Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Primary Question

MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:- Jimbo la Ukonga lina shida kubwa ya umeme katika Kata zifuatazo; Kata ya Chanika (Ngwale, Nguvu Mpya, Virobo, Kidugalo, Yongwe, Lukooni, Vikongoro na Tungini); Kata ya Zingiziwa (Zogoali, Zingiziwa, Ngasa, Ngobedi, Somelo na Gogo, Lubakaya na Kimwani); Kata ya Majohe (KIvule na Viwege); Kata ya Buyuni (Zavala, Buyuni, Mgeule Juu, Nyeburu, Mgeule Chini, Kigezi, Kigezi Chini na Taliani); Kata ya Pugu Station (Bangulo, Pugu Station na Kichangani); Msongola (Yangeyange, Mbondole, Kidle, Mkera, Sangara, Kiboga, Uwanja wa Nyani, Kitonga, Mvuleni na Mvuti) na Kata ya Kivule (Bombambili). Maeneo hayo yote yanahudumiwa na Wilaya ya Kisarawe kama maeneo ya vijijini. Je, ni lini maeneo hayo yatapata umeme wa REA?

Supplementary Question 1

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwanza naomba niseme tu kwamba nashukuru kwa ushirikiano ambao naupata kutoka pale TANESCO, Gongolamboto, Kisarawe na Mheshimiwa Naibu Waziri nikimpigia simu anapokea, siyo kama wengine walivyosema hapa.
Mheshimiwa Spika, pia naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Jimbo la Ukonga lina shida kubwa ya umeme, lakini pia kuna shida nyingine zimeongezeka, Ukonga kuna wajasiriamali wadogo wenye viwanda vidogo vya kusaga unga wa sembe na dona, lakini pia na chakula cha kuku; umeme unakatika sana katika eneo hilo. Kwa hiyo, naomba kama kuna utaratibu wa dharura, ufanyike ili kuzuia hiyo kero kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, eneo la Kitonga Sekondari, Mvuti Sekondari, Mbondole Sekondari, Bombambili Shule ya Msingi na Shule ya Msingi Nzasa II kuna visima vya maji havifanyi kazi kwa sababu kuna shida kubwa ya umeme katika eneo hilo.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza akawa na mkakati mahususi wa kuondoa kero katika maeneo haya ambayo ni maeneo muhimu kwa walimu, wanafunzi na jamii inayozunguka eneo hili? Ahsante.

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa na mimi namshukuru Mheshimiwa Mbunge anavyofuatilia masuala ya wananchi wake wa Ukonga. Niseme tu, katika swali la kwanza kuhusu kukatika kwa umeme; katika maeneo ya Kisarawe hivi sasa tulikuwa tunajenga miundombinu ya kusafirisha umeme kutoka Gongolamboto na Kipawa ili wananchi wengi wafikiwe na umeme unaojitosheleza. Ujenzi wa utaratibu huo unaendelea na unakamilika mwezi wa Oktoba tarehe 22.
Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Waitara kwamba mara baada ya kukamilika, tatizo la kukatika kwa umeme kwa maeneo ya Kisarawe, Gongolamboto, Mvuti pamoja na Chanika yatakwisha mara moja.
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Ukonga yapo maeneo ambayo yanapata umeme kutoka eneo la Kisarawe na kwa maana hiyo yanahesabika kama yapo vijijini. Maeneo hayo ni pamoja na kama ambayo ametaja Mheshimiwa Waitara, ni Kitonga lakini yapo maeneo ya Namanga, Bombambili pamoja na Uwanja wa Nyani, yote hayo yanapata umeme kutoka Kisarawe. Kwa maana hiyo, visima vilivyopo katika maeneo hayo, yataunganishwa sasa na umeme wa Mradi wa REA ambao unakuja sasa ili wananchi waweze kupata maji kwa urahisi.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwa niaba ya wananchi wote kwamba Mradi wa REA Awamu ya Tatu, pamoja na kupeleka umeme kwenye vitongoji na vijiji, utaunganisha pia miundombinu ya maji kote nchini.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waitara maeneo ya Kitonga, Uwanja wa Nyani, Msongole, Mvuti na Vijiji vingine ambavyo vina visima vitaunganishwa na mradi huu wa REA.