Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 22 Works, Transport and Communication Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 184 2018-05-04

Name

Deogratias Francis Ngalawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Primary Question

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA aliuliza:-
Bandari katika mwambao wa Ziwa Nyasa kutoka moja kwenda nyingine zipo kwa umbali mrefu sana hususan upande wa Wilaya ya Ludewa; hii imekuwa ni kero kubwa kwa sababu hakuna miundombinu ya barabara ambayo ingerahisisha huduma ya usafiri:-
(a) Je, ni lini Serikali itatupatia bandari katika Vijiji vya Nkanda, Nsele, Kyaghomi, Makonde na Yigha?
(b) Je, ni lini huduma za usafiri wa meli zitaanza tena ili kupunguza kero ya usafiri kwa wananchi waishio kandokando ya Ziwa Nyasa?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deogratias Francis Ngalawa, Mbunge wa Ludewa, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ina mkakati wa kuboresha na kujenga miundombinu ya bandari na gati mbalimbali katika Ziwa Nyasa. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali kupitia TPA ilitenga fedha kwa ajili ya kuendeleza Bandari za Mbambabay, Itungi, Kiwira, Ndumbi, Manda, Matema, Liuli na Lupingu Wilayani Ludewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mipango hiyo, bado kuna timu toka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania inafanya usanifu wa awali katika vijiji alivyotaja Mheshimiwa Mbunge vya Nkanda, Nsele, Kyaghomi, Makonde, Yigha na maeneo jirani. Baada ya usanifu wa awali, Serikali itatambua maeneo gani yanafaa kuweka vituo vya kushusha na kupakia abiria na mizigo ili kuwaondolea adha abiria katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali bado inaendelea kumalizia ujenzi wa meli ya abiria itakayotoa huduma katika eneo la Ziwa Nyasa, hivyo tunatumaini wananchi watapata huduma ya usafiri wa meli kabla ya mwaka huu 2018 kwisha.