Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Tecla Mohamedi Ungele (6 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii kwa ajili ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kunipatia nafasi hii ya Bunge ni nafasi adimu, mimi ninaisema ni kwa neema yake Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Pia nakishukuru Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Lindi na kutokana na juhudi na kazi zilizoonekana za Dkt. John Pombe Magufuli zimetia imani kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi hata mwaka jana tumepata majimbo yote kwa Chama cha Mapinduzi ukilinganisha na mwaka 2015. Pia nashukuru familia yangu na rafiki zetu wote kwa support walionipatia kwa muda wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika napenda kuchangia kwa muda mchache huu hotuba ya Mheshimiwa Rais kwenye ukurasa wa 32, 33 na 34 kwa maeneo ya sekta ya afya, maji na elimu. Napongeza kwa kazi zote alizofanya na ndiyo maana zimeandikiwa kwenye taarifa hii na pia hata kwenye Ilani ya Uchaguzi kwamba nini tutaenda kufanya kwa miaka hii mitano mpaka mwaka 2025.

Mheshimiwa Spika, sekta ya afya kwa mafanikio ni makubwa, mimi mwenyewe nina uzoefu mkubwa kwenye sekta ya afya ndio nilipokulia mpaka sasa hivi, kwa sababu zaidi ya miaka 30 nimeendelea kuudumu huko kama mwalimu muuguzi, na mkunga kwa hiyo, ninauzoefu mkubwa sana na maendeleo yaliyotokea na mafanikio yaliyotokea kwakweli ni makubwa sana huwa ninamwangalia Dkt. Johh Pombe Magufuli huyu ni daktari, huyu ni muuguzi ama yaani ana kila kila sifa, lakini nikiangalia kumbe ni sababu wa utegemezi wake kwa Mungu aliye hai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini napenda kuchangia kwa machache tu katika huduma za afya, pamoja na mafanikio yote hayo lakini kuongezwe ajira za wafanyakazi wa Wizara ya Afya ama idara hiyo ya afya ili tupate skilled personnel.

Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema hivyo? Nasema hivyo kwa sababu ukiwa na wafanyakazi wa kutosha hata huyu mama nikitolea mfano mama mjamzito au mama anayekuja kujifungua au mtoto anayekuja kupata huduma pale watakuwa na muda mfupi wa kukaa pale kwa huduma kama ni huduma za kutwa ama hata za kulazwa hospitali lakini kutakuwa na muda mzuri wa hudumu hawa kuwaudumia hawa wagonjwa na pia hata stress za wafanyakazi zitapungua, kwa sababu wafanyakazi wako wengi na hata huduma atakayopata yule mgonjwa ama mama yeyote basi itakuwa ni nzuri.

Mheshimiwa Spika, lakini pia katika eneo hilo hilo afya mimi kama Mbunge kwenye mkoa wangu au popote nitakaopita na utaalamu wangu nitaendelea kuwahamasisha akinamama wajawazito na watoto hata na jamii kwa ujumla waende kupata huduma za hospitali.

Mheshimiwa Spika, lakini pia napenda kuchangia kwenye sekta ya afya mafanikio mengi yamepatikana lakini tumeona changamoto hata Mheshimiwa Rais aliiona wakati wa kampeni kwamba maji bado vijijini. Kwa hiyo hata vijiji mbalimbali vya Mkoa wa Lindi vile vijiji vingine bado havijapata maji, nikiangalia yule mama mjamzito bado anaenda kuhangaika kutafuta maji bado anaangaika ili na lile kuangalia familia hivyo basi ni tatizo tunaomba maji, mwanamke huyu tumtue maji angalau hata anapokuwa mjamzito asihangaike kutafuta maji, akihangaika huku na kule bado hata uzazi wake hautakuwa salama.

Mheshimiwa Spika, pia nachangia kwenye sekta ya elimu kwa haraka haraka, nashukuru kwa elimu bila malipo hata mwanafunzi hata mtoto wa Mkoa wa Lindi anapata elimu na hata Tanzania nzima kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne. Lakini katika hili ninashukuru pia kwa kuzingatia masomo ya sayansi. Kwa uzoefu wangu wa vyuo vya afya mara nyingi tunakosa wanafunzi wazuri kwa sababu hawakufaulu sayansi kwa hiyo hilo nalo nalipongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia katika elimu tunaomba elimu ya juu kwa Mkoa wa Lindi hakuna Chuo Kikuu kwa hiyo naomba kuwe na compass ya Chuo Kikuu Mkoa wa Lindi ili nako tupate elimu ya hali ya juu ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutupatia uhai na hata sasa tunaendelea kuhudumu katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake ya bajeti iliyosheheni matumaini makubwa katika mwaka 2021/2022. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia kwenye maeneo mawili; la kwanza kuhusu watumishi wa Idara ya Afya; kwa uzoefu na observations nyingi za Mkoa wa Lindi, vituo vingi vya afya vinahudumiwa na wahudumu wa afya yaani Medical Attendants. Sasa hii inaathiri utoaji wa huduma ya dharura ya uzazi yaani CEmONC na hiyo itaashiri kufikia malengo ya kupunguza vifo vya akinamama wakati wa ujauzito na kujifungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitolea mifano michache tu, najua wilaya zote zina shida hizo, lakini mfano Kituo cha Afya cha Nanjilinji, kimepata huduma nzuri za majengo na tunashukuru Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, lakini watoa huduma ambao wana ujuzi hawapo. Kunapotokea dharura ya uzazi, mzazi huyo anakimbizwa kwenye Hospitali ya Wilaya jirani ambayo ni Ruangwa ambapo kuna kilomita 44 kutoka Nanjilinji, tofauti na kutoka Nanjilinji kwenda Hospitali ya Wilaya Kinyoga kule Kilwa ambayo kuna kilomita 174.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara inayotoka Nanjilinji kwenda Ruangwa nayo sio nzuri, ni barabara ya vumbi lakini pia inapita kwenye Mto Nakiu ambao hauna daraja, sasa masika kama haya ukijaa, hebu ona sasa hapo, mgonjwa yule ni mama anayehitaji kujifungua, anayehitaji operation ya kujifungua, lakini anashindwa kuvuka pale na ambulance unayo lakini kuna shida. Mkoa wa Lindi una shida sana una changamoto za huduma za afya, majengo tumepata tunashukuru na vifaa sehemu nyingine vipo, lakini watoa huduma ni wachache. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuchangia kwenye miundombinu, Mkoa wa Lindi kuna sehemu chache sana ile barabara kutoka Kibiti – Lindi – Masasi – Tunduru – Songea; ni hiyo tu ndiyo ya lami, lakini tunaomba ile barabara ya kutoka Masasi – Nachingwea; Nanganga – Ruangwa; Ruangwa - Nachingwea, Nachingwea – Liwale; na Nangurukuru -Liwale, tunaomba ijengwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna changamoto ya barabara za vijijini; natolea mfano kwa sasa ni masika, barabara zingine hazipitiki, mfano barabara ya kutoka Mipingo kwenda Mnyangara mpaka kule Namapwia ambako anatoka yule mjusi unayemsikia, sasa hivi hakupitiki kabisa. Pia kuna barabara ya kutoka Hoteli Tatu kwenda Pande na Lihimalyao kwenyewe ni changamoto kubwa. Pia kuna barabara inayotoka Somanga kwenda mpaka Kibata, nako ni changamoto; kwa ujumla barabara za vijijini Mkoa wa Lindi kuna changamoto kubwa. Jamani, tafadhali tunaomba mkoa ule uangaliwe kwa jicho la pekee ili kuwanusuru wananchi wale, ili nao angalau na wenyewe wachangie kwenye maendeleo ya nchi hii na wajisikie kwamba kwenye nchi yao ya kufaidi matunda.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja katika Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Awali ya yote, napenda kushukuru Wizara hii, kwa ajili ya ujenzi unaoendelea, sasa hivi mkandarasi yupo pale kwenye barabara ya Nanganga
kwenda Ruangwa. Ila ombi langu naomba ujenzi uende na viwango, lakini pia uende kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Nachingwea kwenda Liwale, kilometa 130; Nangurukuru – Liwale, kilometa 230; na Kiranjeranje - Namichiga – Ruangwa, kilometa 120. Hizi zote zipo kwenye hatua za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ufikie wakati zijengwe kwa lami. Kwa nini naomba hivyo? Barabara hizi kuwa katika kiwango cha lami ni muhimu sana kwa sababu usafirishaji wa watu, lakini usafirishaji pia kwa wagonjwa, lakini usafirishaji wa mazao ya korosho na ufuta ambayo ni mazao ya biashara kwenye Mikoa ya Lindi na Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposhindwa kusafirisha mazao haya Maisha ya watu kule Mkoa wa Lindi yanakuwa duni. Naamini kabisa siku moja ukipata bahati kwenda Liwale utaona kabisa huku ulipo ni kugumu sana, lakini kule kunapatikana korosho na ufuta kiasi kwamba unaweza kukwamua wananchi wa kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo ni mfanyabiashara gani atakayehangaika kwenda kununua korosho kule, badala ya kwenda kununua kwenye maeneo ambayo yanapitika. Naomba ufike wakati kuwepo na barabara ya lami kwenda Liwale na kwingineko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuongelea pia habari ya Uwanja wa Ndege wa Nachingwea. Nimeona kwenye Randama kunataka kuwekwa lami, naomba hilo lifanyike kwa umuhimu wake sana. Uwanja wa Ndege wa Nachingwea una umuhimu sana kwa sababu pale ni center mtu wa Liwale, Ruangwa, Masasi anaweza kusafiri kupitia Nachingwea kuliko kwenda Mtwara kilometa 200 kutoka Masasi. Pia itarahisisha wawekezaji, kule kwetu sasa hivi kuna madini, kuna madini Nditi, kuna madini Ruangwa, ni rahisi kwa wafanyabiashara wawekezaji kupitia kuanzia Nachingwea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia na-share tu experience niliyoipata wakati wa mazishi ya Mzee Mkapa. Ndege nyingi, viongozi wengi walitua katika Uwanja wa Ndege wa Nachingwea, lakini uwanja ule kwa sababu ni wa vumbi adha iliyopatikana wanaifahamu mmojawapo akiwa Mheshimiwa Spika mwenyewe wa Bunge letu, Mheshimiwa Ndugai, anapafahamu Nachingwea. (Makofi)

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ungele kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Hamida Abdallah.

T A A R I F A

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji anayezungumza hivi sasa kwamba Uwanja wa Ndege wa Wilaya ya Nachingwea, atambue kwamba tumerithi kutoka kwa wakoloni kikiwemo pia Kiwanja cha Lindi Mjini. Kuna umuhimu mkubwa sasa Serikali kuona namna bora ya kuboresha uwanja ule, tena kwa haraka zaidi. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tecla Ungele.

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, napokea kwa mikono miwili taarifa hiyo. Uwanja ule pia ni muhimu sana kwa ulinzi na usalama. Nachingwea tuna vikosi vya jeshi, kwa hiyo kunavyokuwa hali yoyote ya kuhitajika usalama ndege pale zitatua na mambo mengine yataendelea. Ufikie wakati Wizara iiangalie Nachingwea na Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa ujumla. Ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili nami nichangie hoja hii iliyotolewa na Kamati ya Masuala ya UKIMWI, dawa za kulevya, kifua kikuu na magonjwa yasiyoambukiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote tunamshukuru na tunampongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza na kuongeza ujenzi wa madarasa katika shule zetu ili kupunguza msongamano wa wanafunzi katika madarasa hayo. Msongamano huo ndio uliokuwa unaleta magonjwa ya maambukizi ikiwa ni pamoja na kifua kikuu na mengineyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nitauelekeza kwenye kifua kikuu na ukoma. Kifua kikuu ni ugonjwa mkubwa na ni tatizo kubwa nchini Tanzania. Tunaona Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 ulimwenguni zenye maambukizi makubwa ya kifua kikuu; mwaka 2019 kulikuwa na wagonjwa 137,000. Kikubwa zaidi, kwa kifua kikuu kama mgonjwa hakugundulika mapema na hakupata matibabu mapema basi kuna hatari ya kwenda kwenye kifua kikuu sugu na hatimaye kusababisha kifo. Mgonjwa wa kifua kikuu asipopata matibabu anaambukiza watu wengine 10 mpaka 20 kwa siku. Hilo ni tatizo kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitachangia kuhusu ugonjwa wa ukoma. Bado ukoma ni tatizo kwenye nchi yetu; na ukoma nao unaambukiza kwa njia ya hewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha mwaka 2019 kulikuwa na wagonjwa 1,600 nchini, lakini pia hata kihistoria ugonjwa wa ukoma una asili fulani ya unyanyapaa. Kwa hiyo kuna hatari wagonjwa hawajitokeza. Sasa, ushauri wangu ni kwamba, kuimarisha elimu ya afya katika jamii, lakini pia kutumia kikamilifu kada ya community health workers nchini kwetu. Tumeona sasa hivi wanaajiriwa kama medical attendance, lakini kada hii ilikuwa specifically kwa ajili ya kwenda kwenye jamii na ndiko watakakoshughulika na magonjwa haya sugu, kugundua wagonjwa wa kifua kikuu na maambukizi mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri kuwe na mafunzo maalum, iwe short courses ama course za muda mrefu kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ambukizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia hoja kwenye Wizara hii muhimu sana Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kupongeza kazi kubwa inayofanywa na Wizara hii. Mheshimiwa Waziri Dkt. Dorothy Gwajima na timu yake yote, Katibu Mkuu na timu yote mpaka kule kwenye vituo vya afya na zahanati wanafanya kazi kubwa sana kuokoa maisha ya watoto, akina mama na wananchi wote kwa ujumla. Pia naipongeza Serikali nzima kwa ujumla kwa kazi kubwa inayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia muda, naomba nijikite kwenye mambo makuu mawili. La kwanza, upungufu wa watoa huduma katika sekta ya afya lakini la pili, uhaba wa vitendea ikiwepo ambulance na vifaa vingine katika hospitali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kwa ufupi hii suala la ambulance. Tunaona maeneo mengi yako mbali na hospitali za wilaya na huko kwenye maeneo hayo ya vijijini na kwenye kata kunatoa huduma mbalimbali lakini hakuna huduma ya ambulance. Nikitolea mfano kuna sehemu ambayo kuna zaidi ya kilomita 70 lakini inapotokea tatizo hakuna ambulance, mfano Nachingwea tuna ambulance moja ambayo ni mpya kwenye Kituo cha Afya Kilimarondo lakini zile ambulance zilizoko katika Hospitali ya Wilaya ni chakavu, hapa na hapa zinapata breakdown kiasi kwamba hata mgonjwa mwenyewe anaweza akafia njiani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye upungufu wa watumishi kwenye sekta ya afya, tumeona hapa Kitaifa kuna upungufu zaidi ya asilimia 53, hicho ni kiasi kikubwa sana. Nikienda kwenye Mkoa wa Lindi nikitolea mfano Wilaya kadhaa, Wilaya ya Ruangwa tulipaswa tuwe na watoa huduma 840 lakini waliopo ni 257 sawasawa na asilimia 31, upungufu ni asilimia 69. Nachingwea mahitaji ni 1,077 waliopo sasa hivi ni 305 tu upungufu ni 772. Wilaya ya Liwale wafanyakazi wa sekta ya afya ni 510 lakini waliopo ni 221 tu, upungufu ni 289. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama nilivyokuwa nimesema siku moja nilivyochangia mchango wangu hapa kwamba zahanati nyingi zinahudumiwa na medical attendants. Nasema hivi pamoja na upungufu huo, kwa mfano Wilaya ya Liwale mpaka kufika Hospitali ya Wilaya zahanati na vituo vya afya vingine viko mbali sana na ndipo pale tunapokuja kutoa mchango kwa kusema kwamba kuna tembo huko na kadhalika. Kwa hiyo, anapokuwepo mtoa huduma mmoja kwenye health facility fulani anapokuja kupata mshahara na kupeleka taarifa mbalimbali kwenye Hospitali ya Wilaya, humo njiani anakabiliana na mambo mbalimbali ikiwepo na wanyama wakali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huduma ya afya kunapokuwa na upungufu wa rasilimali watu matokeo yake ni kutokutoa huduma nzuri au huduma hafifu matokeo yake yanatokea pale pale, haisubiri baadaye. Labda ni mtu kutokuhudumiwa jambo fulani ni pale pale. Naamini kabisa kuna sekta zingine kama leo kukitokea kupata huduma hafifu matokeo au madhara yake yanatokea baadaye lakini kwenye sekta ya afya kama hakuna huduma nzuri matokeo yake yanatokea pale pale. Kama ni vifo vitatokea pale, kama ni mtu ana changamoto gani ni pale pale haisubiri baadaye. Kwa hiyo, jambo hili la kuwa na rasilimali watu wa kutosha kwenye health facilities ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Nimeona baada ya kutoa changamoto hiyo niseme nini kifanyike? Ya kwanza nimeona, Waziri wa TAMISEMI ametangaza hapa ajira kama zaidi ya elfu mbili kwenye sekta ya afya. Naona jambo hili likitekelezwa kwangu ni faraja kubwa kweli na naamini kabisa Waziri wa TAMISEMI akiungana na Waziri wa Afya watasaidia kuangalia Mikoa ya Lindi na Mtwara na kwingineko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suluhisho lingine ni mikataba ya ajira. Miaka iliyopita Wizara ya Afya iliungana na sekta binafsi kama vile bima na HITECH kupata ajira ya mkataba kwa ajili ya maeneo ya pembezoni, ile ilisaidia sana sijui ile program inaendelea au namna gani? Naomba Wizara ya Afya wajipange kutafuta kama ni wadau wengine kunusuru tatizo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine naomba Wizara husika itoe vibali kwa halmashauri zetu ziajiri kwa mkataba lakini pia kutumia own source kwa ajili ya kuwa-retain wale wafanyakazi. Mara nyingi vijana wanaajiriwa kwenye maeneo yetu lakini kutokana na mazingira fulani baada ya miaka miwili au mitatu wanaomba kuhama. Kwa hiyo, naomba jambo hili la retention liangaliwe sana. (Makofi)

Sisi tulifanya research kuangalia ni jinsi gani itasaidia kuwa na retention mechanism Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa kutumia vyuo vyetu vya afya na halmashauri husika na hili jambo liliwezekana. Naomba jambo hilo liwezekane Wizara husika ya Utumishi itoe vibali vya kutumia own source kwa ajili ya retention mechanism. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na awali ya yote naipongeza Wizara hii ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzungumzia kuhusu jinsi Tanzania tulivyoshiriki ukombozi wa Bara la Afrika hasa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, waasisi wetu Mwalimu Nyerere na wenzake waliamini kabisa kwamba uhuru wetu Tanzania hautakuwa na maana kama nchi za Kusini mwa Bara la Afrika hazitakuwa huru na ndiyo maana ilikuwa ni ajenda kubwa ya wakati ule. Hivyo basi, kwa nchi hii ya Tanzania tulivyoshiriki kwa kiasi kikubwa na wakati ule hasa kwenye Mikoa ya Kusini ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ikawa ndiyo base kubwa ya wapigania uhuru wa nchi ya Msumbiji, Angola, Namibia, Afrika Kusini na Zimbabwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi imekuwa kama historia, lakini nakumbusha kwamba maeneo ya Lindi ikiwepo Nachingwea kulikuwa na maeneo ya Matekwe, Kwamsevumtini na kule Mtwara maeneo ya Samora na Lindi Vijijini, Lutamba, Ruvuma maeneo ya Namtumbo yale sehemu ya Seka Maganga na kwingineko ili kuwa ndiyo base na ma-camp ya wapigania uhuru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yale pamoja na kuwa base tu lakini bado jamii husika ilikuwa nayo iko katika harakati zile, wanaotoka maeneo yale wanafahamu sana. Hivyo basi, wakati ule sasa, wakati wote wa harakati wa kupigania uhuru mikoa ile ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ilikuwa ni vigumu kwa wawekezaji kwenda kuwekeza kule kwa sababu wakati wowote Mreno anaweza akaja akaleta vurugu kule na wengine, kwa hiyo, hakukuwa salama. Hivyo tukaja kujikuta kwamba maeneo yale kwa namna fulani yakawa nyuma kimaendeleo, huo ni ukweli usiopingika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya harakati zile kwisha maeneo yale sasa Halmashauri husika zikaendeleza maeneo yale, wakaanzisha Sekondari zile za Matekwe na kwingineko, lakini ni juhudi za Halmashauri husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa baada ya kufanya hivyo nini ushauri wangu. Nashauri hivi tunaomba kwa Wizara hii ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa wizara hii naamini kabisa inaongozwa na Mheshimiwa Mama Mulamula na Naibu Waziri na timu yote ya Wizara ya Mambo ya Nje naamini kabisa wanavyofika wakuu wa nchi hizi za Kusini mwa Bara la Afrika tulizopambana kwa kiasi kikubwa kuwakomboa tunaomba muwaambie na muwalete maeneo ya Nachingwea na kule Ruvuma ili waje waone yale makambi, waje waone jitihada zile tulizozifanya sisi wenyewe ndani ya halmashauri husika bado hazitoshi tunaomba mchango wao, tunaomba waje waweke wafanye jambo fulani kama ni la maendeleo ili tuone kumbukumbu kubwa ifanyike kama inavyofanyika sehemu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia hii kwa uchungu kweli, tumeachwa hivyo na ndiyo hiyo naona kama vile historia inajiendeleza vile kwamba kila kitu tuko hivyo tuko nyuma tu…

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tecla Ungele kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Zuberi Kuchauka.

T A A R I F A

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe Taarifa mama yangu anachokizungumza ni kweli kabisa na ndiyo maana Mikoa ya Lindi na Mtwara miaka ya nyuma ilikuwa mikoa ya adhabu kwamba mtu akifanya makosa anapelekwa mikoa hiyo na mikoa hiyo haikuendelezwa ni kwa sababu tu ya hayo makambi ya hiyo vita za ukombozi wa Kusini mwa Afrika.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tecla Ungele, malizia mchango wako.

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napokea hiyo taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili siyo jambo geni kwa watu uliowafanyia hisani wakashukuru na kama mtu hashukuru basi kama kunauwezekano wa kumkumbusha. (Makofi)

M imi naamini kabisa watakapoletwa wale viongozi kule wakaona wakasema hapa ndiyo ilipokuwa camp fulani, hapa ndiyo ANC walikuwa hapa, watakuwa na uchungu fulani wa kuweka jambo fulani vinginevyo wala hawafahamu kwa sababu wako kwenye neema sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo ndiyo ombi langu na hii imeshatokea na kwingine na kwingine, siyo ajabu hili ninalolizungumza, wakipelekwa kule wakaja kuona hali halisi ninaomba, ninaomba, ninaamini kabisa Mheshimiwa Mulamula ninakuaminia, ni mama, una uchungu wa nchi hii, ninaomba hilo uliweke katika priority naomba utuangalie kwa kila hali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)