Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Mary Machuche Mwanjelwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mbeya Mjini

Primary Question

MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA (K.n.y MHE. ORAN NJEZA) aliuliza:- Wananchi wa Jimbo la Mbeya Vijijini wanaipongeza Serikali kwa kuanzisha Wilaya ya Kipolisi Mbalizi. • Je, ni lini Ofisi ya Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi itajengwa zikiwemo nyumba za kuishi askari? • Je, Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi ina magari mangapi na Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya vituo vya polisi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasimama kwa niaba ya Mheshimiwa Oran ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mbeya kijiografia imekaa vibaya sana, vituo vingi zaidi hasa katika Kata ya Igoma Tarafa ya Tembela pamoja na kule Isangati hakuna vituo vya polisi kabisa na jiografia yake kama nilivyosema ni mbaya. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alikuwa ameahidi kabisa kwamba vituo hivi vijengwe, lakini mpaka leo hakuna. Nataka kujua majibu ya Serikali ni lini itajenga Vituo vya Polisi huko Igoma pamoja na Ilembo katika Tarafa ya Isangati?
Swali la pili, Wabunge wa Mkoa wa Mbeya wote kwa pamoja tunachanga kwa juhudi zetu na wananchi kujenga Kituo cha Polisi cha Mbalizi. Ninataka kujua ni nini mkakati wa Serikali katika kuongeza nguvu katika kituo hiki cha Polisi Mbalizi? Ahsante.

Name

Eng. Edwin Amandus Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mary Mwanjelwa, Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo hili na Wabunge wa Mkoa wa Mbeya ambao wameshirikiana katika kujenga kituo hiki. Binafsi nilikwenda pale kuzindua ujenzi huo na sisi vilevile tulichangia, lakini niwapongeze pia, wananchi wa Mbeya kwa kuweza kujitolea kukijenga kituo hiki katika hatua ambayo sehemu iliyofikia ni karibu asilimia 50 ya ujenzi imekamilika na huu ni mfano wa kuigwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, changamoto ambayo ameizungumza katika maeneo mengine ya Isangati, nitoe changamoto kwamba wakiendelea na jitihada kama hizi itasaidia kuharakisha ukamilishaji wa ujenzi wa vituo katika maeneo mengine kwa haraka ili kusaidia kukamilisha dhamira njema ya Serikali ya kukamilisha ujenzi wa vituo 65 nchi nzima vyenye mapungufu katika maeneo mbalimbali nchini.