Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 3 Sitting 16 Information, Culture, Arts and Sports Wizara ya Fedha 139 2016-05-10

Name

Hafidh Ali Tahir

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dimani

Primary Question

MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. MHE. HAFIDH ALI TAHIR) aliuliza:-
Mheshimiwa Spika, katika Bunge la 2005 – 2010 kulitokea hoja ya TFF kujiunga katika Shirikisho la Mpira la Kimataifa (FIFA) bila ridhaa ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar; hoja hiyo ilipelekea aliyekuwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda kuunda Kamati Maalum yenye Wajumbe kutoka ZFA na TFF ili kuondoa utata huo:-
(a) Je, ni nini matokeo ya Kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu?
(b) Je, Serikali haioni kuwa kutopatikana muafaka au uamuzi uliofikiwa kwa pamoja ni kuchelewesha agizo la Waziri Mkuu?
(c) Je, Serikali inasemaje kuhusu ubabaishaji unaofanywa na TFF?

Name

Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Answer

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hafidh Ali Tahir, Mbunge wa Dimani, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, kufuatia majadiliano na vikao kadhaa vilivyofanyika katika kipindi cha mwaka 2005/2010 kumbukumbu zinaonyesha kwamba suala zima la uanachama wa TFF na ZFA lilifanyiwa kazi kwa ukamilifu na Serikali za pande zote mbili kwa ushirikiano na vyama vyote viwili.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa ZFA kupata uanachama wa FIFA, mwaka 2010 Ujumbe wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ukiongozwa na aliyekuwa Naibu Waziri Kiongozi Mheshimiwa Juma Shamhuna pamoja na aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Mheshimiwa Joel Bendera walikwenda Zurich-Switzerland ambako walikutana na Rais wa FIFA wa wakati huo. Aidha, katika msafara huo walifuatana na viongozi wa TFF na ZFA. Madhumuni ya safari hiyo ilikuwa ni kuwasilisha maombi ya ZFA kupewa uanachama wa FIFA.
Mheshimiwa Spika, mwezi Juni 2011, FIFA iliiandikia ZFA ikiwajulisha kuwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo isingewezekana Zanzibar kupata uanachama wa FIFA kwa kuwa uanachama wao ni nchi zinazotambuliwa na Jumuiya ya Kimataifa kama ilivyoelezwa katika aya ya 10 ya Katiba hiyo.
(b) Mheshimiwa Spika, kwa maelezo haya, ni dhahiri kuwa suala la usajili wa TFF na ZFA linafahamika vyema ndani ya Serikali ya Mapinduzi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata hivyo naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa uanachama wa TFF katika FIFA upo kwa mujibu wa muafaka wa pande zote mbili.
(c) Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia utaratibu huo wa FIFA kuhusu suala hilo, Wizara yangu imewaelekeza TFF na wako tayari kufanya maridhiano na ZFA ili kukamilisha utaratibu wa wazi wa kukidhi mahitaji ya Zanzibar kushiriki katika masuala ya FIFA kupitia TFF bila kuathiri ushiriki wa klabu za Zanzibar katika mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika yaani CAF.