Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 17 Sitting 3 Union Affairs Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira 33 2019-11-07

Name

Jaku Hashim Ayoub

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Primary Question

MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:-

Kwa mujibu wa taarifa ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya mwaka 2014, Kisiwa cha Latham ni mali ya Zanzibar tangu kilipofunguliwa rasmi mwaka 1898. Hata hivyo, zipo taarifa zilizothibitishwa kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu iliiandikia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwaarifu kuwa Kisiwa hicho ni cha Tanzania Bara.

(a) Je, ni lini Serikali hizi mbili ambazo ni ndugu wa damu watakaa kutatua kero hii ya muda mrefu?

(b) Je, Serikali haioni kuwa umefika muda muafaka kulifanyia kazi suala hilo?

Name

Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, Ibara ya 2(1) inatamka wazi kuwa eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni eneo lote la Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar pamoja na sehemu ya bahari ambayo inapakana na nchi za Kenya, Shelisheli, Comoro na Msumbiji. Hivyo basi, kwa mujibu wa tafsiri ya mipaka hiyo, Kisiwa cha Latham (Fungu Baraka) kiko ndani ya eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mgogoro wa umiliki wa eneo la kisiwa hicho kwa vile kimo ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.