Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hawa Abdulrahiman Ghasia

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Primary Question

MHE. HAWA A. GHASIA (K.n.y. MHE. AMINA N. MAKILAGI) aliuliza:- Je, Serikali ina mikakati gani ya kupima ardhi yote ya Tanzania na kuipangia matumizi yaliyo bora kufuatia kuwepo kwa tatizo kubwa la migogoro ya ardhi kati ya wakulima, wafugaji na Mamlaka ya Hifadhi?

Supplementary Question 1

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa tatizo hili la migogoro baina ya wakulima na wafugaji siyo la Mkoa wa Morogoro peke yake, tumelishuhudia katika Mkoa wa Pwani na Mkoa wa Lindi, sasa kwa nini Wilaya zote tatu za majaribio zimekuwa katika mkoa mmoja? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, je, Mkoa wa Pwani na Lindi
zoezi hilo litafanyika lini ili kuondoa changamoto ya wakulima na wafugaji hasa katika Wilaya za Rufiji, Kilwa na yale maeneo ambayo wafugaji wapo kwa wingi? (Makofi)

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwanza napokea pongezi zake ambazo ametoa na mimi nashukuru, ni kutokana na ushirikiano wetu sote. Katika maswali yake mawili aliyozungumza; la kwanza, amesema tatizo la migogoro lipo katika mikoa mingi nchini na kwa nini tumeamua kuanzia Mkoa wa Morogoro peke yake na Wilaya zote tatu za mfano zipo Mkoa wa Morogoro?
Mheshimiwa Spika, napenda nilithibitishie Bunge lako hili, nadhani wote ni mashahidi kwamba katika ile migogoro ya wakulima na wafugaji kwa Mkoa wa Morogoro ilikuwa ni kama imekithiri.
Mheshimiwa Spika, mauaji mengi yalikuwa yanatokea kule na kila leo kulikuwa na changamoto za hapa na pale na ndiyo maana tukasema sasa kwa sababu maeneo hayo yamekuwa na mgogoro mkubwa tuanzie pale ili tuweze kupata uzoefu pia wa kuweza kutatua migogoro ya aina hiyo katika maeneo mengine.
Kwa hiyo, kuanzia Morogoro lengo lake kubwa ilikuwa tu ni katika kuhimili ile migogoro iliyokuwepo na kuona namna gani tutaweza kuisitisha ili tuweze kufanya kazi hii vizuri zaidi katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anasema, ni lini tutakwenda katika Mkoa wa Pwani na Lindi na hususan Rufiji na Kilwa, kama alivyotolea mfano.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme tu, kwa sababu utatuzi wa migogoro hii na upangaji na upimaji utafanyika kwa awamu mbili na tumekwishaanza, mimi niseme pale ambapo tutakuwa tumepanga ratiba inayofuatia, basi tutaweka na mikoa ambayo ina migogoro ukiwemo na Mkoa wa Pwani ambao nao pia unaonekana una migogoro mikubwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tutafanya hivyo kutegemeana na uzoefu tulionao katika migogoro iliyopo lakini pia katika kuhakikisha migogoro mingine haiibuki.