Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Jonas William Mbunda (4 total)

MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru Naibu Waziri wa TAMISEMI kwa majibu mazuri, lakini vile vile niipongeze Serikali kwa kutoa huduma nzuri katika maeneo mbalimbali kwenye fani ya afya. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa hospitali hiyo ilijengwa mwaka 1970, jengo la OPD na jengo la upasuaji ni majengo ambayo yamepitwa na wakati na hayaendani na hadhi ya hospitali ya wilaya pamoja na jengo la wodi ya watoto ambao limekosekana kabisa.

Je, Serikali itaanza lini kushughulikia ujenzi wa majengo ya OPD, upasuaji na wodi ya Watoto?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika hospitali hiyo kuna uhaba wa watendaji, wafanyakazi, Madaktari na watendaji wasaidizi. Je, ni lini Serikali itachukua hatua ya kuhakikisha kwamba changamoto hiyo inatatuliwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jonas William, Mbunge wa Mbinga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nipokee pongezi za Mheshimiwa Mbunda na kwamba Serikali imeendelea kuboresha sana huduma za afya kwa kujenga miundombinu, lakini pia kuhakikisha vifaatiba na dawa zinapatikana. Kuhusiana na hospitali hii kuwa kongwe ni kweli. Hospitali hii imejengwa miaka ya 70 na ni hospitali ambayo kimsingi ni chakavu, inahitaji kuboreshewa miundombinu ili iweze kuendana na majengo ambayo yanaweza kutoa huduma bora za afya kwa ngazi ya hospitali ya halmashauri.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hayo, ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimeeleza kwamba Serikali imeanza kufanya tathmini ya uchakavu wa majengo yale na upungufu wa majengo ambayo yanahitajika katika hospitali ile ili sasa tuweze kuona namna ya kutenga fedha kwa ajili ya kuanza either, kukarabati majengo yale na kuongeza yale majengo yanayopungua au kuanza ujenzi wa hospitali mpya. Kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tathmini hiyo itakapokamilika tutakuja na jawabu la njia sahihi ya kwenda kutekeleza ili kuondokana na changamoto hiyo.

Mheshimiwa Spika, pili, ni kweli kuna changamoto ya upungufu wa watumishi katika kada mbalimbali katika hospitali hiyo na nchini kote kwa ujumla. Katika bajeti yetu tumeeleza mipango kwamba baada ya kukamilisha miundombinu ya majengo, tutakwenda kuhakikisha tunaboresha upatikanaji wa vifaatiba, lakini suala linalofuata muhimu na linapewa kipaumbele cha hali ya juu ni kuhakikisha sasa tunakwenda kuomba vibali vya kuajiri watumishi wa afya katika ngazi zote za vituo vya afya, zahanati na hospitali ili tuweze kutoa huduma bora zaidi. Kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunda kwamba, katika Hospitali hii ya Mji wa Mbinga pia tutaweka kipaumbele katika kuajiri watumishi ili kuendelea kuboresha huduma za afya.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza niishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, Mji wa Mbinga unakua kwa kasi na kipindi cha mvua barabara nyingi ambazo zimejengwa kwa kiwango cha changarawe huwa zinaharibika. Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kuongeza kiasi kilichotengwa katika msimu wa 2020/2021 na 2021/2022 ili kuhakikisha kwamba angalau kipande kirefu kijengwe ili kukidhi matakwa ya wananchi wa Jimbo la Mbinga Mjini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Serikali imefanya vizuri sana katika program ya ULGSP na TSCP na kuna uwezekano mradi wa TACTIC, je, Halmashauri ya Mbinga Mjini itakuwepo katika programu hii ya TACTIC?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipate majibu ya Serikali. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge alikuwa anaomba tu kwamba katika bajeti ya mwaka 2021/ 2022 Serikali iweze kuongeza fedha katika Mji wa Mbinga Mjini ili angalau Serikali iendelee kujenga barabara nyingi za kutosha. Kwa sababu bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilishapitishwa na kiwango tulichokitenga kwa ajili ya fedha kipo kulingana na ukomo, lakini katika majibu yetu ya msingi tumeainisha hapo kwamba kwa kadri fedha zitakavyoendelea kupatikana, udharura na kadhalika, tutaendelea kupeleka fedha katika Halmashauri ya Mji Mbinga ili wananchi wake waweze kupata barabara nzuri na zinazopitika wakati wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ameuliza kama Mji wa Mbinga upo katika ule mradi wa TACTIC. Nimwambie tu kabisa kwamba katika ule mradi, Halmashauri ya Mji Mbinga ipo. Ni sehemu ya ile miji 45 ambayo imeainishwa.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nina swali moja la nyongeza. Barabara hiyo ili iweze kukamilika inatakiwa yajengwe madaraja mawili; je, Serikali haioni kwamba kiasi cha fedha cha shilingi milioni 10 kilichotengwa hakitatosheleza kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameuliza, kwa nini Serikali isijenge pamoja na daraja lingine kwa sababu hiyo barabara ina madaraja mawili na fedha tuliyotenga ni ndogo kukamilisha hiyo barabara. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakwenda kufanya tathmini na baada ya hiyo tathmini tutatafuta fedha ili tuweze kumalizia na hilo daraja lingine ili liweze kukamilika. Ahsante sana.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza naomba nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali. Vile vile naomba niishukuru Serikali kwa kutekeleza miradi ya Lusaka, Mradi wa Mpepai na mradi wa Lifakara. Mwaka 2020 Serikali ilianza kutekeleza mradi katika Kata ya Myangayanga na Kata ya Ruahita, miradi hiyo miwili hadi sasa bado haijatekelezwa. Kwa hiyo nataka nijue, je, Serikali ina mpango gani wa kutekeleza miradi katika hizo kata mbili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jonas Mbunda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hizi kata alizozitaja ziko kwenye mpango wa utekelezaji na kwa Mbinga Mjini tunatarajia hadi kufika 2023 Disemba, labda vitabaki kama vijiji viwili tu ambavyo vitakuwa bado havijapata maji. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kwa namna ambavyo tunashirikiana nampongeza sana na nimhakikishie maji Mbinga yanakwenda kupatikana.