Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Maria Ndilla Kangoye

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIA N. KANGOYE aliuliza:- Kumekuwepo uhaba wa watumishi katika Halmashauri nyingi nchini ambao unaleta athari katika utekelezaji wa shughuli za Halmashauri kwa kutotoa huduma katika kiwango kinachohitajika. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuajiri wataalam hasa vijana waliomaliza vyuo ambao wanazurura mitaani kwa ukosefu wa ajira?

Supplementary Question 1

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri kutoka kwa Waziri, ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kumekuwa na utaraibu wa wastaafu kuongezewa mikataba ya kufanya kazi. Je, Serikali haioni kwamba hii ni sababu mojawapo ya ukosefu wa ajira kwa vijana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kati ya Wilaya saba za Mkoa wa Mwanza, Wilaya sita ambazo ni Sengarema, Ilemela, Nyamagana, Misungwi na Magu, pamoja na Ukerewe, zinategemea asilimia kubwa ya mapato yake kutoka kwenye sekta ya uvuvi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri vijana wenye taaluma ya uvuvi ili kuweza kukidhi haja ya elimu ya kilimo cha samaki pembezoni mwa Ziwa Victoria? Ahsante.

Name

Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kuhusiana na Serikali kuongezea muda wastaafu au kuwapa mkataba wa ajira, nipende kusema yafuatayo; kwanza kabisa tunao waraka ambao ndio mwongozo unaotoa taswira au mwongozo ni watu gani au kada zipi ambazo zinastahili kuweza kuongezewa mkataba wa ajira.
Nipende tu kusema kwamba kwa sasa kipaumbele kipo kwa marubani, kipaumbele kipo kwa wahadhiri wa vyuo vikuu na hao ndio wanaopewa mikataba. Lakini ni lazima wao pia wanapoomba kuongezewa mkataba wa ajira baada ya kustaafu, ni lazima waweze kuwasilisha mpango wao wa kurithishana madaraka, lakini vilevile ni lazima na wenyewe waweze kutoa wamefanya jitihada gani za kuhakikisha kwamba wanawawezesha watumishi wengine walioko chini yao kuhakikisha kwamba wanaweza ku-take over baada ya wao kuondoka katika nafasi hizo walizonazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la pili hasa katika ajira za vijana na ameongelea zaidi katika ajira za uvuvi; kwanza nipende tu kusema kwamba Mkoa wa Mwanza katika takribani Wilaya zake nne tunatambua ndizo ambazo zina upungufu mkubwa wa watumishi ikiongozwa na Wilaya ya Buchosa, Wilaya ya Kwimba pamoja na Wilaya ya Ukerewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika ikama ya mwaka huu 2016/2017 nitolee tu mfano katika Wilaya ya Ukerewe, wavuvi wasaidizi takribani watano wamepangiwa na hizo ni katika nafasi chache ambazo zimewekwa katika utaratibu wa ikama ya mwaka 2016/2017. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kada ambazo zina upungufu mkubwa katika Halmashauri hizo tutazipa kipaumbele ili kuhakikisha kwamba, wanaweza kufanya kazi kwa ufanisi na kwa uweledi mkubwa.

Name

Hawa Abdulrahiman Ghasia

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Primary Question

MHE. MARIA N. KANGOYE aliuliza:- Kumekuwepo uhaba wa watumishi katika Halmashauri nyingi nchini ambao unaleta athari katika utekelezaji wa shughuli za Halmashauri kwa kutotoa huduma katika kiwango kinachohitajika. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuajiri wataalam hasa vijana waliomaliza vyuo ambao wanazurura mitaani kwa ukosefu wa ajira?

Supplementary Question 2

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunavyozungumza ni Februari tunaelekea Juni, mwaka wa fedha unaishia na Mkoa wa Mtwara ni miongoni mwa mikoa ambayo ina tatizo kubwa la watumishi na hasa wa sekta ya afya. Nilitaka kufahamu ni lini hicho kibali kitatolewa na ajira hizo zitaajiriwa? Kwa sababu ninavyo vituo viwili vya afya vyenye vyumba vya upasuaji, lakini hakuna upasuaji unaofanyika kwa sababu hakuna watumishi na Wilaya nyingine zote za Mkoa wa Mtwara hali ni hiyo hiyo, ni lini kibali kitatolewa?

Name

Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa namna anavyofuatilia masuala mazima ya utumishi na tunatambua pia, na yeye alishakuwa Waziri wa Utumishi na alifanya kazi kubwa na nzuri sana hapo alipokuwa na sisi tumeweza kuvaa viatu vyake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa sasa, kama nilivyoeleza, tumeanza na watumshi wa sekta ya elimu pamoja na mafundi sanifu wa maabara na tunatarajia ifikapo mwezi wa tatu wataweza kuingia katika ajira. Kwa upande wa watumishi wa sekta ya afya, muda si mrefu tutaanza pia awamu yao na ninadhani kati ya mwezi wa tatu mpaka wa nne watakuwa wameshaingia katika utumishi.

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Primary Question

MHE. MARIA N. KANGOYE aliuliza:- Kumekuwepo uhaba wa watumishi katika Halmashauri nyingi nchini ambao unaleta athari katika utekelezaji wa shughuli za Halmashauri kwa kutotoa huduma katika kiwango kinachohitajika. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuajiri wataalam hasa vijana waliomaliza vyuo ambao wanazurura mitaani kwa ukosefu wa ajira?

Supplementary Question 3

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Ni kweli kwamba kuna changamoto nyingi kwa watumishi wa umma, ni pungufu kwa uwezo mdogo wa Serikali kuajiri na wengine wametumbuliwa katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nijue ni nini kauli ya Waziri wa Utumishi kwa watumishi wale ambao wanashushwa vyeo, wanadhalilishwa na kutukanwa na viongozi, hasa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa na ukizingatia matokeo ya form four yametoka, wameanza kutumbuliwa. Sasa nini kauli ya Serikali kuwatia moyo waliopo kazini na kuwatia moyo ambao watapata ajira, ili wajue wataenda mahali salama wakafanye kazi nzuri kutumikia Watanzania?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupata majibu.

Name

Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niseme tu kwamba masuala mazima ya nidhamu, ajira pamoja na upandishwaji wa vyeo na kushushwa vyeo yanaongozwa na kanuni, sheria na taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kusema tu ni kwamba, kama kuna ambaye anaona kanuni hazikufuatwa, basi tuweze kupata taarifa ili tuweze kufuatilia. Lakini tumekuwa tukitoa miongozo mbalimbali kwa viongozi wa kisiasa pamoja na watendaji kuhakikisha kwamba, wanazingatia Sheria ya Utumishi wa Umma, wanazingatia Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma, pamoja na Kanuni za Utumishi wa Umma. Kwa hiyo, nipende tu kusema kwamba kama kuna mtumishi ambaye naona yeye hakutendewa haki basi asisite kuwasilisha malalamiko yake.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana yaliyotolewa na Waziri Mheshimiwa Kairuki, napenda niongezee tu kwenye swali lililoulizwa na Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kumekuwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kutokana na watumishi wazembe. Na mtambue kwamba katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi tulisema kwamba kwa watumishi wazembe hatutakubali kuendelea nao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichukue nafasi hii kusema kwamba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wamegawiwa maeneo yao ya utawala na wanasimamia masuala yote, lakini wanasimamia yote kwa mujibu wa sheria. Haiwezekani unapewa pesa ya basket fund, wewe ni DMO halafu huzitumii na watu wanakosa huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya utafiti katika mikoa minne, ziko hela nyingi kwenye Halmashauri hazitumiki, wanataka kuzifanyia nini? Mnasema tusichukue hatua, haiwezekani. Haiwezekani unapewa shule una walimu zaidi ya 15 pamoja na changamoto zilizopo ambazo ni haki yao kuzidai, lakini si sababu ya wao kutokutimiza wajibu wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema tu kwamba Wakuu wa Mikoa wanayo haki ya kisheria kuchukua hatua kwa mtumishi yeyote awe ni Mkuu wa Shule, kwa mfano uteuzi wa Mkuu wa Shule unateuliwa na RAS ambaye ndio Katibu Mkuu wa Mkoa. Kwa hiyo, Mkuu wa Mkoa akichukua ile hatua, nimekuwa nikiulizwa na Wabunge wengi hapa kwamba mbona wanaingilia mambo mengine. Jamani, mkumbuke mlikuwa mnasema watumishi wetu ni wazembe. Ngonjeni kidogo tubanane ili twende kwenye ufanisi na Watanzania wanangojea hayo mabadiliko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwasihi tu Waheshimiwa Wabunge, tushirikiane. Wenzetu nao wale ni binadamu katika namna moja au nyingine wanaweza wakafanya makosa, tuwasiliane, turekebishane, ndio maana ya administration and leadership. Si kwamba wao hawakosei, wanaweza wakakosea kwa namna moja ama nyingine, lakini na mazingira yale tuyaangalie, lakini huku nikitambua kwamba watumishi nao wana haki yao, lakini na wao pia watekeleze majukumu tuliyowapa.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nilitaka kuongezea tu kwenye jibu linalohusu mkakati wetu wa kupeleka huduma za upasuaji kwenye vituo vya afya nchini wakati hakuna watumishi wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwishakutoa maelekezo kama Serikali kwa Makatibu Tawala wote wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kufanya redistribution ya watumishi ndani ya maeneo yao, kuwatoa kwenye maeneo ambapo wapo wengi na kuwapeleka kwenye vituo hivyo ambavyo tunataka vitoe huduma za upasuaji. Huu ni mkakati wa muda tukisubiri mkakati wa kudumu.