Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 2 Sitting 6 Youth, Disabled, Labor and Employment Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu 73 2021-02-09

Name

Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. COSATO D. CHUMI Aliuliza:-

Kituo cha Uwekezaji (TIC) kinampa haki mwekezaji kuajiri wataalam lakini upande wa pili sheria inampa mamlaka Kamishna wa Kazi kufanya maamuzi kuhusu maombi ya vibali vya kazi:-

Je, ni lini Serikali italeta marekebisho ya sheria ili kuondoa mgongano huo?

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuzungumza katika Bunge hili, naomba nichukue fursa hii pia kuwashukuru sana wananchi wa Shinyanga ambao walinichagua kwa kishindo. Pia nikishukuru zaidi Chama cha Mapinduzi, wakiongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kwa ushindi wa kishindo nchi nzima usio na mashaka yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe pole kwa wananchi wa Shinyanga kwa kupotelewa na Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Mapinduzi, Ndugu Erasto Kwilasa. Mwenyezi Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu, amina.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kufungua milango kuwavutia wawekezaji kuwekeza nchini. Serikali kupitia Sheria ya Uwekezaji, Sura 38 kama ilivyofanyiwa marekebisho na marejeo yake mwaka 2015 inatoa motisha mbalimbali (incentives) kwa wawekezaji. Miongoni mwa motisha hizo ni kuwaruhusu wawekezaji kuajiri wataalam wa kigeni watano, kwa lugha ya kigeni inaitwa Immigration Quota wakati wa hatua za awali za utekelezaji wa miradi yao (startup period) inapoanza kufanyika chini ya kifungu cha 24 cha Sheria ya Uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kulinda uchumi wetu, ajira za wazawa, maslahi na usalama wa nchi yetu, Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni Na.1 ya mwaka 2015 kupitia kifungu cha 5(1)(b) na 11 kinampa Kamishna wa Kazi mamlaka ya kusimamia ajira za raia wa kigeni nchini kwa lengo la kuhakikisha ajira zinazotolewa kwa wageni ni zile ambazo sifa za kielimu, ujuzi, uzoefu wa kazi ni adimu hapa nchini. Katika kutekeleza jukumu hili, Kamishna wa Kazi hupokea na kuchambua maombi ya vibali vya kazi vya raia wa kigeni kutoka kwenye kampuni/taasisi zinazohitaji kuajiri wageni wanaokidhi vigezo na masharti yaliyowekwa kwa mujibu wa sheria tajwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamishna wa Kazi ameendelea kuzingatia sheria zote, taratibu, sera na kanuni katika kufikia maamuzi yake. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge katika kupokea maoni na mapendekezo yanayolenga mabadiliko ya sheria na sera ili kuimarisha zaidi uwekezaji nchini bila kuathiri matakwa ya sera, sheria, taratibu na kanuni na miongozo iliyowekwa nchini.