Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Musa Rashid Ntimizi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Primary Question

MHE. MUSA R. NTIMIZI aliuliza:- Serikali iliahidi kujenga viwanda mahali zinapopatikana malighafi. (a)Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanda cha Tumbaku Mkoani Tabora? (b)Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kiwanda cha Kusindika Asali Mkoani Tabora?

Supplementary Question 1

MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini pia pamoja na Serikali kutoa maelekezo kwa TIC kuhusu kunadi fursa hiyo kwa wawekezaji kuja kujenga kiwanda hiki Mkoani Tabora lakini wawekezaji wa Philip Morris wanaozalisha sigara duniani wanatarajia kuja kujenga kiwanda hiki mkoani Morogoro. Pamoja na kwamba Serikali kupitia Halmashauri yetu ya Nzega, Tabora Manispaa na Wilaya ya Uyui tulishatoa maeneo kwa ajili ya kiwanda hiki kuja kujengwa Tabora, lakini bado tunasikia Philip Morris wanakuja kujenga kiwanda hiki Mkoani Morogoro.
Je, Serikali haioni kwamba haiwatendei haki wana Tabora ambao ndiyo watoka jasho wakubwa katika zao hili la tumbaku? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali dogo la pili, Serikali imekiri asali bora na nyingi inazalishwa katika Mkoa wa Tabora hususani katika Jimbo la Igalula. Kwa nini Serikali kwa makusudi makubwa kabisa isingesaidia uongezaji wa thamani wa zao hili la asali kwa maana ya kupata utaalamu na packaging ili kusaidia kipato cha wana Igalula na nchi kwa ujumla? Ahsante.

Name

Dr. Charles John Tizeba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Answer

WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WIZARA YA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ntimizi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Kampuni ya Philip Morris wamekwishaanza ujenzi wa kiwanda cha kuongeza thamani ya tumbaku pale Morogoro. Wawekezaji wanazo sababu na vigezo wanavyovitumia katika kuchagua maeneo ya mahali gani wawekeze. Kazi ya Serikali mara zote imekuwa ni kuwashawishi na kuwashauri lakini hatufiki mahali tukawalazimisha kama wao wanaamini kwamba sehemu fulani ndipo patakapowapa tija katika uwekezaji wao. Kwa hivyo, Philip Morris pamoja na kushauriwa kwamba wakajenge kiwanda hicho Tabora wao waliamua kuendelea kuwekeza hapo Morogoro. Tukiwalazimisha wanaweza wakaamua kwenda kujenga kiwanda hicho nchi nyingine ambayo pia inazalisha tumbaku. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini baada ya kuona hilo, Chama Kikuu cha Ushirika cha Tumbaku Mkoa wa Tabora (WETCU) katika mkutano wao mkuu waliamua kwamba na wao wawekeze kwenye kiwanda cha kuongeza thamani tumbaku. Mpaka leo wamekwishapata eneo kule Urambo na limepimwa. Sasa hivi wanafanya tathmini ili walipe fidia kwa wananchi walioko pale. Wakishawaondoa wale wananchi walio kwenye eneo hilo, ujenzi wa kiwanda cha kuongeza thamani katika mkoa wa Tabora Wilaya ya Urambo utaanza kufanyika mara moja kupitia Chama hiki cha Msingi cha Ushirika cha WETCU.
Mheshimiwa Spika, swali la pili la nyongeza la Mheshimiwa Ntimizi lilihusu wananchi kueleweshwa namna bora ya kusindika na kufungasha asali. Hili jambo linaendelea, viko vikundi na kupitia Halmashauri vikundi hivi vimekuwa vinaendelea kupatiwa mafunzo ya namna hii na SIDO Mkoa wa Tabora na wao wamekuwa wakijihusisha na hili jambo la kuwafundisha wananchi namna bora ya usindikaji wa asali ili iweze kuwa na ushindani katika soko la ndani na soko la Kimataifa.