Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Question to Prime Minister

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 3 Sitting 23 Questions to Prime Minister Wizara ya Viwanda , Biashara na Uwekezaji 1 2016-05-19

Name

Freeman Aikaeli Mbowe

Gender

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Hai

Primary Question

MHE. FREEMAN A. MBOWE:
Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi ya kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu maswali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu unatambua kwamba sasa hivi nchi ina uhaba mkubwa wa sukari. uhaba huu wa sukari umesababishwa na amri iliyotolewa na Mheshimiwa Rais mwezi Februari mwaka huu ya kuzuia uagizaji wa sukari bila kufuata utaratibu ama kufanya utafiti wa kutosha kuhusiana na tatizo zima ama biashara nzima ya uagizaji na usambazaji wa sukari katika Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunatambua kwamba nchi yetu inazalisha takribani wastani wa tani milioni 300 na zaidi ya tani 180 hivi zinaagizwa kutoka nchi za nje na sasa hivi wewe mwenyewe umetoa kauli kwamba Serikali imeagiza sukari.
Sasa swali langu ni hili; maadam sukari ina utaratibu maalum wa uagizaji ambao unasimamiwa na Sheria ya Sukari ya mwaka nafikiri Sugar Industry Act ya mwaka 2001 na kwamba Bodi ya Sukari inatoa utaratibu maalum wa uagizaji wa sukari hii na biashara ya uagizaji sukari sio tu uagizaji kwa sababu ya fedha ni pamoja na muda maalum, circle maalum wakati gani agizo hili isingane na uzalishaji katika viwanda vya ndani ambavyo Mheshimiwa Rais alidai alikuwa na
nia ya kuvilinda ambalo ni jambo jema.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, sasa unaweza ukatuambia hiyo sukari uliyoagiza umeiagiza kwa utaratibu gani? Anaiagiza nani? Inategemewa kufika lini? Ni kiasi gani? Na itakapofika haitagongana na uzalishaji katika viwanda vyetu local baada ya kuisha kwa msimu wa mvua na hivyo kusababisha tatizo la sukari kwa mwaka mzima ujao?

Name

Kassim Majaliwa Majaliwa

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Answer

WAZIRI MKUU:
Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbowe, Mbunge wa Hai na Kiongozi wetu wa Kambi ya Upinzani kwa kuuliza swali hili kwa sababu tulitaka tutumie nafasi hii kuwaondoa mashaka Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wakati wote anapotoa tamko ni kutokana na mwelekeo na mpango wa Serikali ambao umepangwa kwa lengo maalum. Sukari nchini ni k
weli kwamba inaratibiwa na Bodi ya Sukari ambayo pia imewekwa kisheria na moja kati ya majukumu yao kufanya utafiti, lakini pia kusimamia viwanda vinavyozalisha kwa lengo la kusambaza sukari nchini na iweze kutosha.
Mheshimwia Spika, kwa miaka mitatu, minne ya nyuma, sukari imekuwa ikiletwa kwa utaratibu ambao baadaye tuligundua kwamba unavuruga mwenendo wa viwanda vya ndani na viwanda vya ndani havipati tija. Kwa hiyo, Serikali hii ilipoingia madarakani moja kati ya mikakati yake ni kuhahakikisha kwamba viwanda vya ndani vinalindwa, unavilindaje? Ni pale ambako sasa sukari inayoingia ndani lazima idhibitiwe lakini pia kuhamasisha viwanda hivyo kuzalisha zaidi sukari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mahitaji ya sukari nchini ni tani 420,000. Sukari ambayo inazalishwa nchini ni tani 320,000 na upungufu ni kama 100,000 hivi. Tani 100,000 hii kama hatuwezi kuiagiza kwa utaratibu na udhibiti mzuri kunaweza kuingia kwa sukari nyingi sana kwa sababu kwenye sukari tuna sukari za aina mbili, sukari ya mezani ile ambayo tunaitumia kwenye chai na sukari ya viwandani na haina utofauti mkubwa sana kwa kuingalia na sukari ya viwandani na ya
mezani ni rahisi sana kwa mwagizaji kama hatuwezi kudhibiti vizuri unaweza kuleta sukari nyingi ya mezani halafu kukajaa sokoni.Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kauli ya Mheshimiwa Rais ni katika mpango wa kulinda viwanda vya ndani kama ambavyo umekiri, lakini jukumu la Bodi sasa ya Sukari baada ya kauli ile inatakiwa sasa iratibu vizuri. Kwa hiyo, sukari imeratibiwa vizuri na bodi ya sukari na mahitaji ya sukari ile ya tani 100,000 na
mahitaji ya sukari ambayo inatakiwa kuingia ili isivuruge uzalishaji ujao ni kazi ambayo inafanywa Bodi ya Sukari.

Additional Question(s) to Prime Minister

Name

Freeman Aikaeli Mbowe

Gender

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Hai

Question 1

MHE. FREEMAN A. MBOWE:
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu nakushukuru kwa ajibu yako na ninaomba nikuulize maswali mengine machache ya ziada.
Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na nia njema sana ya kulinda viwanda
vya ndani ni dhahiri kwamba maamuzi yote ya kiutawala lazima yafanyiwe kwanza utafiti. Na tunapozungumza ninahakika Serikali yako inatambua kwamba kuna mradi mkubwa wa uwekezaji wa kiwanda cha sukari uliokuwa umependekezwa katika eneo la Bagamoyo uliouzungumza ambao umeanza kuratibiwa tangu mwaka 2006 wenye capacity ya kuzalisha sukari tani 125,000 kwa mwaka, lakini Serikali mpaka dakika hii tunapozungumza urasimu unasababisha mradi huu haujapewa kibali cha kuanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu, pamoja na kwamba ulisema kuna bei ya
elekezi sukari ambayo ingehitaji soko la sukari liweze kuwa controlled na Serikali, jambo ambalo linaonekana kushindikana. Unatupa kauli gani Watanzania kuhusiana sasa na hatima ya hayo mambo niliyokuuliza?

Name

Kassim Majaliwa Majaliwa

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Answer

WAZIRI MKUU:
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali pana la Mheshimiwa Mbowe, Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kama ifuatavyo:-
Kwanza tuna hilo shamba la Bagamoyo ambalo umelisema ambalo
umesema kumekuwa na urasimu wa muda mrefu. Nataka nijibu hili vizuri kwa sababu pia Wabunge tumeshirikiana nao sana katika kufanya maamuzi ya shamba lile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, shamba la Bagamoyo kwa ukubwa wake na
mategemeo yake kwa mipango ya kuzalisha sukari inategemea sana Mto Wami. Mpakani mwa Mto Wami tumepakana na Mbuga ya Saadani, Mbuga ya Saadani uwepo wake na sifa iliyonayo inategemea sana wanyama wale kunywa maji Mto Wami. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, uwekezaji wa shamba la sukari unahitaji maji mengi nayo yanatakiwa yatoke Mto Wami. Bado kuna mgongano kidogo wa mpaka kati ya shamba letu hilo la sukari linalotegemewa kulima miwa na Mbuga ya Saadani. Kamati ya Kudumu ya Bunge imefanya ziara na imeishauri Serikali kuangalia vinginevyo na mimi nimepokea ushauri wao vizuri kwa sababu una mantiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Kamati ya Bunge imeishauri Serikali kwamba ni vyema
tukahifadhi mbuga, tukatafuta maeneo mengine ya kilimo cha sukari ili kulinda Mto Wami ambao unatumiwa na wanyama wetu kwenye Mbuga ya Saadani kuliko kupeleka shamba tukatumia maji yale tukafukuza wanyama hakutakuwa na mbuga tena.
Mheshimiwa Spika, sisi bado tuna nafasi kubwa ya maeneo mengi ambayo yamefanyiwa utafiti ya kulima sukari, mbali ya eneo la Morogoro na kule Kigoma, lakini tuna eneo la shamba lililokuwa linamilikiwa na Bodi ya Sukari kule Kilombero, nalo pia lina nafasi nzuri tu tunaweza kuzungumza na wakulima wanaolima mashamba ya kawaida watuachie tuweze kuwekeza.
Mheshimiwa Spika, lakini tuna Mto Rufiji tuna bonde kubwa sana uliokuwa
unamilikiwa na watu wa Bonde la Rubada, wana eneo kubwa sana. Kwa hiyo, tuna maeneo hayo mengi, tutakapopata wawekezaji wengi tutaanza kupima viwanda vilivyopo na uzalishaji wake. Makubaliano ya kiwanda kipya na uzalishaji wake tukigundua kwamba, uzalishaji wake unatosha mahitaji ya nchi.
Tutaanza kuwakabidha Kigoma, tutawepeleka Morogoro kule Kilosa, tutawapeleka hapa Ngerengere na Bagamoyo iwe sehemu ya mwisho baada ya kuwa Kamati ya Bunge imetushauri vizuri juu ya kulinda Mbuga yetu ya Saadani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la pili, ambalo umelitaja ni hili la bei elekezi, kwa
nini tunatoa bei elekezi.
Mheshimiwa Spika, mara nyingi tunakaa sana na wazalishaji wa viwanda
wa sukari na kufanya mapitio na kwa mara ya mwisho tumekutana hata wale waagizaji wa muda mrefu na sasa tunajua kupitia mitandao tunajua bei wanayonunulia sukari huko ughaibuni. Brazil na kule Uarabuni tumeshafanya calculation za pamoja mpaka sukari inaingia nchini na kulipa kodi zake.
Mheshimiwa Spika, usafirishaji kutoka Dar es Salaam na kuipeleka mpaka
mkoa wa mwisho Kagera, Lindi, Ngara, tunajua kule Ngara itauzwa bei gani.
Kwa hiyo, wajibu wa Serikali kutoa bei dira ni kumlinda sasa mwananchi wa kawaida asije auziwe kwa gharama kubwa kwa kisingizio cha usafirishaji huku tukiwa tunajua usafirishaji kutoka Brazil mpaka Dar es Salaam, Dar es Salaam mpaka Ngara na mwananchi wa Ngara atanunua sukari kwa kiasi gani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo suala la bei elekezi litategemea linaweza
likabadilika kutegemea na gharama ya usafirishaji ambayo na sisi pia tunafuatilia kwa karibu kupitia Bodi yetu ya Sukari. Kwa hiyo, suala bei dira linaweza kubadilika na sisi tunatoa kauli kutegemea na uagizaji lakini lazima wananchi waamini kwamba Serikali hii inawalinda walaji wadogo ili wasinunue sukari kwa bei ya juu.