Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 18 Sitting 4 Justice and Constitutional Affairs Katiba na Sheria 42 2020-01-31

Name

Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-

Kwa mujibu wa GN. No. 222 na 223 ya mwaka 1972 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2002, Wazee wa Mabaraza ya Mahakama wanateuliwa na vikao vya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Kamati za Maadili za Mahakimu zipo chini ya Uenyekiti wa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya:-

Je, ni lini Mahakama itaacha kuingiliwa na siasa?

Name

Dr. Augustine Philip Mahiga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Tanzania ni moja ya mihimili mitatu ya dola ambayo kwa mujibu wa Ibara ya 4 na 107(B) ya Katiba, Mahakama ni Mhimili huru na hauingiliwi na chombo chochote katika utekelezaji wa majukumu yake ya utoaji haki.

Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa majukumu yake, Mahakama imekuwa ikiwatumia Wazee wa Baraza katika ngazi ya Mahakama za Mwanzo na Mahakama Kuu ambao hupatikana kwa mujibu wa Kanuni za Wazee wa Baraza katika Mahakama za Mwanzo
G.N. No. 222/223 za Mwaka 1972, ambao huteuliwa kulingana na sifa za umri na uzoefu walionao katika masuala mbalimbali hasa ya kijamii katika eneo husika.

Aidha, Wazee wa Baraza huwa na jukumu moja la kuishauri Mahakama na ushauri wao hauifungi Mahakama katika kutoa uamuzi inaouona unafaa. Hata hivyo, Wizara yangu imeanza mchakato wa kuboresha sekta ndogo ya mfumo wa haki, jinsia nchini ambao pamoja na mambo mengine inapitia Sheria za Kamati zote ambazo zimetungwa miaka mingi iliyopita ili ziendane na wakati.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya, Sheria ya Usimamizi wa Mahakama ya Mwaka 2011, imebainisha majukumu ya Kamati hizi kwa mujibu wa vifungu vya 50 na 51. Lengo la Kamati hii ni kushughulikia malalamiko ya ukiukwaji wa maadili ya utendaji wa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo na Mahakimu Wakazi katika kutimiza shabaha na kulingana na kusawazishana (checks and balances) katika utendaji wa Mihimili ya dola. Kamati hizi haziingilii uhuru wa Mahakama ambayo inatekeleza majukumu yake ya utoaji haki ambao unatajwa kwa mujibu wa Ibara ya 107 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, ninapenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, nchi yetu itaendelea kuheshimu misingi ya mgao wa madaraka baina ya mihimili ya Dola na kamwe Mahakama haiwezi na haiingiliwi na chombo kingine cha Dola katika utekelezaji wa majukumu yake.