Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Primary Question

MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:- Mfumo wa sasa wa kuwahudumia wakulima wa zao la tumbaku wa Wilaya ya Urambo na Mkoa wa Tabora kwa ujumla una mapungufu mengi yanayowaletea wakulima usumbufu kama vile bei za pembejeo kuwa kubwa kutokana na kuagizwa nje na riba kubwa za benki, masoko ya tumbaku kutokuwa na uhakika na hatimaye kusababisha kushuka thamani ya tumbaku, bei inayobadilika pamoja na uchache wa wanunuzi:- (a) Je, ni kwa nini hasara inayotokana na matatizo hayo ibebwe na mkulima peke yake? (b) Je, Serikali imejipanga vipi kuondoa matatizo hayo ili mkulima wa tumbaku anufaike na kilimo na hatimaye ajikwamue kiuchumi?

Supplementary Question 1

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri amekiri kwamba mfumo uliopo una matatizo katika kumhudumia mkulima. Lakini Serikali inashiriki kikamilifu katika kupanga bei katika mfumo mzima. Sasa kwa kuwa Serikali inashiriki kwa kupitia wakala wake bodi au council, je, Serikali haioni kwamba inawajibika kubeba sehemu ya hasara anayopata mkulima?
Kwa kiasi gani mmefaulu kupata wanunuzi zaidi kutoka China ili soko liwe la haraka na wakulima wanufaike?

Name

William Tate Olenasha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, Tobacco Council au Halmashauri ya Tumbaku inawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya tumbaku. Serikali yenyewe haihusiki moja kwa moja katika kupanga bei lakini imeweka tu utaratibu ambao wadau wenyewe wanaweza kukaa kukutana kwa uhuru wao na kupanga bei. Hata hivyo, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba bei ya tumbaku inaendelea kuwa nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba tokea mwaka 2013 Bunge hili lilipitisha Sheria mpya ya Vyama vya Ushirika, utaratibu mpya wa Vyama vya Ushirika ni utaratibu ambao pamoja na mambo mengine unawaruhusu wakulima wa mazao mbalimbali kuendesha shughuli zao kwa kuwa na uhuru zaidi. Lakini vilevile mpango ule umeunda Tume ya Ushirika ambayo inakuwa karibu na Vyama vya Ushirika ili kuwezesha kuondoa kero zilizopo. Tunafikiri kwamba utaratibu huu utaleta ufanisi zaidi katika kilimo cha tumbaku pamoja na mazao mengine ikiwa ni pamoja na kusaidia katika suala la bei.
Lakini nitumie tu fursa hii kuwawelezea vilevile Waheshimiwa Wabunge kwamba pamoja na changamoto nyingi zilizopo kwenye sekta ndogo ya tumbaku, tunafikiri sekta ndogo ya tumbaku ni eneo ambalo limeanza kuonesha mifano ya kufanikiwa. Hii ni kwa sababu ndiyo sekta ndogo ya pekee ambayo mkulima anakuwa na uhakika wa kuuza zao lake tokea siku ya kwanza anapoanza kuweka mbegu shambani kwa sababu ni kilimo cha mkataba. Kwa hiyo, tukiondoa changamoto zilizopo tunafikiri ni eneo ambalo bado inawezekana kupata mafanikio makubwa. Lakini vilevile tungependa kutumia fursa hii kuwaeleza wakulima…
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia. Kuwafahamisha kwamba kufanikiwa kutumia mfumo wa mkataba utasaidia tu kama kila mtu akiheshimu mkataba. Kwa mfano, mwaka huu tayari wakulima wanafahamu inatakiwa wazalishe tumbaku kiasi gani, tunaomba wale ambao hawako kwenye mkataba usizalishe tumbaku kwa sababu ukizalisha hautaweza kupata mnunuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipengele cha pili cha swali ni kwamba ni kiasi gani na kwamba tumefikia wapi na kuwapata wanunuzi kutoka China.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inajitahidi kuongea na wafanyabiashara kutoka China, tumefika hatua nzuri sana kilichobakia sasa ni wao kumaliza taratibu za nchi mwao ili nao waweze kuingia kwenye mfumo rasmi wa kununua tumbuku ili kuondoa ukiritimba ambao mpaka sasa hivi nchi nzima kampuni zinazonunua tumbaku ni nne tu.
Kwa hiyo, tunafikiri kampuni zikiwa nyingi maana yake tunaondoa monopoly na hivyo bei itakuwa nzuri nashukuru sana.