Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 7 Works, Transport and Communication Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 60 2019-04-10

Name

Abdallah Majurah Bulembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Primary Question

MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO aliuliza:-

Mheshimiwa Rais alipofungua Uwanja wa Ndege wa Bukoba alisema kuwa Uwanja wa Kanjunguti hautajengwa tena, badala yake shilingi bilioni tano zilizokusudiwa kutumika huko Omukajunguti ziende kwenye upanuzi wa kiwanja cha Bukoba:-

(a) Je, ni lini Serikali itatekeleza agizo la Mheshimiwa Rais?

(b) Je, Serikali haioni ni tatizo kwa utuaji wa ndege kutokana na hali ya hewa ya eneo hilo?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Alhaj Abdallah Majurah Bulembo, Mbunge wa Kuteuliwa, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa uzinduzi wa kiwanja cha ndege cha Bukoba tarehe 6 Novemba, 2017, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, aliagiza ufanyike uchambuzi wa kina, kama kuna haja ya kujenga kiwanja kipya cha ndege katika eneo la Omukajunguti au kupanua kiwanja cha ndege kilichopo Bukoba, yaani kutoka Daraja la II C hadi Daraja la II C.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na agizo hilo la Mheshimiwa Rais, Serikali iliunda timu ya wataalam ili wafanye uchambuzi wa kina na hatimaye waweze kuishauri Serikali ipasavyo. Baada ya uchambuzi, timu hii ya wataalam ilibaini mambo yafuatayo:-

(1) Kupanua kiwanja cha ndege cha Bukoga kutoka Daraja la II C hadi la III C, kutahitaji utoaji wa ardhi isiyopungua hekari 75 ambayo tayari imeendelezwa. Ardhi hii inayohitajika itagusa nyumba za makazi zipatazo 200, Kituo cha Afya Zamzam, Makanisa mawili (WinnerS Chapel na Pentekoste Assembly of God), Msikiti, Shule za Msingi mbili, Zamzam na Bilele, barabara za Kashozi na Kashai pamoja na kuziba njia ya Mto Kanoni.

(2) Kupanua kiwanda hiki, kutasababisha jengo la abiria kuhamishwa ili kukidhi matakwa ya kiusalama ya usafiri wa anga. Pia kutakuwa na ugumu wa kupata eneo la kusimika taa za kumsaidi rubani kutua.

(3) Kutakuwa na ugumu wa kukiendeleza kiwanja hiki kufikia madaraja ya juu zaidi huko mbeleni.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kubaini mambo hayo, wataalam walitoa ushauri ufuatao kwa Serikali:-

(1) Kwa sasa Kiwanja cha Ndege cha Bukoba hakina eneo la kutosha kwa Daraja la II C, tunakipandisha kwenda daraja la juu, ardhi zaidi itahitajika.

(2) Kwa sasa Kiwanja cha Ndege cha Bukoba kinafaa kusimikwa sehemu ya taa (AGL System) za kukiwezesha kufanya kazi usiku na mchana.

(3) Uongozi wa Mkoa wa Kagera ufanye utafiti wa kina (detail survey) kujua gharama na athari za utoaji wa ardhi inayotakiwa kwa ajili ya upanuzi wa kiwanja ndege cha Bukoba.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Serikali ikiendelea kushughulikia mapendekezo haya ya wataalam, sehemu ya fedha iliyokuwa itumike kulipa fidia kwenye eneo la Omukajunguti, zitatumika kusimika taa katika Kiwanja cha Ndege cha Bukoba ili zisaidie marubani wakati wa uwepo wa hali mbaya ya hewa, pia kukiwezesha kiwanja kutoa huduma usiku na mchana.