Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Husna Juma Sekiboko (3 total)

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Wizara ya Mambo ya Ndani, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia katika maeneo mengi, Jeshi la Polisi limeshindwa kufika kwa wakati kwenye matukio kwa sababu za kukosa mafuta na matengenezo ya magari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ustawi wa jamii yetu unategemea sana ulinzi na usalama unaofanywa na Jeshi letu la Polisi. Swali la kwanza, je, Wizara haioni sasa ni wakati muafaka wa kufanya marekebisho hayo ya kisheria?

Mheshimiwa Spika, pili, Wizara haioni ni muda muafaka sasa kupeleka hizo fedha moja kwa moja kwa Wakuu wa Polisi wa Wilaya badala ya kupitisha kwa Wakuu wa Polisi wa Mikoa ambapo imetengeneza urasimu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Husna Sekiboko, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza amesema kwamba hatuoni haja ya kufanya mabadiliko ya sheria hii? Mabadiliko ya sheria siku zote yanakwenda na mahitaji. Inawezekana ikawa kuna hitaji la kufanya hivyo, lakini sheria hii ikawa iko hivi hivi mpaka tufike wakati tuone namna ambavyo tunaweza kufanya mabadiliko ya sheria hii.

Mheshimiwa Spika, nataka kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba ukiangalia Sheria ya Bajeti, kuna kitu kinaitwa vote holder na kuna kitu kinaitwa sub-vote holder. Sasa vote holder moja kwa moja anayo IGP na sub- vote holder anayo RPC. Kwa hiyo, fungu likitoka kwa IGP linakuja kwa RPC. Huo ndiyo utaratibu halafu sasa ndiyo zinagawiwa Wilaya husika kama ambavyo tumeeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama sasa inafika wakati tunahitaji mabadiliko ya sheria hii, basi acha tulichukue hilo tukakae na wadau halafu tuone namna ambavyo tunaweza tukalifanyia mabadiliko. Kwa sababu, suala la kufanya mabadiliko ya sheria is a matter of procedure… (Makofi)

SPIKA: Unajua Waheshimiwa Wabunge huwa mnapiga makofi ambapo hamjui hata mnapiga makofi ya nini? (Kicheko)

Ahsante, malizia kujibu. Umemaliza eeh!

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Ndiyo.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mpango mzuri wa kuwawezesha wanafunzi hao ambao wameshindwa kufaulu mitihani ya darasa la saba na kidato cha tano, lakini ikumbukwe kwamba wanafunzi tunaowazungumzia ni wale ambao wazazi wao wameshindwa kulipa ada ya 20,000 na kwa maana hiyo Serikali imewapa elimu bila malipo. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha mafunzo maalum ya bure kupitia Mfuko wa Uwezeshaji wa Vijana chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili wanafunzi hao ambao wanashindwa mitihani na wanarudi nyumbani na kuwa tegemezi kwa taifa waweze kupata mafunzo hayo na hatimaye waweze kujiajiri? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tunayo Idara ya Elimu ya Watu Wazima lakini idara hii haijafanya vizuri kwa muda mrefu. Kutokana na wahitimu kuongezeka sababu ya mpango wa elimu bila malipo nchini wanafunzi wengi wanahitaji kupata elimu hii ya ziada. Je, Serikali sasa ipo tayari kutoa elimu ya watu wazima bure ili kuwawezesha wanafunzi ambao wanashindwa mitihani ya kidato cha nne na darasa la saba kupita kwenye mfumo huu ambao siyo mfumo rasmi wa elimu nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Husna, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani maswali yote aliyouliza Mheshimiwa Husna ni mapendekezo ambapo anapendekeza kwa jinsi yeye anavyofikiri. Kwa hiyo, naomba maswali hayo yote mawili kwa pamoja tuyachukue na tuweze kwenda kuyaongeza kwenye mipango pamoja na Sera yetu ya Elimu na kuweza kuangalia namna gani ya kufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, nikirejea swali la Mheshimiwa Mbunge na hasa ushauri wake, kupitia Programu ya Ukuzaji Ujuzi ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, alikuwa anafikiri kwamba Vyuo hivi vya Maendeleo ya Jamii vingeweza pia kutumika kuwafundisha na kuwasaidia vijana kukuza ujuzi katika skills ambazo zinatumika kwenye mazingira husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba program hizo zinaendelea na Serikali imekwisha kutenga bajeti kwa mwaka wa fedha 2021/2022 tutaendelea kutenga hiyo bajeti lakini kwa mwaka wa fedha 2020/2021 tayari tunavyo Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, ambavyo mwezi huu wa nne vitaanza kutoa mafunzo ya ujuzi kwa vijana, kuwasaidia vijana kuweza kupata ujuzi katika maeneo mbalimbali, lakini asilimia kubwa ya malipo ya ujuzi huo yatagharamiwa na Serikali. Tutakwenda kuangalia vyuo vyote ambavyo vinaweza kutoa mafunzo hayo, tutafanya tathmini yake kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, kuona vile ambavyo vina uwezo wa kufanya kazi hiyo tutaendelea kuvijumuisha kwenye mpango na vitaendelea kutoa mafunzo hayo na kuwafikia vijana wengi wa Tanzania kwenye programu hiyo maalum ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili ufaulu mzuri uweze kupatikana inategemea sana mazingira ya kujifunzia na kufundishia hasa ikama nzuri ya walimu.

Je, Serikali haioni kwamba sio haki kuwashindanisha au kushindanisha Halmashauri za Mjini na Vijijini ambako kuna mazingira magumu ya kujifunzia na kufundishia na kuna uhaba mkubwa wa walimu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Serikali haioni ni wakati sahihi sasa kutazama upya vigezo hivi vya kuzingatia katika kupanga madaraja haya ya ufaulu kwa kuwa kwa kuzingatia maeneo hayo ya mjini na vijijini ambako shule za vijijini zina mazingira magumu sana ya kujifunza na kufundishia ukilinganisha na shule za mjini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sekiboko kwa niaba ya Mheshimiwa Shangazi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba tuna changamoto kubwa ya walimu kwenye shule zetu na mwaka jana mwezi Novemba, Serikali kupitia Wizara ya TAMISEMI ilifanya uajiri wa walimu zaidi ya 8,000 na maeneo makubwa ambayo yali-focus au walipelekwa walimu wale ni maeneo ambayo yenye changamoto kubwa sana ya walimu hasa hasa kule vijijini na maeneo ya pembezoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa suala la ikama ya walimu nipende tu kusema kwamba Serikali bado tunafanyia kazi, kuna walimu wengine zaidi ya 5,000 ambapo kupitia Wizara ya TAMISEMI tunaratajia hivi punde walimu hao watasambazwa kwenye maeneo hayo ili kuweza kusawazisha ile ikama na kuondoa changamoto hii ya upungufu wa walimu kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la utaratibu wa madaraja, utaratibu huu wakupanga madaraja katika ngazi ya shule na kwa wanafunzi wetu imezingatia vigezo vya kitaifa, kikanda na kimataifa. Kwa hiyo tukisema kwamba leo hii tuweze kubadilisha vigezo hivi kwa sababu tu kuna shule ambazo hazina ikama ya walimu itakuwa hatutendei haki kwenye eneo letu hili la kutoa elimu kwa vijana wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nadhani eneo kubwa la kujikita ni pale kwenda kuhakikisha kwamba ikama ya walimu inapatikana, lakini kwa upande wa vigezo hivi vilivyowekwa imezingatia sana ubora wa elimu yetu na katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa. Naomba kuwasilisha.