Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Anna Joram Gidarya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ANNA J. GIDARYA aliuliza:- Mkoa wa Manyara ni mojawapo ya mikoa inayoongoza kwa ukeketaji wa watoto wa kike; takwimu za mwaka 2017 zinaonesha kuwa Mkoa wa Manyara unaongoza Kitaifa. (a) Je, Serikali ina mpango gani madhubuti wa kukomesha ukatili huo wa kijinsia pamoja na kutoa semina elekezi kuhusu madhara yatokanayo na ukeketaji wa mtoto wa kike hususan Wilaya ya Hanang, Simanjiro, Kiteto na Mbulu? (b) Kwa kuwa, Ngariba sasa wanatumia mbinu mbadala za kuwakeketa watoto wa kike wa kuanzia miezi sita (6) hadi mwaka mmoja na miezi sita. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwakamata Ngariba wote wanaofanya ukatili huo na kuwachukulia hatua za kinidhamu, hatua za kibinadamu ili wawe sehemu na fundisho la kukomesha ukatili huo?

Supplementary Question 1

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo. Kwanza, Mheshimiwa Waziri kwenye majibu yake amesema wameunda madawati 516, pamoja na madawati haya ni idadi ya watoto wangapi waliokufa kwa kukeketwa?
Pili; Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na takwimu zinazoonesha 2016/2017, ni hatua zipi na ni watuhumiwa wangapi ambao wamechukuliwa hatua za kisheria. (Makofi)

Name

Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya kwanza, kuhusu takwimu za watoto waliokeketwa, mpaka sasa hatuna takwimu halisi za watoto ambao wamekeketwa, kwa sababu kwa kiasi kikubwa vitendo hivi vinafanyika katika zama hizi katika mazingira ya usiri mkubwa kwa sababu Serikali imetoa jicho lake kila kona kwamba vitendo hivi toka tumevi-criminalize kwenye Sheria ya Mtoto mwaka 2006. Mpaka sasa tumekuwa wakali, tumeanzisha hayo madawati, tumetoa mafunzo kwa Polisi na kwa kiasi kikubwa kila mtu sasa amekuwa aware kwamba hili ni tatizo na sio mila tu ambayo tunairuhusu katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, vitendo hivi sasa vimehamishwa kutoka utaratibu wa kizamani wa kimila ambapo vilikuwa vinafanyika wazi na kwa sherehe na sasa vinafanyika katika taratibu za usiri. Kwa hivyo imekuwa ngumu kwa kweli kuweza kutengeneza takwimu halisi za namba ya watoto ambao wamekeketwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ni watu wangapi ambao wamewahi kukamatwa kwa vitendo vya ukeketaji. Mpaka sasa pia sina takwimu halisi mahsusi hasa za kuhusu wakeketaji, kwamba wangapi wamewahi kushtakiwa na wangapi wamewahi kuhukumiwa. Kwa sababu pia toka tumetunga hiyo sheria kama nilivyosema awali hata wale Mangariba ambao walikuwa ni mashuhuri kwa kukeketa nao pia hawakeketi waziwazi na hawakubali pia kukeketa kwa sababu wanajua ni kinyume cha sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tumeona kwa sababu bado vitendo vinaendelea kwa njia za kichini chini ni vema tukatumia njia mbadala za kufanya kazi na Mangariba kwa kuwaelimisha, kuwajengea uwezo lakini pia kuwapa tahadhari kwamba kitendo hiki ni kosa la jinai na kwamba akikutwa anafanya kitendo hicho, yeye, wazazi wa mtoto, ndugu wa mtoto na watu wote ambao wamesherehekea kitendo hiki kifanyike, wanachukuliwa hatua kali za kisheria. Kwa hivyo, hata Mangariba nao wamekuwa wanasita kushiriki kufanya vitendo vya ukeketaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, tumeanza mradi wa kufanya njia mbadala ya kufanya graduation ya watoto kwenda kwenye ujana ambayo inajulikana kama Alternative Rights of Passage (ARP) ambapo tunatumia sasa Viongozi wa Kimila zaidi, hao Mangariba pamoja na Viongozi wa Kimila kama Malaigwanan, Machifu na Watemi kwenye maeneo mbalimbali ili kuwaelimisha kuhusu jambo hili na kuwaambia kwamba mtoto anaweza akahitimu kutoka kwenye utoto kwenda kwenye utu uzima bila kukatwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa msingi huo, anapata mafunzo yote ambayo yanahusu mambo ya kiutu uzima kwa sababu sasa anakua bila kukatwa na tunapata mafanikio makubwa na ndio maana vitendo hivi vimepungua kwa kiasi kikubwa.