Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon Tamima Haji Abass (3 total)

MHE. TAMIMA HAJI ABASS aliuliza: -

Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kutoa elimu kwa jamii dhidi ya udhalilishaji na ukatili wa watoto?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tamima Haji Abass, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kupitia mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili kwa wanawake na Watoto, Serikali imeunda Kamati za Ulinzi wa Watoto na kuandaa vijarida na vitini vya kutoa elimu katika jamii kuhusu madhara ya ukatili, vyombo mbalimbali vya habari vinatoa vipindi vya kitaalamu kuhusu haki na ulinzi wa mtoto pia elimu ya athari za ukatili; walimu wa malezi na unasihi wamepata mafunzo ya kutoa elimu ya ulinzi wa watoto kwa walimu wenzao na wanafunzi; pia kupitia viongozi wa kijamii walio sehemu ya kamati ya jamii kwa kushirikiana na maafisa maendeleo, ustawi na elimu wanatumika katika kubadili mitazamo na fikra hasi za jamii, ahsante.
MHE. TAMIMA HAJI ABASS aliuliza: -

Je, kuna utafiti uliofanywa na Serikali kujua sababu za uwepo wa Watoto wa mitaani?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wananwake na Makundi Maalum napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tamima Haji Abass, Mbunge wa Viti Maalum) kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017/2018 ilifanya tafiti katika Mikoa ya Dar es salaam, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Arusha na Iringa ili kubaini idadi na sababu za watoto kuishi na kufanya kazi mitaani ambapo walibainiwa jumla ya Watoto 6,393 (wavulana 4,865, wasichana 1,528). Vilevile, mwaka 2020/2021 Serikali ilirudia utafiti katika maeneo hayo na kubaini kuwa idadi ilipungua hadi watoto 4,383 (wavulana 3,508 wasichana 875).

Mheshimiwa Spika,miongoni mwa sababu zilizobainiwa ni pamoja na, malezi duni, yatima, migogoro kwenye familia, shinikizo la makundi rika, ukatili na unyanyasaji nyumbani, umasikini wa kipato katika familia na utumikishaji wa watoto mijini, ahsante.
MHE. TAMINA HAJI ABASS aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kukarabati nyumba za makazi ya Askari Polisi Kaskazini Unguja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tamina Haji Abass, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tathmini kwa ajili ya ukarabati wa nyumba zote 14 za makazi ya askari polisi katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, imefanyika na kiasi cha shilingi 447,065,000 zinahitajika. Fedha hizo zinatarajiwa kutengwa kwenye Bajeti ya Serikali ya 2024/2025, ahsante.