Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Jonas William Mbunda (4 total)

MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga na kukarabati majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Mbinga kutokana na kukosa baadhi ya majengo na yaliyopo kuchakaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Mbinga ina majengo saba ambayo ni jengo la akinamama, jengo la huduma za Bima, jengo la upasuaji, jengo la maabara, jengo la kuhifadhia maiti, jengo la mionzi na jengo la wagonjwa wa nje. Baadhi ya majengo hayo yana uchakavu wa wastani na mengine yana uchakavu wa hali ya juu. Jengo muhimu linalokosekana katika hospitali hiyo ni jengo la wodi ya watoto. Serikali imefanya tathmini ya hali ya uchakavu wa miundombinu ya hospitali hiyo ili kuona namna bora ya kufanya ukarabati au ujenzi wa hospitali mpya ya halmashauri. Kuanzia Mwaka wa Fedha 2017/2018 hadi 2019/2020, Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri imefanya ukarabati wa jengo la wodi maalum na jengo la wagonjwa wa nje kwa gharama ya shilingi milioni 45.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga na katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imeipatia Halmashauri ya Mji wa Mbinga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa Kituo cha Afya, Kalembo ambacho ukarabati wake umekamilika na huduma zinatolewa ikiwemo huduma za upasuaji. Aidha, mwaka 2021 Serikali imeipatia shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma matatu ya Zahanati za Kagugu, Iringa na Ruwaita. Vile vile katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, Serikali imeomba kuidhinishiwa shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma matatu ya zahanati katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa awamu itaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya kutolea huduma za afya nchini kote ikiwemo katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika Mji wa Mbinga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mbinga Mji, ina barabara zenye urefu wa kilomita 7.45 zilizojengwa kwa kiwango cha lami zikiwemo kilomita 0.2 zilizojengwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 kwa gharama ya shilingi milioni 170. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa barabara ya Mbuyula Hospitali hadi Ikulu ndogo yenye urefu wa kilomita moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya barabara nchini kote ikiwemo Halmashauri ya Mji wa Mbinga kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza kujenga Barabara ya Kijiji cha Uzena kwenda Kijiji cha Njomlole katika Jimbo la Mbinga Mjini kwa kiwango cha changarawe ili iweze kupitika kwa wakati wote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini, kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara inayounganisha Vijiji vya Uzena na Njomlole inayojulikana kama barabara ya Masimeli – Njomlole na ina urefu wa kilomita 5.5, katika mwaka wa fedha 2021/2022 TARURA, Halmashauri ya Mji Mbinga imetenga Shilingi milioni 10 kwa ajili ya matengenezo ya barabara hiyo.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/ 2022, Wakala wa Barabara za Vijijni na Mijini umepanga kufanya tathmini ya miundombinu ya barabara na madaraja nchini kote ikiwemo Jimbo la Mbinga Mjini ili kuandaa mpango wa namna bora ya kutoa kipaumbele cha ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara na madaraja.
MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafikisha maji safi na salama katika Kata za Kikolo, Utiri, Mbangamao, Kilimani na Mateka?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Mbinga Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa huduma ya Majisafi na salama katika Wilaya ya Mbinga ni wastani wa asilimia 59.2. Katika kuboresha huduma ya maji katika Wilaya ya Mbinga, Serikali imeendelea kutekeleza Miradi ya Maji ya Mpepai, Mabuni, Amanimakolo, Luhagara, Myangayanga, Luwaita, Lifakara/Uzena na Ruanda. Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa Matangi kumi na moja (11) yenye jumla ya ujazo wa lita 775,000, ulazaji wa mtandao wa mabomba umbali wa kilometa 105.1 na ujenzi wa Vituo 116 vya kuchotea maji. Miradi hiyo ikikamilika itanufaisha wananchi wapatao 45,478.

Mheshimiwa Spika, jukumu la Serikali ni kuhakikisha maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Mbinga yanapata huduma ya majisafi na salama na yenye kutosheleza. Katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imekamilisha kazi ya usanifu wa Miradi ya Maji katika Kata za Mateka, Kikolo na Utiri na ujenzi wa miradi katika Kata za Mateka na Utiri utaanza mwezi Aprili, 2022 na Mradi wa Maji wa Kikolo unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2022/2023. Vilevile, Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Maji katika Kijiji cha Uzena (Kata ya Kikolo) kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO – 19 na unatarajia kukamilika ifikapo Juni, 2022.

Mheshimiwa Spika, Kata ya Kilimani inapata huduma ya maji kupitia mtandao wa maji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbinga. Katika kuboresha huduma ya maji katika kata hiyo, Serikali imepanga kutekeleza upanuzi wa Mradi wa Maji wa Lifakara kupeleka Kata ya Kilimani katika mwaka wa fedha 2022/2023.