Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Suma Ikenda Fyandomo (2 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi uliyonipatia ya kuweza kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais. Awali ya yote nipende kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye amenijaalia uzima na afya njema hatimaye nimekuwa mmoja wa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwashukuru sana wanawake wa Mkoa wa Mbeya kwa namna ambavyo wamenipatia kura nyingi ambazo zilisababisha jina langu kupelekwa kwenye Kamati Kuu Taifa. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu ambaye ndiyo Mwenyekiti wetu wa Chama Cha Mapinduzi Taifa. Namshukuru yeye pamoja na Kamati Kuu kwa kupendekeza jina langu nami nimekuwa Mbunge sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nikupongeze wewe kwa kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini. Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu hongera sana kwa kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini na Mbeya Mjini sasa imetulia kama lilivyo jina lako. Napenda vile vile kuwashukuru sana wananchi wa Mbeya Jiji na wananchi wa Mkoa wa Mbeya wote kwa ujumla kwa namna ambavyo waliweza kukichagua Chama Cha Mapinduzi kwa kura nyingi za heshima. Napenda kuwashukuru Watanzania wote kwa ujumla. Tanzania yetu sasa inapendeza, imekuwa ni ya kijani na ina amani ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi kubwa nzuri anazozifanya ambapo Tanzania yetu sasa inatambulika dunia nzima na inaheshimika dunia nzima kwa namna anavyoleta maendeleo kwenye nchi yetu. Nawapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa nafasi zao hizo. Natambua ni watu makini na ni mahiri sana watazitendea haki kwa maana ya kuisaidia Serikali ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Mbeya katika kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais, namshukuru sana Mheshimiwa Rais alisema kwamba kwenye hotuba ile atavipa vipaumbele sana vikundi tofauti tofauti kwenye mikopo kwa maana ya kwamba viendelee kusonga mbele. Naomba sana Mheshimiwa Rais kwa hotuba hii awape kipaumbele wanawake wa Mkoa wa Mbeya na Tanzania yote kwa ujumla, maana akiwezeshwa mwanamke, mwanamke ndiyo kila kitu, mwanamke ndiyo mama ambaye anajali familia, anasaidia Watoto, anamjali hata baba pia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuomba asilimia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kengele imenikatili, lakini nitaandika kwa sababu napenda sana kuongelea habari za wanawake namna gani waweze kusaidiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikupongeze wewe kwa kazi nzuri na namna ambavyo unaliongoza Bunge hili Tukufu. Pia nimpongeze Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa vile ambavyo anasimamia Kanuni hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi imara wa Mheshimiwa wetu, Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna ambavyo ameweza kufanikiwa kuingia katika uchumi wa kati kabla ya kipindi kilichokuwa kimetazamiwa. Kwa namna ambavyo tumeweza kuingia kwenye uchumi wa kati Benki ya Dunia wameshangazwa na kasi ya Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, naomba kuishauri Serikali iendelee kuweka mkazo kwenye Halmashauri zetu ili ziweze kuwekewa fedha za kutolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili wawe kuendesha maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kufanikiwa zaidi kwa namna ya kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwenye uchumi wetu wa kati, ili kasi iendelee kuhusiana na namna ya kutoza kodi kwa wafanyabiashara, naomba elimu kwa upande wa wafanyabiashara imekuwa ni ndogo. Kipindi cha nyuma mfanyabiashara anapokuwa anafanya biashara mfanyakazi wa TRA alikuwa ni rafiki wa mfanyabiashara lakini sasa hivi hali imekuwa siyo, wafanyabiashara wamekuwa wakilalamika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo napenda kuishauri Serikali kuanzia elimu ya msingi, sekondari na vyuo ikiwezekana kuwe na elimu kuhusu kodi kwa maana Mtanzania yeyote pindi anamaliza chuo asijute kwamba anaonewa namna ya kutoa kodi aone ni uzalendo kutoa kodi kwa maana ya kuendesha nchi yetu. Maana nchi inaendeshwa kwa kulipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa Watanzania wanaelewa vizuri sana kazi ambayo ameifanya Mheshimiwa Rais wetu ya kuijenga nchi yetu ya Tanzania. Mheshimiwa Rais wetu baada ya kuchaguliwa 2015 ndani ya siku mia moja alipongezwa kwelikweli hata wananchi mbalimbali wengine walisema Mheshimiwa Rais akae miaka 100, wengine walisema miaka 40, kila mtu aliongea la kwake kwa namna ambavyo amekuwa akiendesha nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema kwamba Mheshimiwa Rais ameweka nidhamu Serikali lakini ameweka nidhamu mpaka kwenye ndoa za Watanzania. Naongea hivyo kipindi cha nyuma watu walikuwa wakilalamika sana baba anarudi nyumbani usiku wa manane, mama anarudi nyumbani muda atakao akilalamika kwamba kuna foleni kubwa. Baada ya kuingia Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kama Rais, baba na mama wanawahi nyumbani kupanga mipango ya maendeleo ya familia zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hayo miaka ya nyuma mara nyingi sana tulikuwa tukiwashuhudia hawa watu wa Kilimanjaro ikifika Disemba wanarudi nyumbani kwao, kwetu haikuwa hivyo. Hata hivyo, baada ya kuingia Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli sasa hivi wazazi wanafurahia watoto wao, watoto wao walikuwa hawaonekani mikoani mwingine anakuwa hajaenda hata miaka mitano, mitatu mpaka kumi lakini sasa hivi ikifika Disemba magari yanapishana huko mikoani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana sana Watanzania tumuelewe Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Watu wanasema pesa haziko mifukoni lakini maendeleo yamekuwa ni makubwa, ukipita mitaani huko barabarani unaona jinsi wananchi wanavyojenga nyumba tena wanaezeka mabati ya m-South au tunapenda kuita mabati ya rangi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi nzuri anazoifanya. Ahsante sana. (Makofi)