Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Raphael Masunga Chegeni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Primary Question

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:- Mafao ya wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Mashirika mengi ya Hifadhi ya Jamii yamekuwa na utata kuhusu fao la kujitoa. Je, Serikali inatoa tamko gani ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuunganisha mifuko hiyo na kuondoa mkanganyiko kwa wanachama?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo yamejikita katika kuelezea uhalisia wa mifuko hii na changamoto zilizopo, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwanza, kwa vile inaonekana wazi kwamba watumishi wengi na hasa wanachama wa mifuko hii wanapokuwa wameachishwa kazi au wametorokwa na waajiri wao wanahangaika sana kuweza kujikimu katika maisha yao na hiyo sio hiari yao isipokuwa wameachishwa kazi au wametorokwa na waajiri. Sasa Serikali haioni kwamba kuna haja hawa watu ambao wanapata dhahama hii, wasaidiwe kuchukua mafao yao ili wajikimu katika maisha yao wakati wakitafuta kazi zingine za kuweza kujipatia kipato?
Swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kabisa kwamba mifuko hii ina changamoto nyingi sana, ikiwa ni pamoja na gharama za uendeshaji ambayo inakula mifuko ya wanachama hawa, lakini pili kutokana na kwamba mifuko hii imekuwa mingi mno na utitiri ambao mafao yao hata hayana tija kwa wanachama wenyewe.
Je, ni lini sasa Serikali, kufuatia kauli ya Mheshimiwa Rais siku ya sherehe ya Mei Mosi Moshi katika Mkoa wa Kilimanjaro alipotaka Serikali ilete hoja hapa Bungeni, Muswada wa kuweza kuigawa mifuko hii kutoka utiriri huu na kubakiwa na angalau mifuko miwili tu ambayo itakuwa na sekta ya umma au na sekta binafsi?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba ni lini Serikali itatii maagizo ya Mheshimiwa Rais kwa kuleta Muswada hapa Bungeni ili tuweze kurekebisha suala la mifuko hii? (Makofi)

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza naomba tu nirudie majibu yangu ya msingi ya kwamba katika kuliangalia suala hili la fao la kujitoa kama lilivyokuwa linaitwa, sisi kama Serikali na kupitia maazimio ya Bunge hili mwaka 2012 ambayo ilisema Serikali iangalie utaratibu mzuri wa kushughulika na suala hili la fao la kujitoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kama nilivyosema tayari tumekwishaanza maandalizi ya kuja na utaratibu mwingine mbadala ambao utamfanya mfanyakazi wa Kitanzania yule ambaye ataachishwa kazi na hajafikisha umri huo wa miaka 60 wa kuchukua mafao yake, tuone namna ya kuweza kuliweka sawa na kumsaidia asipate shida katika muda huu wote wakati bado anasubiria kupata ajira nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo kwa sababu jambo hili linakuja Bungeni, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge avute subira. Muda sio mrefu tutawasilisha mapendekezo yetu hayo na ninyi kama Wabunge mtapata nafasi za kuweza kuchangia na kutushauri vema sisi kama Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lke la pili; ni lini tutatii maagizo ya Mheshimiwa Rais ya kuunganisha mifuko hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba sisi baada ya tamko la Mheshimiwa Rais kazi hiyo imefanyika mara moja na katika majibu yangu ya msingi nimesema tayari tumeshakutana na wadau, tumezungumza namna bora ya kuunganisha mifuko hii na muda sio mrefu tutatoa pia taarifa sehemi ambayo tumefikia na tutawapa pia the way forward ya namna ambavyo mifuko hii itakuwa. Hivyo Mheshimiwa Mbunge vuta subira tu, hii yote iko katika mipango na agizo la Mheshimiwa Rais tumelitii na tumelitekeleza. (Makofi)

Name

Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Primary Question

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:- Mafao ya wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Mashirika mengi ya Hifadhi ya Jamii yamekuwa na utata kuhusu fao la kujitoa. Je, Serikali inatoa tamko gani ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuunganisha mifuko hiyo na kuondoa mkanganyiko kwa wanachama?

Supplementary Question 2

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Badala ya kuwa na fao la kupoteza ajira, kwa nini Serikali isilete sheria na kuibadilisha katika mafao ya mtu apewe angalau theluthi moja ya mafao yake baada ya kuwa amepoteza ajira?

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirejee tu maneno yangu ambayo nimeyasema pale awali katika jibu la msingi ya kwamba Serikali tutaleta mapendekezo yetu na Bunge hili litakuwa na nafasi ya kuweza kutushauri vema. Mimi nafikiri katika hali hii ambayo tumefikia hivi sasa, Waheshimiwa Wabunge mtuvumilie na msubiri muone mapendekezo ya Serikali na baada ya hapo mtatushauri tuone namna bora ya kuweza kulifanya jambo hili tuondoe matatizo kwa wafanyakazi wetu. (Makofi)

Name

Kasuku Samson Bilago

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Buyungu

Primary Question

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:- Mafao ya wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Mashirika mengi ya Hifadhi ya Jamii yamekuwa na utata kuhusu fao la kujitoa. Je, Serikali inatoa tamko gani ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuunganisha mifuko hiyo na kuondoa mkanganyiko kwa wanachama?

Supplementary Question 3

MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili mfanyakazi aliyemaliza kazi kwa kustaafu au kupoteza kazi aweze kulipwa mafao yake katika mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ni pamoja na kupata barua yake ya mwisho. Wafanyakazi waliopatikana na vyeti fake hawajapata mafao yao kutoka kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa sababu hawana barua za kumaliza huo ufanyakazi fake.
Je, Serikali iko tayari kuwapa barua zao ili wakahangaike kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii?

Name

Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na majibu fasaha na huo ndiyo utaratibu wa Serikali katika kushughulikia yale ya awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jibu la Mheshimiwa Bilago, swali hili la mafao ya watumishi ambao wameonekana kwamba ni watumishi wenye vyeti fake na ambao wamepatikana na masuala kadha wa kadha katika utumishi wao, limekuwa likijibiwa na Serikali mara kadhaa ndani ya Bunge lako Tukufu na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma. Ninaomba Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine wote waendelee kuvuta subira, yale ambayo yamekuwa yakijibiwa na Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma hayo ndiyo ambayo yatakuja kutekelezwa baada ya Serikali kufikia maamuzi yale ambayo Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma amekuwa akieleza humu ndani ya Bunge lako Tukufu kila siku.