Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 17 Sitting 4 Industries and Trade Viwanda na Biashara 52 2019-11-08

Name

Anatropia Lwehikila Theonest

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ANATROPIA L. THEONEST aliuliza:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwalipa fidia wananchi ambao maeneo yao yalichukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Uwekezaji vya Nkwenda na Murongo?

(b) Je, ni lini ujenzi wa Vituo hivyo utaanza?

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kuwa ujenzi unaotarajiwa kufanyika ni wa Masoko ya Kimkakati ya Kimataifa ya Nkwenda na Murongo na sio Vituo vya Uwekezaji kama alivyouliza swali lake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inamiliki maeneo yanapojengwa masoko ya Kimkakati ya Nkwenda na Murongo kwa asilimia 100. Eneo la kiwanja cha soko la kimkakati la Nkwenda lilikuwa chini ya Serikali ya Kijiji cha Nkwenda na lilitumika kama shamba kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Kijiji (MFUMAKI). Eneo hilo liliendelea kutumika kama shamba darasa (Farmers Extension Centre Demonstration Area) chini ya Wizara ya Kilimo, hivyo halihitaji fidia. Aidha, Eneo linapojengwa soko la kimkakati la Murongo ni mpakani mwa Nchi ya Tanzania na Uganda linalomilikiwa na Serikali, hivyo halihitaji fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Masoko ya Kimkakati ya Kimataifa ya Nkwenda na Murongo ni masoko yaliyokuwa yanajengwa kama sehemu ya utekelezaji wa Programu ya kuendeleza Sekta ya Kilimo (Agricultural Sector Development Program-ASDP) kupitia Mradi wa Uwekezaji katika sekta ya kilimo ngazi ya Wilaya (District Agricultural Sector Investment Project- DASIP). Ujenzi wa masoko hayo mpaka sasa umekamilika kwa asilimia hamsini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inayoratibu Programu ya kuendeleza Sekta ya Kilimo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020, imetenga shilingi bilioni 2.5 fedha za ndani kwa ajili ya kukamilisha mradi wa ujenzi wa masoko ya kimkakati. Katika kuhakikisha kuwa ujenzi wa masoko hayo unakamilika na kuanza kutumika, Wizara ya Kilimo imetuma wataalam kutoka Wakala wa Nyumba (TBA) kwa ajili ya kufanya tathmini ya gharama za umaliziaji wa ujenzi wa masoko hayo.