Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 17 Sitting 4 Works, Transport and Communication Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 49 2019-11-08

Name

Musa Rashid Ntimizi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Primary Question

MHE. MUSA R. NTIMIZI aliuliza:-

Wananchi wa Kata ya Tura katika Vijiji vya Mwamlela, Mmunyu na Nkongwa hawana kabisa mawasiliano ya simu licha ya umuhimu wa mawasiliano kiusalama na kiuchumi:-

Je, Serikali inatoa ahadi gani ya kupatikana kwa mawasiliano katika vijiji hivyo?

Name

Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Musa Ntimizi, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba uniruhusu nitoe ufafanuzi wa Serikali kuhusu hoja iliyojadiliwa jana na baadhi ya wajumbe kuhusu sifa za mtu kuajiriwa kufanya kazi katika Shirika letu la Ndege la ATCL. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika letu la Ndege la ATCL na Serikali kwa ujumla limeainisha sifa mbalimbali zinazomruhusu Mtanzania kuweza kuajiriwa na Shirika hilo la Ndege. Sifa yetu ya kwanza kabisa ni Mtanzania yeyote mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea ambaye anafahamu kwa ufasaha lugha mbili za Kiingereza na Kiswahili. Pia Mtanzania huyo anatakiwa awe na Cheti cha Kuongoza Ndege au Cheti cha Kufanya Kazi ndani ya Ndege (cabin crew) ambacho kitakuwa kina mafunzo maalum ya usalama ndani ya ndege lakini na huduma kwa abiria ambao wanatumia ndege ile. Sifa nyingine ya tatu na muhimu kabisa ni lazima awe na leseni ya kuruka inayotolewa na Mamlaka ya Anga au TCAA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sifa ya ziada ni lazima awe na uelewa mkubwa wa masuala ya kitaifa, kidunia, utalii hasa nchini kwetu lakini awe ni mtu awe na hekima, ana discipline na very ethical na tutamchunguza katika hayo kuhakikisha kwamba anaweza kuajiriwa ndani ya Shirika letu la Ndege. Sifa nyingine zote zilizozungumzwa siyo ambazo zinazingatiwa na ATCL wala zinazingatiwa na Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, nijibu swali la Mheshimiwa Musa Ntimizi, Mbunge wa Igalula kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kufikisha huduma za mawasiliano kote nchini. Mwezi Julai, 2019, Mfuko ulitangaza zabuni ya awamu ya nne kwa ajili ya kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata 521 zenye vijiji 1,222. Kata ya Tura ilijumuishwa kwenye zabuni hiyo ikiwa na vijiji vya Karangasi, Mmunyu na Mwamlela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zabuni hiyo ilifunguliwa na baada ya tathmini, tulipata wazabuni katika maeneo hayo. Utekelezaji utaanza baada ya mkataba kusainiwa mwezi Desemba, 2019.