Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 16 Works, Transport and Communication Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 131 2018-04-24

Name

Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Primary Question

MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Barabara ya Tabora – Mambali – Bukumbi – Shitage - Tulole mpaka Kahama ipo katika mpango wa Serikali wa kujenga barabara za lami nchini:-
(a) Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza?
(b) Kumekuwa na mvutano wa wapi barabara hiyo ingepita baada ya kufika Mambali, mapendekezo ya Bodi ya Barabara ya Mkoa ni kuwa barabara hiyo ipite Bukumbi, Shitage, Tulole na kuunga Kahama; Je, Serikali inatoa msimamo gani baada ya mapendekezo hayo ya Bodi ya Mkoa wa Tabora?
(c) Je, ni lini kipande cha barabara hiyo kitachukuliwa na TANROADS?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ambayo ipo katika mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami ni ya Tabora – Mambali – Itobo - Kagongwa - Kahama yenye urefu wa kilometa 180. Barabara hii ipo katika hatua za mwisho za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambapo kazi ya usanifu inafanywa na Mhandisi Mshauri NIMETA Consult na inatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Julai mwaka 2018. Baada ya kazi ya usanifu kukamilika Serikali itatafuta fedha ili kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kupandishwa hadhi kwa barabara ya Mambali – Bukumbi - Shitage na Tulole tayari sehemu ya barabara ya Mambali hadi Bukumbi yenye urefu wa kilometa 28.5 ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na TANROADS na sehemu ya Bukumbi - Mhulidede kilometa 24.7 imekasimiwa kufanyiwa matengenezo na TANROADS kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Spika, sehemu ya Mhulidede – Tulole kilometa 21 imeanza kuhudumiwa na TANROADS kuanzia mwaka huu wa fedha 2017/2018 na kufanya barabara yote ya Mambali – Bukumbi – Mulidede - Tulole - Kahama kuhudumiwa na TANROADS. (Makofi)