Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 53 Works, Transport and Communication Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 468 2019-06-26

Name

Joyce Bitta Sokombi

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga barabara itokayo Bunda kwenda Musoma Vijijini ili kuwapunguzia wananchi wa Saragana, Bugoji, Mabui Merafuru, Melaturu, Kangetutya na Kanderema aidha ya kuzunguka kupitia Musoma Mjini?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo; ingawaje marekebisho aliyoyafanya sikuyapata sawasawa kwa hiyo kama nitakosea haya majina magumu naomba aniwie radhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipande cha barabara kuu kutoka Bunda hadi Manyamanyama chenye urefu wa kilomita 5.79 kinahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mara. Aidha, ukarabati wa kipande hiki ulikamilika mwaka 2016 na kwa sasa kipo katika hali nzuri hivyo kupitika kwa urahisi wakati wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mkoa kutoka Manyamanya kupitia Vijiji vya Bugoji – Saragana hadi Nyambui kilomita 37.45 inahudumiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Mara na kwa sasa barabara hii inapitika vizuri. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali ilitenga jumla ya shilingi milioni 351.976 kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hii. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 130.855 kwa ajili ya kuendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili ipitike majira yote ya mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara inayoanzia Saragana hadi Kanderema kupitia Vijiji vya Mabui Merafuru na Kangetutya ni barabara ya wilaya ambayo ipo chini ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini (TARURA). Hivyo namshauri Mheshimiwa Mbunge awasiliane na TAMISEMI kuhusu mipango waliyonayo kwa sehemu hiyo ya barabara.