Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Tecla Mohamedi Ungele (4 total)

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali pia napongeza kazi inayofanywa na Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi na Halmashauri zake katika kutatua migogoro hii.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, ni lini itajenga mabwawa kwa ajili ya kunywesha mifugo hiyo? Hapa tumeona katika jibu la msingi shida kubwa ni kugombania maji pamoja na malisho.

Mheshimiwa Spika, pili, tunaomba kazi hii ya kutatua migogoro katika Mkoa wa Lindi iharakishwe maana Sekretarieti ya Mkoa imeelemewa na migogoro hiyo. Je, Serikali inasemaje kuhusiana na suala hili?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tecla, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Lindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza kwa kutambua umuhimu na katika mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wa kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji, katika bajeti ya mwaka huu 2021/2022 tumetenga jumla ya shilingi milioni 900 kwa ajili ya kujenga mabwawa katika Mkoa wa Lindi. Bwawa moja litajengwa katika Wilaya ya Liwale na lingine katika Wilaya ya Nachingwea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Lindi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imejipanga vyema kwa kutumia Kamati inayoshughulikia migogoro ya ufugaji na wakulima kwenda kuweka kambi kuzungumza nao na kushirikiana katika kutafuta mbinu za kusuluhisha migogoro hii, ikiwa ni pamoja na kutatua lile tatizo la nyanda za malisho.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi kubwa ya Wizara ya Serikali kufanya ukarabati wa chuo hiki cha Ualimu Nachingwea, lakini kuna uhaba mkubwa wa samani, yani viti, meza, kwa ajili ya wanafunzi hao, lakini pia chuo hakina uzio. Je, Serikali ipo tayari kupanga bajeti kukamilisha mahitaji hayo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kutokana na jitihada kubwa ya vijana wa Mkoa wa Lindi kuwa na ufaulu mzuri katika kidato cha sita kwa miaka mitatu mfululizo inaonesha kabisa vijana hawa wako tayari kwa ajili ya elimu ya juu.

Je, ni lini Serikali itajenga chuo kikuu Mkoa wa Lindi kwa ajili ya kuchochea maendeleo kielimu, kiuchumi, kiutamaduni na kijamii? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika majibu yangu ya swali la msingi kwamba, Serikali imeendelea kukarabati vyuo hivi kwa kuhakikisha kwamba, tunakwenda kuimarisha, lakini tunakwenda kuongeza nguvu ili kuongeza udahili kutokana na uhitaji mkubwa sana wa walimu. Nikaeleza katika swali lile la msingi kwamba, Serikali bado inakihitaji chuo hiki ili kiweze kutoa taaluma hiyo ya astashahada na stashahada ili kuongeza idadi hiyo ya walimu.

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile katika swali lake ambalo linauliza suala la miundombinu ya samani, kwa takwimu tulizokuwanazo chuo chetu cha Nachingwea kina jumla ya viti 400 mpaka hivi sasa, kwa rekodi tulizonazo, lakini wanafunzi waliopo ni 295. Katika muktadha huo haioneshi kwamba, kuna uhaba wa samani kama viti na meza, lakini sambamba na hivyo tuna computer 30 ambazo zinawezesha vitengo vyetu vile vya kutumia computer kupata mafunzo kwa kutumia computer, lakini tuna projector tano ambazo zimenunuliwa hivi sasa na computer mbili ambazo zilikuwa za zamani.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali imeendelea na juhudi zake za kuhakikisha kwamba, tunatengeneza mazingira mazuri ya kupata walimu wa kutosha. Na katika kipindi kilichopita Serikali imeweza kutumia jumla ya shilingi bilioni 84.1 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, tunatengeneza miundombinu, lakini vilevile samani zinapatikana.

Mheshimiwa Spika, suala la uzio; Serikali bado inaendelea na mkakati wa kuhakikisha tunaboresha mazingira haya. Na hili sasa tunaliingiza kwenye bajeti kuhakikisha maeneo haya yanapata uzio ili kuweza kutengeneza usalama wa mali pamoja na samani za vyuo.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili kuhusiana na suala la chuo kikuu:-

Mheshimiwa Spika, nipende tu kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwa hivi sasa bado vyuo vyetu vilivyopo hapa nchini, vyuo vikuu, vina nafasi za kutosha. Na tunawashauri tu wananchi wa Lindi waweze kuvitumia vyuo ambavyo vipo kwasababu, vyuo havijengwi kwa kufuata mikoa wala kanda, bali vyuo hivi vinakuwa ni vya kitaifa, basi wanafunzi hawa wanaweza kwenda katika vyuo vingine ambavyo pale Mtwara tuna chuo kile cha St. Marius wanaweza kupata taaluma yao pale, lakini tuna matawi ya vyuo vikuu huria karibu katika mikoa yote ikiwemo na Mkoa huu wa Lindi.

Mheshimiwa Spika, lakini katika Chuo chetu cha Dodoma walihitajika kudahiliwa wanafunzi au kuna nafasi 40,000 lakini mpaka hivi sasa wanafunzi waliodahiliwa ni 29,595 kwa hiyo, tuna nafasi za kutosha katika vyuo hivi ambavyo vinatosheleza ku-absorb wanafunzi wote. Ahsante sana.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kadhia inayowapata wananchi wa Karatu ndiyo hiyo inayowapata wananchi wa Mkoa wa Lindi Wilaya ya Kilwa, Liwale, Lindi Vijijini, Nachingwea. Hata hivi juzi tu Wilaya ya Liwale, Kata ya Mbaya kuna mwananchi kule ameuawa na tembo. Pia wanaharibu mashamba ya vyakula na mazao kiasi kwamba wananchi wanaendelea…

NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. TECLA M. UNGELE: Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza tatizo hili la wanyama kule Nachingwea, Liwale na Kilwa ili wananchi wa huko nao wawe na maisha mazuri? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum Lindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimekwishakuelezea kwenye jibu langu la msingi nimetoa rai kwa wananchi kupanda mazao ambayo yanaweza yakaepusha hawa wanyama. Hata hivyo, tukumbuke kwamba tunaishi kwenye maeneo ambayo yalikuwa ni njia za wanyama na tukumbuke kwamba hawa wanyama walikuwepo kabla hata ya sisi kuwepo.

Kwa hiyo, wanyama siku zote wanaenda kwenye maeneo yao ya siku zote ambayo sisi ndiyo tumefanya mashamba. Niwaombe wananchi tena kwamba waendelee kupanda mazao haya ambayo tunahamasisha, lakini ikishindikana basi wasilime kwenye maeneo ambayo yako kandokando ya hifadhi. Ahsante.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nina maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi katika Mkoa wa Lindi na hii inaleta ufaulu hafifu kwa wanafunzi katika masomo hayo.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kupatikana walimu wa sayansi kwa haraka iwezekanavyo kunusuru shida hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia naona kwenye majibu kuna upatikanaji/kibali cha kuajiri walimu 10,000. Katika hilo naomba sana Serikali watupe kipaumbele Mkoa wa Lindi, kwa sababu tuna changamoto kubwa ya walimu. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tecla Mohamedi Ungele Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tumekuwa na upungufu wa walimu wa sayansi katika shule zetu za sekondari nchini kote na tumefanya tathmini, kubaini mahitaji ya walimu wa sayansi angalau kuwezesha shule zetu kuwa na walimu wanaoweza kutosheleza mahitaji ya wanafunzi. Ndio maana katika ajira zilizopita asilimia 75.5 ya walimu wote walioajiriwa walikuwa ni walimu, wa masomo ya sayansi na utaratibu wa kuendelea kutoa kipaumbele kwa walimu wa sayansi katika ajira zinazofuata utaendelea.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la kibali cha walimu katika halmashauri hiyo kupewa kipaumbele katika walimu 10,000, tutawapa kipaumbele na kazi iliyofanyika tumeainisha Mikoa yote yenye upungufu mkubwa zaidi wa walimu na watumishi wengine. Mikoa hiyo na Halmashauri hizo zitapewa kipaumbele wakati wa kuajiri watumishi hao. Ahsante. (Makofi)