Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Primary Question

MHE. MCH.PETER S. MSIGWA (K.n.y. MHE. RUTH H. MOLLEL) Aliuliza:- Nchi yetu inaendeshwa kwa kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni katika kuajiri na kuwasimamisha kazi watumishi wa umma. Kuna baadhi ya watumishi wa umma wamesimamishwa kazi na Mheshimiwa Rais, RC na hata DC bila kuzingatia Sheria ya Utumishi wa Umma na Kanuni zake. Je, Serikali inasemaje kuhusu hili?

Supplementary Question 1

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Wizara ya Utumishi ina watumishi wanaofanya kazi vizuri, hawajatumbuliwa, Serikali kwa maana ya Chuo cha Ualimu, kutokana na swali langu namba 81 ambalo nilijibiwa kwamba suala la upandishaji madaraja na likizo za Watumishi wamelipwa kwa kiasi kile ambacho walikuwa wamekitaja.
Je, watakuwa tayari sasa kutoa orodha ile ya wale waliokwishalipwa kwa Chuo kile cha Korogwe cha
Ualimu ili kusudi Walimu waweze kujitambua kwa sababu huwa kama wanawalipa, wanaingiza moja kwa moja kwenye mishahara, watakuwa tayari kuitoa hiyo orodha ili iende kwa Mkuu wa Chuo kila mtu aweze kutambua kile alichoweza kulipwa?

Name

Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chatanda. Nimelifuatilia swali hili, nadhani wiki iliyopita lilijibiwa na Mheshimiwa Stella Manyanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kusema kwamba nitafuatilia na Wizara ya Elimu kwa karibu ili kuona waliolipwa ni akina nani na orodha iweze kutolewa.

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Primary Question

MHE. MCH.PETER S. MSIGWA (K.n.y. MHE. RUTH H. MOLLEL) Aliuliza:- Nchi yetu inaendeshwa kwa kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni katika kuajiri na kuwasimamisha kazi watumishi wa umma. Kuna baadhi ya watumishi wa umma wamesimamishwa kazi na Mheshimiwa Rais, RC na hata DC bila kuzingatia Sheria ya Utumishi wa Umma na Kanuni zake. Je, Serikali inasemaje kuhusu hili?

Supplementary Question 2

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwenye majibu ya Mheshiwa Waziri amesema, endapo mtumishi hajaridhika na hatua za kinidhamu alizochukuliwa, akate rufaa. Sasa endapo mtumishi huyo ametumbuliwa na Mheshimiwa Rais na hajaridhika na hayo matokeo, wapi achukue hatua za kuja kukata rufaa?

Name

Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza Mheshimiwa Silinde ameuliza swali zuri sana; na kama atakuwa amefuatilia hata katika hotuba yangu ya bajeti ya Ofisi ya Rais (Utumishi), ziko kesi mbalimbali ambazo hata Ofisi ya Rais (Utumishi) pia tunashitakiwa. Wako ambao wanafungua kupinga maamuzi ya Mheshimiwa Rais, wako ambao wanafungua kesi kupinga maamuzi ya Katibu Mkuu Kiongozi, lakini pia
katika Tume yetu ya Utumishi wa Umma ambayo ni mamlaka yenye Mamlaka ya Urekebu wamepokea kesi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, katika mwaka huu wa fedha tu peke yake, zaidi ya watumishi wa umma 76 wameweza kukata rufaa katika Tume ya Utumishi wa Umma na endapo hawataridhika, bado tunacho Kitengo cha Rufaa chini ya Mheshimiwa Rais pia (Public Service Appeals) wanaweza pia wakakata rufaa nyingine. Kwa hiyo, namhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu zipo na zinafuatwa na ziko wazi kabisa na wako ambao hata wanajikuta walikata rufaa dhidi ya Mheshimiwa Rais na wakaja kushinda endapo kama kuna taratibu inaonekana hazikufuatwa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Utumishi kwa majibu mazuri sana. Nilitaka kuongezea, kuna moja ambalo limewataja Wakuu wa Mikoa
na Wakuu wa Wilaya kuchukua hatua za kuwasimamisha au kuwafukuza kazi watumishi wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kifungu cha (5) cha Sheria ya Tawala za Mikoa, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ndio wawakilishi wa Serikali Kuu kwenye maeneo yao. Ukisoma pia kifungu cha 87 cha Sheria ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, kinawataja hawa na kwa ajili ya usahihi wa nukuu, napenda nisome kwa sababu wakati mwingine tunauliza swali lile lile kila siku. Bahati mbaya imeandikwa kwa Kiingereza, inasema hivi; “In relation to the exercise of the powers and performance of the functions of the Local Government Authorities confered by this Act, the role of the Regional Commissioner and the District Commissioner shall be to investigate the legality when questioned of the actions and decisions of the Local Government Authorities within their areas of jurisdiction and to inform the Minister to take such other appropriate action as may be required.”

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukisoma kifungu hiki unaona kabisa kwamba wao kuchukua hatua zozote zile, ziwe za kiutumishi ni sahihi, isipokuwa utaratibu aliouzungumza Mheshimiwa Waziri wa Utumishi ndiyo unaotakiwa.
Kwa mfano, Mkuu wa Mkoa anaposema wewe hufai, umefanya makosa haya, akasema publicly, siyo ndiyo kafanya tendo hilo la kumsimamisha au kumuadhibu yule mtumishi, anachofanya pale, baada ya tamko lile, sasa Mamlaka ya Nidhamu ya mtumishi husika ndiyo inachukua hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika level ya Halmashauri, sasa Mkurugenzi atamwandikia barua kama ni ya kumsimamisha au kumtaka atoe maelezo fulani kulingana na maagizo ya Mkuu wa Wilaya, au Mkuu wa Mkoa atafanya hivyo. Kwa ngazi ya Mkoa, RAS ndio Mamlaka ya Utumishi, naye anaweza kuagizwa na kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, siyo kutamka tu kwa Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya, ndiyo tayari basi yule amemchukulia hatua za kinidhamu.

Name

Rev. Peter Simon Msigwa

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Iringa Mjini

Primary Question

MHE. MCH.PETER S. MSIGWA (K.n.y. MHE. RUTH H. MOLLEL) Aliuliza:- Nchi yetu inaendeshwa kwa kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni katika kuajiri na kuwasimamisha kazi watumishi wa umma. Kuna baadhi ya watumishi wa umma wamesimamishwa kazi na Mheshimiwa Rais, RC na hata DC bila kuzingatia Sheria ya Utumishi wa Umma na Kanuni zake. Je, Serikali inasemaje kuhusu hili?

Supplementary Question 3

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nakubaliana naye kwamba kwa mujibu wa Sheria na Katiba yetu, Rais ndiye mwenye mamlaka ya mwisho na ndiye Mwajiri Mkuu.
Swali la msingi limeulizwa kwamba kumekuwa na practice ya kuanzia Rais mwenyewe na ma-DC na RCs kutumbua au kuwasimamisha watu kwa njia ya mnada, kupigia kura atumbuliwe au asitumbuliwe, kwa hiyo, swali la msingi linaulizwa hapa, ni kwa nini Serikali isifuate utaratibu na kanuni na sheria ambazo sisi wenyewe tumeziweka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, hawa ma-RC na ma-DC ni kada ya kisiasa kama sisi Wabunge tulivyo, hawana weledi na ndiyo maana Baba wa Taifa alisema tuliweka sheria ngumu sana ili mtu asizuke tu na kufukuza watu ovyo ovyo. Kwa kumuenzi Baba wa Taifa ambaye alithamini sana kada ya watendaji wa umma; je, Serikali itatoa tamko sasa kwamba ma-RC na ma-DC wasikurupuke tu kuwafukuzisha watu bila kufuata taratibu na kanuni za nchi?

Name

Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kuhusiana na kwa nini Serikali isifuate utaratibu, napenda kuendelea kusisitiza kwamba Serikali inafuata uratatibu na kwamba kwa wateule ambao wameteuliwa na Mheshimiwa Rais, hatua zao za kinidhamu huchukuliwa na Katibu Mkuu Kiongozi kwa mujibu wa kifungu cha 4(3)(d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema katika Ibara ya 36(4), Mheshimiwa Rais pamoja na kukasimu bado anayo mamlaka ya mwisho na hakatazwi kutumia mamlaka yake. Kwa watumishi wengine wa umma, kwa mujibu wa kifungu cha 6(1)(b) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Mamlaka za Nidhamu zimepewa mamlaka yao ya mwisho kabisa ya kuweza kuchukua hatua kwa watumishi wengine ambao sio wateule wa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuendelea kusisitiza kwamba jambo la msingi katika mamlaka za kinidhamu zinapochukua hatua, wanatakiwa wazingatie hatua tatu zifuatazo:-
Kwanza kabisa waweze kutoa hati ya nashtaka; pili, watoe fursa ya kujitetea kwa yule mtuhumiwa au mtumishi; na mwisho, tatu, uchunguzi wa kina uweze kufanyika ili kuthibitisha tuhuma hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, napenda kusema, utaratibu mzima wa kina na mwongozo umefafanuliwa katika kanuni ya 46 na 47 za Kanuni za Utumishi wa Umma. Endapo kuna mtumishi wa umma anaona hajaridhika na hatua za kinidhamu zilizochukuliwa, anayo fursa kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha Sheria ya Utumishi wa Umma kuweza kukata rufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la pili kwamba Serikali inatoa tamko gani katika hatua ambazo zimechukuliwa na ma-RC na ma-DC? Naendelea kusisitiza kwamba kifungu cha 6(1)(b) na kifungu cha 4(3)(d) kimeelekeza Mamlaka za Nidhamu ni zipi? Ndicho ambacho
Serikali imekuwa ikifuata.