoma Sheria ya Fedha kwa mwaka 2017/2018 kutakuwa kuna mabadiliko ambayo yatazingatia maoni mengi ambayo yametolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati nawasilisha bajeti yangu lakini katika mazungumzo mbalimbali kupitia maswali ya Wahemishiwa Wabunge.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na asilimia kumi ambayo inatolewa kama mikopo kwa vijana na akina mama, tutajaribu kuangalia kama tunaweza tukaanzisha sheria mahsusi kwa ajili ya jambo hili kwa sababu kwa sasa lilikuwa limewekwa kisera tu lakini hakukuwa na sheria inayo- enforce. Hata hivyo na lenyewe tumeliweka katika utaratibu endapo tutapata fursa ya kuleta mabadiliko ya sheria mbalimbali basi tutaliweka na maandalizi yake sisi kama Wizara tayari tumekwishayafanya.