Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 18 Sitting 9 Livestock , Fisheries, Agriculture, Food Security and Cooperatives Wizara ya Mifugo na Uvuvi 110 2020-02-07

Name

Hamadi Salim Maalim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Kojani

Primary Question

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM (K.n.y. MHE. HAMADI SALIM MAALIM) aliuliza:-

Uvuvi si suala la Muungano na wavuvi wengi wa Visiwa vya Unguja na Pemba wanapokuwa katika maeneo mbalimbali ya mwambao wa Afrika Mashariki hukumbana na changamoto nyingi ikiwemo kukamatwa wanapokuwa katika shughuli zao za uvuvi, kutozwa tozo zisizo za lazima na kadhalika:-

Je, Serikali imejipangia mikakati gani ili kupunguza changamoto hizo?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamadi Salim Maalim, Mbunge wa Kojani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa uvuvi katika maji ya ndani na maji ya kitaifa sio suala la Muungano kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo kila upande wa Muungano una sheria, kanuni na miongozo inayosimamia masuala ya uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2018 na 2019 zinaelekeza mvuvi anapohamisha shughuli zake za uvuvi kutoka eneo moja kwenda eneo lingine anapaswa kuwa na leseni na vibali vya kujishughulisha na shughuli za uvuvi na kujitambulisha kwa mamlaka za eneo husika. Vilevile, tozo mbalimbali zinatozwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imeweka mikakati ya kupunguza na kuondoa kabisa changamoto wanazokumbana nazo wavuvi katika maeneo mbalimbali ya mwambao wa Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwaelimisha wavuvi kuzingatia sheria, kanuni za uvuvi na miongozo iliyopo pamoja na kuheshimu mipaka ya nchi kwa kutovua katika maji ya nchi jirani bila kufuata taratibu zilizowekwa. Aidha, katika kuboresha shughuli za uvuvi na mazao yake, Serikali ipo katika hatua ya kufanyia marekebisho sheria na kanuni za uvuvi ili ziweze kuendana na wakati katika kutunza na kuendeleza rasilimali za uvuvi ili sekta hii iweze kuchangia ipasavyo kwenye Pato la Taifa na la mtu mmoja mmoja.

Vilevile, Serikali imekuwa ikifanya vikao vya ujirani mwema na nchi jirani ili kutatua changamoto zinazojitokeza. Serikali kupitia Mheshimiwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Ally Mohamed Shein alitukutanisha na viongozi wa Mamlaka za Pwani ya Kenya siku ya tarehe 26 hadi 28 Jijini Nairobi wakati wa Mkutano Mkubwa wa Blue Economy.