Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Tecla Mohamedi Ungele (3 total)

MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatafuta mkakati wa kudumu wa kutatua tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji katika maeneo ya Mkoa wa Lindi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tecla Mohamed Ungele, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Lindi kumekuwa na ongezeko la migogoro ya wakulima na wafugaji, hususan katika Wilaya za Kilwa, Nachingwea na Liwale. Migogoro hii imetokana na ongezeko la mifugo ambapo kumeongeza uhitaji wa nyanda za malisho na maji.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi pamoja na Halmashauri ya Wilaya za Kilwa, Nachingwea na Liwale imefanya uhakiki na kubaini jumla ya migogoro 19, ambapo jumla ya migogoro 12 imetatuliwa na migogoro saba iko katika hatua mbalimbali za utatuzi.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Sekretariati ya Mkoa wa Lindi imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 81, na kuunda kamati ya utatuzi wa migogoro kwa kila halmashauri ili kuwahamasisha wafugaji kufuga kibiashara kwa kuendeleza ranch ndogondogo, na kila halmashauri kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji vitano kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali kupitia Halmashuri za Mkoa wa Lindi na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imepanga kutumia kiasi cha shilingi milioni 279.22 kwa ajili ya kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji 15, ikiwa ni hatua za utatuzi wa migogoro hiyo. Ahsante.
MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza:-

Je, Serikali haioni haja kukipandisha hadhi Chuo cha Ualimu Nachingwea kuwa Chuo Kikuu cha Ualimu kutokana na mahitaji ya Walimu kuwa makubwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tecla Mohamed Ungele, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, lengo la kuanzisha vyuo vya ualimu hapa nchini, kikiwemo Chuo cha Ualimu Nachingwea, ni kuhakikisha kuwepo kwa walimu mahiri na wanaotosheleza mahitaji ya walimu katika ngazi ya elimu ya awali, msingi, sekondari na elimu ya watu wazima. Vilevile, Vyuo hivi vina jukumu kubwa la kuwezesha mafunzo ya walimu kazini ambapo walimu walio karibu na vyuo hivyo hupata nyenzo mbalimbali za kitaalamu ili kuboresha ujifunzaji na ufundishaji shuleni.

Mheshimiwa Spika, ongezeko kubwa la wanafunzi na shule katika ngazi ya elimu ya awali, msingi na sekondari kutokana na Sera ya Elimu Bila Malipo, limesababisha kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa walimu katika ngazi hizo. Ili kukidhi mahitaji ya walimu katika ngazi hizo, Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya vyuo vya ualimu, uwekaji wa samani pamoja na vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Chuo cha Ualimu Nachingwea ni miongoni mwa vyuo vilivyofanyiwa ukarabati na ujenzi kwa gharama ya shilingi bilioni 1.9.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mahitaji ya walimu, hususan katika ngazi ya elimu ya awali na msingi ni makubwa kutokana na ongezeko kubwa la shule na wanafunzi katika ngazi hiyo, Chuo cha Ualimu Nachingwea bado kinahitajika katika kuandaa walimu wa stashahada na astashahada.

Mheshimiwa Spika, hivyo, wanafunzi wa shahada wanaweza kuendelea kudahiliwa na vyuo vikuu vilivyopo nchini kwa kuwa, bado vina uwezo wa kufanya hivyo. Ahsante.
MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza uhaba wa watumishi katika Idara ya Elimu katika Mkoa wa Lindi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tecla Mohamedi Ungele, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais -TAMISEMI ilifanya tathmini ya mahitaji ya walimu katika shule za msingi na sekondari nchi nzima na kubaini kuwa Mkoa wa Lindi unauhitajii jumla ya walimu wa shule za msingi 4,760 na waliopo ni 3,544 ikiwa ni upungufu wa walimu 1,216 sawa na asilimia 25.5 ya mahitaji. Kwa upande wa shule za sekondari, Mkoa wa Lindi unahitaji walimu 4,580 na waliopo ni 1,682 na upungufu ni walimu 2,898 sawa na asilimia 63.3 ya mahitaji.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hiyo nchini kote Serikali imetoa maelekezo kwa Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kuhakikisha wanafanya msawazo wa walimu katika maeneo yao.

Pili, Serikali inakamilisha muongozo wa walimu wa kujitolea, utakaotumika kuwapata walimu wanaojitolea katika shule zenye uhitaji mkubwa. Walimu hao wanaojitolea watatambulika rasmi kupitia mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya kupata chanzo sahihi cha kurejea utendaji kazi wao.

Tatu, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeomba kibali cha kuajiri walimu 10,000 katika shule za msingi na sekondari nchini ikiwemo Mkoa wa Lindi. Ahsante.