Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 22 Livestock , Fisheries, Agriculture, Food Security and Cooperatives Wizara ya Mifugo na Uvuvi 185 2018-05-04

Name

Susanne Peter Maselle

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SUSANNE P. MASELLE aliuliza:-
Mnamo tarehe 30 Januari, 2017, wavuvi wa maeneo ya Igombe na Ilemela Jijini Mwanza walikamatwa na kunyang’anywa nyavu, mitumbwi na mashine za mitumbwi yao na Maafisa wa Uvuvi wakidai wanatumia nyavu haramu ambazo ni “double” huku Serikali ikitaka watumie “single”:-
(i) Je, Serikali haioni kuwa kuna haja ya kutoa taarifa, elimu na muda kwa wavuvi pindi inapotaka wavuvi wafanye mabadiliko katika shughuli au zana zao za kazi?
(ii) Je, ni lini Serikali itatoa elimu kwa wavuvi wa Igombe na maeneo mengine ya Mwanza kuhusiana na uvuvi wa kutumia nyavu za single badala ya double ili wafanye kazi zao kwa uhuru bila bughudha ya kukamatwakamatwa?
(iii) Je, Serikali inataka wavuvi wavue samaki katika kina kipi cha maji na katika kina cha mita 50 na kuendelea watumie nyavu za mita ngapi kwenda chini?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susane Peter Maselle, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutoa taarifa na elimu kwa wavuvi kuhusiana na usimamizi endelevu wa rasilimali za uvuvi kupitia mikutano, vipindi vya redio na runinga. Pia, leseni za uvuvi huonyesha masharti yanayopaswa kufuatwa ili kuwa na uvuvi endelevu. Kimsingi elimu kwa wavuvi hutolewa kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na wakati wanapopewa leseni na wakati wa kutoa huduma za ugani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kutumia Maafisa Uvuvi wa Idara, Manispaa ya Ilemela na Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) imeendelea kutoa elimu kwa wavuvi wa Igombe na maeneo ya Mwanza juu ya katazo la matumizi ya nyavu za kuunga kwa maana ya double.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi wanaweza kuvua katika tabaka lolote la maji kwa kutumia nyavu zinazoruhusiwa. Isipokuwa hawaruhusiwi kuvua katika maeneo ya mazalia ya samaki na maeneo tengefu. Aidha, katika kina cha mita 50, wavuvi wanapaswa kutumia nyavu zilizoruhusiwa zisizozidi macho au matundu 26 kwenda chini kwa upande wa Ziwa Victoria.