Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Gibson Blasius Meiseyeki (5 total)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Meiseyeki, swali la nyongeza.
MHE. GIBSON B. MEISEYEKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi yetu tukizungumzia hasa mifugo, ng‟ombe hawa wa nyama ni aina ile ambayo inachukua muda mrefu sana kumtunza ng‟ombe kufika angalau kilo 100 unaweza kuchukua karibu miaka minne au mitano ng‟ombe kufikisha kilo 100. Sioni commitment ya Serikali hapa hasa ukilinganisha kwa hii bei ambayo wameitaja hapa shilingi laki nane kwa milioni moja kwa mtamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii bei ni kubwa sana na sidhani kama, labda naomba ku-declare interest, mimi ni mfugaji na ni mkulima pia. Hii bei ya shilingi 800,000/= na shilingi 1,000,000/= ndiyo bei iliyoko sokoni, sasa kuambiwa kwamba hii ndiyo bei yenye ruzuku sitakubaliana na hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kupata commitment ya Serikali katika kubadilisha hasa aina ya mifugo tuliyonayo, ni lini Serikali itakuja na bei ambayo ni affordable kwa wakulima wetu ili tuweze kubadilisha mbegu hizi za hawa ng‟ombe ambao wanachukua muda mrefu kuongeza uzito?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, ni Tanzania ndiyo nchi pekee duniani ambayo maziwa ni rahisi kuliko maji ya kunywa, ni lini Serikali itakuja na bei elekezi ya lita moja ya maziwa ya ng‟ombe ili iweze kuwa na tija kwa wafugaji ambao wanahangaika sana na mifugo, lakini hawapati chochote kutokana na nguvukazi yao hiyo na pengine inaweza kuwahamasisha vijana zaidi kushiriki kwenye ufugaji. Ni lini Serikali itakuja na bei elekezi ya lita moja ya maziwa fresh ya ng‟ombe ili wakulima wetu waweze kupata tija?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kwa bei ya sasa ya mitamba inaonekana kwamba iko juu, lakini kama nilivyosema ukilinganisha na bei iliyoko kwenye soko bado kuna ruzuku.
Kama nilivyosema tofauti inafikia kwenye mitamba yenye ruzuku ya Serikali ni kati ya shilingi 800,000/= na 1,200,000/= wakati kwenye soko inafikia kati ya 1,2000,000/= hadi 2,300,000/=. Kuna tofauti hapo, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha kwamba bei hii inashuka ili wafugaji wengi waweze kumudu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tunamshauri Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wabunge wengine, tujaribu kutumia huduma za uhimilishaji kwasababu zinakuwa bei yake ni afadhali zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu bei elekezi, bei ya maziwa kama bidhaa nyingi nchini kwetu zinaamuliwa na kanuni za soko. Tunachoweza kusema ni vigumu kuweka bei elekezi lakini tunachofanya kama Serikali ni kujaribu kuweka mazingira mazuri ya uchakataji wa maziwa, kujenga viwanda ili bidhaa za maziwa ziweze kupata bei.

WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Kilimo, Ufugaji na Uvuvi, napenda niongeze jibu moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kujenga uchumi wa viwanda na tuwe shindani lazima mazao ya chakula yawe ya bei nafuu. Kwa hiyo, wakulima wanaofuga ng‟ombe, wajibu wa Serikali ni kuwawezesha ili bei ya maziwa iwe chini, bei ya chakula iwe chini, wafuge na kuzalisha kwa tija kusudi uwekezaji Tanzania uwe nafuu, viwanda vya dunia nzima vije Tanzania. Nawapongeza wakulima wa maziwa na bajeti yetu itawasemea.
MHE. GIBSON B. OLE-MEISEYEKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa matokeo ya utekelezaji kazi wa Wakala hawa wa Serikali imekuwa tofauti kabisa na makusudio ya uundwaji wa sheria hizi, nikiwa na maana kwamba vyombo hivi vinaisababishia Halmashauri na Taasisi za Serikali usumbufu mkubwa wa ucheleweshaji wa utengenezaji wa mitambo lakini pia gharama kubwa za utengenezaji wa mitambo hiyo ukilinganisha na bei zilizoko kwenye masoko ya kawaida. Kwa mfano, TEMESA haina kabisa karakana na wataalam wa kutengeneza mitambo yetu hii, kwa maana hiyo Wakala hawa wamekuwa kama kupe wa kufyonza fedha za Serikali badala ya kuisaidia Serikali kuweza kutengeneza miradi kwa gharama nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliuliza kwenye swali langu la msingi kwa nini isifanyiwe marekebisho ya utekelezaji wao wa kazi ili sasa iweze kuleta tija na maendeleo ya haraka katika maeneo yetu badala ya kuweka vyombo ambavyo vinasababisha gharama kubwa katika utekelezaji wake wa kazi. Kwa hiyo, swali langu linabaki pale pale, kwa nini Serikali isibadilishe utaratibu wa utekelezaji kazi wa mamlaka hizi ili kuweza kuleta tija na ku-save fedha badala ya kusababisha gharama kubwa mara mbili, tatu ya gharama sahihi zilizoko mitaani? Kwa nini utaratibu wa utekelezaji wake wa kazi usibadilishwe? Ahsante (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa Mheshimiwa Mbunge nikuambie mimi nimeitumia TEMESA, nilikuwa Meneja wa TANROADS na nilikuwa Wizara ya Ujenzi, kwa hiyo TEMESA naielewa vizuri kwa undani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, amesema kwamba TEMESA imekuwa na usumbufu, gharama kubwa na ucheleweshaji, hayo anayoyazungumza ni kweli. Ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimesema kwamba TEMESA sasa hivi uongozi umebadilishwa na karakana zilizopo zinaboreshwa kwa kuwekewa vifaa vilivyo bora. TEMESA ilikuwa na shida ya namna ya kutumia sheria mliyoiunda ninyi Wabunge ya PPRA, sasa hivi wamewekwa wataalam ambao wataitumia ile sheria vizuri. Sheria ni nzuri sana lakini kulikuwa na wafanyakazi ambao sio waadilifu na Serikali hii ya Awamu ya Tano imechukua hatua ya kuhakikisha kwamba inawaondoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge wazo lake la kusema chombo hiki kwa sasa kibadilishwe, ukianza kuunda kingine leo utaanza tena kuwafundisha mpaka wafike huko watakakofika. Sasa hivi hawa tayari wameshaiva, tunahakikisha wanaboreshwa ili TEMESA iwe na ufanisi mzuri kuliko garage nyingine yoyote ya kawaida. Naomba atupe muda na tushirikiane tuendelee kutekeleza suala hili.
MHE. GIBSON B. MEISEYEKI: Mheshimiwa Spika, nimpe pole Waziri kwa kupata shida kidogo na majina.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na mkwamo mkubwa wa miradi ambayo Mheshimiwa Waziri ameitaja mingine hapa kutokana na urasimu wa malipo ya certificate kwa wakandarasi ambao wapo site. Miradi mingine imekwama kwa zaidi ya mwaka mmoja, mingine karibu miwili. Ni lini urasimu huu utakwisha ili miradi hii iweze kukamilika na kuwaondolea wananchi taabu hii ya maji ambayo imekuwa ni ya muda mrefu?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, Kata zangu mbili za Odonyosambo na Odonyoas, wananchi kule wanataabika kwa kutumia maji yenye madini mengi, kwa maana hiyo wanapinda miguu na kuharibika kinywa nikiwa na maana meno yanaharibika kutokana na maji hayo na kwa sababu kuna chanzo ambacho Wilaya ya Longido wameki-abandon, wamepata chanzo kingine, ni lini Wizara sasa itaanza kuratibu kuwapelekea watu hawa ambao wanataabika kwa maji haya machafu ili kuwanusuru maisha yao na wananchi wengine waliopo pembezoni mwao waweze kufaidika na maji? Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nishukuru kwa maswali yake mazuri, lakini kikubwa ambacho nataka nilieleze Bunge lako Tukufu; sisi kama Serikali tumekuwa na utaratibu mpya wa kuhakikisha kwamba hatupeleki fedha tu, kwamba tunajiridhisha namna mkandarasi alivyofanya kazi kwa yeye ku-raise certificate, lakini kunakuwa na muda maalum, halmashauri inajiridhisha, mkoa unajiridhisha na sisi kama Wizara tunajiridhisha kazi bora iliyofanywa na mkandarasi.
Mheshimiwa Spika, lakini katika kipindi hiki cha uvumilivu au cha kusubiri, yawezekana akaona kama kuna suala la urasimu, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama kuna certificate ambayo imekuwa-raised na inahitaji kulipwa, baada ya Bunge naomba tukutane katika ofisi yangu ili tuhakikishe kwamba tunawasimamia ili wananchi wa Arumeru Magharibi waweze kupata maji ya uhakika na salama kama lengo la Serikali ilivyokuwa imepanga…
Mheshimiwa Spika, katika swali la pili amezungumzia suala zima la wanachi kupinda mifupa kutokana na fluoride. Sisi kama Serikali lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata maji, si maji tu, ni maji safi na salama. Kwa hiyo, sisi kama Serikali tumetengeneza maabara pale Arusha kuangalia teknolojia ambayo tunaweza tukapunguza fluoride, lakini pia kama Wizara tumejipanga kuangalia namna gani tunapata vyanzo vyenye mserereko ili visiwe na fluoride ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanakuwa salama na wanakuwa na afya bora. Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwanza hatudaiwi senti tano kutoka kwenye halmashauri yake, fedha zote tumeshalipa.
Mheshimiwa Spika, pili, tunaendelea kuhakikisha kwamba tuna-tap maji kutoka Mlima Meru na kuwapelekea wananchi wake na kwamba hadi sasa hakuna mwananchi hata mmoja anayeteseka kwa kukosa maji yaliyo safi na salama. (Makofi)
MHE. GIBSON B. OLE MEISEYEKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nirekebishe jina langu tu naitwa Gibson Blasius Ole Meiseyeki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni kulikuwa na zoezi la ubomoaji uliofanyika katika shamba la Mheshimiwa Mbowe katika Wilaya ya Hai. Je, ofisi yako ilibariki tukio hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa, Arumeru Magharibi kuna mashamba mengi ya wawekezaji ambayo kiuhalisia yamejengwa kwenye maeneo ambayo pia ni vyanzo vya maji na wananchi wanakusudia kwenda kuisaidia Serikali kuondoa mashamba hayo ambayo kimsingi yanaharibu vyanzo vyetu vya maji. Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusiana na nia hii ya wananchi ya kuyaondoa mashamba yote ambayo yako kwenye maeneo ambayo hayaruhusiwi kwa mujibu wa taratibu. (Makofi.) Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –TAMISEMI naomba kujibu swali la ndugu yangu Gibson, naomba niishie hapo hapo huko mbele majina ya kimasai yasije yakanichanganya zaidi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama suala la kubariki zoezi lililofanyika Katamba katika shamba la Mheshimiwa Mbowe, kwa sababu hili jambo ni specific sana na sijajua harakati za pale, sitaki kulitolea comment katika hilo. Naomba nizungumze hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu wananchi wapo tayari sasa kushirikiana na Serikali, kuhakikisha kwamba inashirikiana vizuri kwenda kuondoa wale wananchi au mashamba yaliyopo katika eneo husika. Tukifanya rejea jana kulikuwa na mkutano mkubwa sana wa Waziri wa Mazingira na wadau kule katika Mkoa wa Iringa. Bahati nzuri niwashukuru baadhi ya Wabunge hasa katika Mkoa wa Iringa walikuwa katika mkutano ule, kuna mambo mahsusi yalijadiliwa katika suala la hivi vyanzo vya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo yangu ni kwamba Wakurugenzi wote wameelekezwa utaratibu wa kufuata sasa katika vyanzo hivi vya maji. Imani yangu kubwa wazo hilo lake lililokuwa jema na kwa sababu tuna timu kule katika ngazi ya Mkoa na katika ngazi za Halmashauri, ukichukua na combination ya mawazo mazuri ya mkutano wa jana uliofanyika katika Mkoa wa Iringa, naamini litaenda kufanyika jambo sahihi kwa mujibu wa taratibu jinsi hali halisi ilivyo kule katika Mkoa wa Arusha hasa Arumeru.
MHE. GIBSON B. OLE MEISEYEKI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nimekuwa nikisubiria majibu ya swali hili kwa miaka mitatu sasa, lakini majibu niliyopewa siyo ya barabara ambazo Mheshimiwa Rais aliziahidi. Rais alipokuwa anaomba kura mwaka 2005 alitoa ahadi ya kilomita 12 ya bararaba inayoanzia Ngaramtoni kupitia hospitali ya Selian mpaka kwa Luhiyo kilomita 12. Alipochaguliwa 2012 akatuongeza barabara nyingine inayokwenda Hospitali ya Oltrumeti. Barabara zote hizi hazina lami mpaka sasa. Je, ni lini sasa Serikali itapata fedha ili iweze kuteleza ahadi hiyo ya Rais kwa barabara hizo ambazo alituahidi hizi nyingine alizozisema Mheshimiwa Waziri hazihusiani na swali langu?

Mheshimiwa Spika, pia ametaja kwamba barabara ya Sarawani inatengenezwa, ni kweli, lakini imekuwa ikitengenezwa kilomita 0.8 kwa takriban mwaka mzima sasa haijakamilika. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuongoza na mimi kwenda Arumeru Magharibi tukaangalie maendeleo na ubora wa barabara hii ya Sarawani - Oldonyosapuk ambayo kwa zaidi ya mwaka mzima inatengenezwa na bado haijakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, nilikuwa na wasiwasi kwamba Mheshimiwa Mbunge angesema barabara hizi hazijaja kwenye jimbo lake lakini na yeye tunakubaliana kwamba barabara hizi zimejengwa kwenye jimbo lake, kwa hiyo, naamini kuwa Mheshimiwa Mbunge ana kila sababu ya kuipongeza Serikali kwa kujenga barabara hizo ndani ya jimbo lake.

Mheshimiwa Spika, lakini naomba niendelee kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi ambazo tumetoa ni ahadi thabiti na kwa kadri uhitaji wa wakati unavyoruhusu ndio tunaenda kwenye barabara hizo. Kwa hiyo naomba nimhakikishie kwamba ahadi za Rais wetu aliyetangulia ambaye sasa amepokea kijiti Rais tuliyenayo bado ni ahadi za CCM, tutazitekeleza kwa kadiri bajeti itakavyoruhusu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anaomba fursa nikatazame hiyo barabara ambayo imekuwa ikitengenezwa ya kilomita 0.8, nalo ni jambo la kushukuru kwa sababu angeniambia kuwa haijaanza kutengenezwa kabisa then hata kuongea kwake ingekuwa tofauti. Naomba nimhakikishie kwa kadiri ratiba itakavyokuwa inaruhusu mimi nipo tayari kuambatana naye.