Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 6 Sitting 7 Information, Culture, Arts and Sports Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo 78 2017-02-07

Name

Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapunguzia wasanii gharama
za ukaguzi wa filamu ambapo kwa hivi sasa gharama hizo ni shilingi elfu moja
kwa dakika?
(b) Je, Bodi ya Filamu imejipanga kwa kiasi gani kuhakikisha huduma
zake zinatambulika nchi nzima tofauti na sasa ambapo ni wasanii wachache wa
filamu ndiyo wanafahamu wajibu na majukumu wa Bodi hiyo ambayo hata ofisi
zake hazijulikani ipasavyo sehemu zilipo Jijini Dar es Salaam?

Name

Anastazia James Wambura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi,
Mbunge wa Mafinga Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ada za uhakiki kwa nchi yetu zipo kwa
mujibu wa sheria na kanuni. Gharama hizi hulipwa kwa nakala mama tu (master)
baada ya hapo mtayarishaji huzalisha nakala kwa idadi anayohitaji. Nchi yetu
hutoza ada ambazo ni rafiki ukilinganisha na nchi nyingine. Kwa mfano, Nigeria
ambayo ni nchi iliyopiga hatua kubwa kwa upande wa filamu hutoza filamu
yenye urefu wa dakika 60 ambayo ni filamu ya lugha ya asili kwa naira 30,000
sawa na zaidi ya dola 150 ambayo ni sawa na Sh. 337,950 kwa viwango vya
ubadilishaji vya Sh. 2,253 kwa dola na Kenya ni sawa na Sh.190,000 za Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu hutoza filamu za Kitanzania zenye
urefu wa dakika 60 kwa Sh.60,000 sawa na Sh.1,000 kwa dakika. Gharama hizi ni
asilimia 18 ya zile za Nigeria na asilimia 32 ya zile za Kenya. Kwa maana hiyo, ni
wazi kwamba Tanzania hutoza ada ambayo ni nafuu na rafiki.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Bodi ya Filamu imeendelea kujitangaza
kwa wadau kupitia shughuli mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa. Mfano kushiriki
katika Maonesho ya Sabasaba, Nanenane, Wiki ya Vijana na Kilele cha Mbio za
Mwenge wa Uhuru na Jumuiya ya Afrika Mashariki Utamaduni Festivals. Vilevile
Bodi inatumia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo TBC1, E-FM, Clouds Media,
Gazeti la Mtanzania na kadhalika. Pia Bodi imekuwa ikifanya warsha za
kuwajengea wadau weledi katika masuala ya filamu sehemu mbalimbali
ikiwemo mikoa na wilaya ambapo ni sehemu ya kujitangaza. Aidha, Bodi
inakamilisha tovuti yake ambayo itasaidia kujitangaza na itaendelea kutumia
vyombo vya habari, machapisho na warsha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Bodi za Mikoa na Wilaya ambazo
zinafanya majukumu ya Bodi katika ngazi za Mikoa na Wilaya. Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI itaendelea kuimarisha Bodi za Mikoa na Wilaya ili ziweze
kutoa huduma kwa wigo mpana zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ofisi za Bodi awali zilikuwa Barabara ya
Morogoro, Jengo la Textile ambapo hapakuwa rafiki kwa wadau. Mwaka 2012,
Wizara ilihamisha ofisi za Bodi kwenda Mtaa wa Samora, Jengo la Shirika la
Nyumba, Plot No. 2271/32 ambapo zipo Ofisi za Habari Maelezo mkabala na Tawi
la Benki ya NMB, ghorofa ya kwanza.