Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 9 Sitting 10 Youth, Disabled, Labor and Employment Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu 139 2022-11-11

Name

Janeth Elias Mahawanga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuzungumza na taasisi za kifedha ili mikopo kwa watu wenye ulemavu itolewe kwa mtu mmoja mmoja badala ya vikundi?

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Elias Mahawanga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, taasisi mbalimbali za kifedha ikiwemo mabenki zimekuwa zikitoa mikopo kwa mtu mmoja mmoja na makundi mbalimbali wakiwemo watu wenye ulemavu. Aidha, wananchi wa kipato cha chini wakiwemo makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wanashindwa kunufaika na mikopo inayotolewa na taasisi hizo kutokana na mikopo hiyo kuambatana na vigezo vinavyowekwa ikiwemo waombaji kuwa na dhamana au mali isiyohamishika kama viwanja, mashamba na nyumba.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua changamoto hiyo, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI imekuwa ikisimamia utoaji wa mikopo ya uwezeshaji kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa mujibu wa kifungu 37A cha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa na Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu za mwaka 2019 na marekebisho yake ya mwaka 2021. Sheria na Kanuni hizi zimeelekeza kuwa mikopo hii itatolewa kwa vikundi vya wajasiriamali wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa uwiano wa asilimia nne kwa wananwake; nne kwa vijana na mbili kwa watu wenye walemavu kwa lengo la kuwawezesha kuanzisha na kuendeleza shughuli zao za ujasiriamali ili kujiongezea kipato na kupunguza umaskini.

Mheshimiwa Spika, habari njema ni kwamba Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imefanya marekebisho ya Kanuni mwaka 2021 ambayo yametoa fursa kwa mtu mmoja mmoja mwenye ulemavu kuomba mkopo. Hivyo, niombe Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote kwamba tufikishe taarifa hii ya mabadiliko ya kanuni za mikopo hiyo ambayo imetoa fursa kwa mtu mmoja mmoja mwenye Ulemavu kuomba mkopo.