Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 3 Sitting 12 Energy and Minerals Wizara ya Nishati na Madini 104 2016-05-04

Name

John Wegesa Heche

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tarime Vijijini

Primary Question

MHE. JOHN W. HECHE aliuliza:-
Mgodi wa North Mara (Acacia Gold Mine) umeanza uchimbaji wa ardhini (underground) sasa yapata mwaka mzima bila kuweka wazi kama kuna mabadiliko ya kimkataba na kitendo hiki ni hatari kwa usalama wa kijiografia kwa wakazi wanaozunguka mgodi huo:-
Je, kwa nini Serikali isizuie zoezi hili mpaka mikataba iridhiwe na Serikali za Kijiji na kuanza upya bila kuwepo makandokando?

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Wegesa Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba uchimbaji wa madini chini ya ardhi (ungerground mining) katika mgodi wa North Mara (Acacia Gold Mine) ulianza mwaka 2015 katika eneo la Gokona baada ya Tathmini ya Kimazingira kufanyika na kibali kutolewa tarehe 23 Aprili, 2015. Aidha, mgodi haukuwahi kuwa na mkataba wa uchimbaji baina yake na vijijii vinavyozunguka eneo hilo. Kifungu cha 48(1)(a) cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 kinamtaka mmiliki wa leseni ya uchimbaji mkubwa (Special Mining Licence) kubadili njia ya uchimbaji madini (mining method) pale inapohitajika kufanya hivyo hasa kwa lengo la kufanya uchimbaji kuwa endelevu kulingana na uwepo wa mashapo na jiografia yake. Mabadiliko hayo ya uchimbaji yalihusisha pia kufanya Tathmini ya Mazingira (Environmental Impact Assessment) zinazoweza kujitokeza wakati wa kutekeleza mabadiliko ya uchimbaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mgodi wa North Mara una mikataba na vijiji saba vinavyozunguka mgodi inayohusu namna ya kunufaika na uwepo wa shughuli za uchimbaji kwenye mgodi huo. Vijiji hivyo ni Kerende, Kewanja, Matongo, Ngenkuru, Nyakunguru, Nyamwanga na Nyangoto. Mikataba hiyo haihusiani kabisa na namna mgodi unavyowajibika katika kutekeleza sheria wakati wa uendeshaji wa shughuli za uchimbaji. Hivyo, mgodi haulazimiki kuomba ridhaa ya Serikali ya Vijiji husika wakati wa kubadili aina ya uchimbaji yaani kutoka mgodi wa wazi kwenda mgodi wa chini ya ardhi. Hata hivyo, pamoja na mgodi kubadilisha aina ya uchimbaji, mikataba yote iliyopo kati ya vijiji hivyo pamoja na wadau wengine itaendelea kuwepo kwa mujibu wa mikataba yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kusimamia uchimbaji huo kwa mujibu wa sheria husika na kuchukua tahadhari ili kuhakikisha kwamba uchimbaji wa madini chini ya ardhi katika mgodi huo hauhatarishi usalama wa wananchi wanaozunguka mgodi huo.