Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 8 Sitting 7 Natural Resources and Tourism Wizara ya Maliasili na Utalii 91 2017-09-13

Name

Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Primary Question

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA (K.n.y. MHE. GOODLUCK A. MLINGA) aliuliza:-
Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano aliahidi kuwapatia wananchi wa Kata za Lupiro, Iragua, Milola na Minepa eneo la ardhi oevu ya Bonde la Mto Kilombero kwa ajili ya makazi na kilimo pindi tu atakapoingia madarakani. Je, utekelezaji wa ahadi hiyo imefikia wapi?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Goodluck Asaph Mlinga, Mbunge wa Jimbo la Ulanga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliahidi kumaliza matatizo ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo maeneo ya kata nne zilizotajwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Ibara ya 22(e). Hata hivyo, utaratibu wa kushughulikia ahadi hiyo katika kata hizo haukutajwa kuwa ni kwa kumega sehemu ya ardhi oevu katika Bonde la Mto Kilombero. Napenda kutumia fursa hii kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari kazi ya kushughulikia tatizo hili la ukosefu wa ardhi kwa wananchi wa kata hizo limeanza kupitia Mradi wa KILORWEMP, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) na kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Serikali ya Mkoa wa Morogoro pamoja na Wilaya za Malinyi, Kilombero na Ulanga.
Mheshimiwa Spika, kazi hii inafanyika kwa umakini mkubwa ili kuepuka kukiuka misingi na dhana nzima ya uhifadhi, kwanza kwa kuzingatia vigezo na umuhimu wa ardhi oevu na pili kwa kuhakiki mipaka halali ya vijiji yaani village approved survey plans. Aidha, kupitia Land Tenure Support Program unaotekelezwa chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji inaandaliwa hadi hatua ya kutoa hati miliki za kimila kwa vijiji vyote vinavyozunguka Bonde la Mto Kilombero.
Mheshimiwa Spika, suala hili pia linafanyiwa kazi sambamba na maombi ya wananchi kupitia wawakilishi wao wakiwemo Waheshimiwa Wabunge na Madiwani ambayo yamekuwa yakipelekwa katika ngazi mbalimbali likiwemo Bunge lako Tukufu. Kazi hii ni shirikishi, wananchi wa kata na vijiji katika Wilaya husika wanashirikishwa kikamilifu hadi kufikia maridhiano ya pamoja. Kwa mfano, katika Kijiji cha Igawa, Kata ya Igawa, Wilaya ya Malinyi, baada ya kufikia maridhiano na kwa kuzingatia vigezo vya pande zote, eneo la kijiji liliongezeka kutoka kilometa za mraba 39.8 hadi 86.97 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 118.5. Eneo la Kijiji cha Sofi Majiji liliongezeka kutoka kilometa za mraba 93.9 hadi ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 16.1. Kuongezeka au kupungua kwa eneo kunatokana na vigezo vilivyowekwa ingawa hadi sasa hakuna kijiji kilichopoteza eneo.