Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Vita Rashid Kawawa (6 total)

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa jambo hili ni la dharura kwani kwa sasa wakulima wamelima, wamepanda, wamepalilia na kutia mbolea katika mashamba yao kwa thamani kubwa lakini makundi ya tembo yameingia na kuvuruga mashamba hayo na wakulima wamepata taharuki hasa baada ya mkulima mmoja kuuwawa na tembo hao. Je, Serikali inaweza sasa kupeleka kikosi maalum kufanya operation ya kuwaondoa na kuwafukuza tembo hao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa jambo hili linasababishwa pia na makundi ya ng’ombe waliondolewa katika maeneo ya Mkoa wa Morogoro na kuingia katika maeneo ya hifadhi ya tembo hawa na kuharibu ecology yake na kufanya tembo hawa kufika kwa wananchi. Je, Serikali kwa kutekeleza azma ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa katika hotuba yake ukurasa wa kumi na sita hapa Bungeni kwamba itaongeza maeneo ya hekta kufika milioni sita…

SPIKA: Fupisha swali Mheshimiwa.

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, Serikali imejipangaje kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kuongeza maeneo ya wafugaji ili kuondoa mgongano huu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge la Jimbo la Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la kwanza ambalo amesema kupeleka vikosi kazi kwa ajili ya kwenda kushughulikia uvamizi wa tembo; Serikali ipo tayari na hata leo anavyowasilisha tayari Serikali ilishafanya mchakato wa kuhamisha hao tembo na inaendelea kuwaondoa katika maeneo hayo ya mashamba na shughuli za kibinadamu. Kwa hiyo nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Kawawa, kwenye hili suala la uvamizi wa tembo katika maeneo yanayozunguka au ya kandokando ya hifadhi kwamba, Serikali ina vikosi ambavyo viko katika Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa kutumia Jeshiusu inaendelea kuwaondoa hawa tembo na wanyama wengine wakali ili kuwawezesha binadamu kuendelea na shughuli zao za kila siku.

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la kundi la ng’ombe kwamba wanahamia kwenye maeneo ambayo yamepakana na hifadhi; naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Vita Kawawa kwamba Kamati ya Mawaziri iliundwa na Serikali kuangalia maeneo yote yenye migogoro ikiwemo migogoro inayozunguka mipaka yote ya hifadhi. Sasa hivi Kamati hii ilishamaliza kazi yake na utekelezaji wake unaenda kuanza baada ya Bunge hili Tukufu kumalizika. Hivyo maeneo yote ambayo yana migogoro kama ya namna hii Serikali inakwenda kuyamaliza na niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa kwamba wote ambao wana changamoto hii inakwenda kumalizwa na maamuzi ya Kamati ya Mawaziri. Ahsante. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Sisi Namtumbo kule tuna miradi ya maji yenye takriban miaka nane lakini bado haijakamilika na kuna changamoto ya ukamilifu wa miradi hiyo hasa vifaa na mabomba. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kuwa tayari kuongozana nami kabla ya Bunge la Bajeti kwenda kuona miradi hiyo na changamoto yake na kuona ni jinsi gani atatuongezea nguvu ili kukamilisha miradi hiyo? (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Vita Kawawa unataka kuongozana na Naibu Waziri au Waziri? Ni yupi uliyemwomba kati ya hao? (Makofi/Kicheko)

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri. (Makofi/Kicheko)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa namna anavyojibu maswali vizuri na nimpongeze na Mheshimiwa Mbunge kaka yangu Kawawa kwa kazi kubwa anayoifanya Namtumbo. Kubwa mimi nipo tayari kuongozana naye. Mkoa wa Ruvuma pia ni moja ya mikoa ambayo tumeainisha hii changamoto ya maji na tumewapatia zaidi ya bilioni nane na katika wilaya yake tumeipa 1.3 billion katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji. Kwa hiyo, tunamtaka Mhandisi wa Maji, Namtumbo aache porojo, afanye kazi kuhakikisha wananchi hawa wanaweza kupata huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwanza naomba niipongeze Serikali Kuu kwa kazi nzuri inayoifanya ya kutusambazia umeme. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wananchi wa Namtumbo nyumba zao na taasisi wamefanyakazi yao nzuri ya wiring, lakini wanacheleweshewa kuunganishiwa umeme hususan kijiji cha Mbimbi na Taasisi ya Hunger Seminary na Shule ya Sekondari ya Msindo.

Je, Serikali inaweza kuielekeza TANESCO waharakishe uunganishwaji wa umeme katika vijiji na taasisi hizo?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mazingira ya Namtumbo maeneo mengi yana mchwa na yanasumbua sana nguzo za umeme zisizokuwa treated vizuri. Je, Serikali inaweza kuelekeza namna bora ya ku-treat nguzo zinazowekwa au kuwekwa nguzo rafiki na mazingira ya mchwa ya Namtumbo na kwingineko ili kuepuka hasara inayoweza kujitokeza katika mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Namtumbo ni mojawapo ya Wilaya ambazo zilikuwa zinapelekewa umeme katika awamu ya tatu mzunguko wa kwanza wa REA. Kilichotokea ni kwamba baada ya kufanyika kwa kazi ya awali wakandarasi waliowengi waliongezewa kazi za nyongeza katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuwafikia wananchi walio wengi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Namtumbo imekuwa ni mojawapo kati ya maeneo ambayo yameongezewa maeneo ya nyongeza na hivyo kushindwa kukamilisha kazi iliyopangwa kwa wakati. Mkandarasi ambaye alikuwa anafanyakazi katika Mkoa wa Ruvuma NAMIS Cooperate ameongezewa muda wa kukamilisha kazi katika mkoa huo mpaka kufikia mwezi Aprili na katika Wilaya ya Namtumbo tayari ile kazi iliyokuwa imeongezeka nguzo zimesimikwa, waya zimepelekwa na kilichobaki sasa ni upatikanaji wa mita kuweza kuwafikishia huduma wale wote waliopelekewa umeme. (Makofi)

Kwa hiyo, nimuahidi Mheshimiwa Vita kwamba ifikapo mwezi Aprili tayari wale wote waliounganishiwa umeme watakuwa wamewashiwa umeme katika maeneo yao bila kuchelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili alitaka kujua uwezekano wa kuweka miundombinu itakayokuwa rafiki na ya uhakika katika maeneo ambayo tayari yana matatizo mbalimbali. Tunafahamu na sasa ni maelekezo ya Wizara kwamba katika yale maeneo ambayo oevu kwa maana ni maeneo yenye majimaji, katika maeneo ya hifadhi na katika maeneo yenye matatizo mengine na changamoto kama hizo za miti kuliwa na mchwa tumeelekeza kwamba wenzetu wa TANESCO na REA basi watumie nguzo za zege zinaitwa concrete polls ili kuhakikisha kwamba tukiziweka basi zinakuwa za kudumu na zinakaa kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niongezee kwamba kwa sababu Waheshimiwa Wabunge wanayafahamu maeneo yao yana matatizo gani, basi maelekezo ya Wizara ni kwamba wale wakandarasi watakaoenda kufanyakazi katika Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili wa REA wahakikishe wanawasiliana pamoja na mamlaka nyingine watakazoziona kwa maana ya TANESCO kupeleka …. kwa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya lakini pia wafanye consultation kwa Waheshimiwa Wabunge ili waweze kutoa maoni yao na ushauri wao maeneo gani yanaweza yakafanyiwa nini hata kama siyo ya kitaalam lakini yakichanganywa na ya kitaalam yatatusaidia kuhakikisha miundombinu yetu inadumu katika maeneo husika. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kule kwetu Namtumbo kuna vituo vya afya viwili; Kituo cha Afya cha Mkongo na Kituo cha Afya cha Mputa ambavyo vilijengwa mwanzoni mwa miaka 1980 na hali yake kwa sasa hivi ni mbaya sana.

Kwa kuwa wakati ule vilipojengwa kulikuwa hakuna majengo ya upasuaji, je, Serikali inaweza ikatusaidia kutuletea au kututengea fedha kwa ajili ya kukarabati vituo hivyo vya afya na kujengewa vyumba vya upasuaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya utoaji huduma za afya na kwa muktadha huu inajumuisha ujenzi wa vituo vya afya, upanuzi na pia ukarabati vituo vya afya. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Kituo cha Afya cha Mkongo na Mputa ni Vituo vikongwe na vinahitaji kufanyiwa upanuzi na vinahitaji kukarabatiwa na kuongezewa baadhi ya majengo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Vita Kawawa, Mbunge wa Namtumbo kwamba Serikali inachukua hoja hii na kwenda kuifanyia kazi ili tuweze kuona kadri ya upatikanaji wa fedha, tunatenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa vituo hivyo na pia kuongeza majengo; yakiwepo ya upasuaji na majengo mengine ili viweze kutoa huduma bora kwa wananchi.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. kwanza, kwa ruhusa yako, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, alikuja mwenyewe Namtumbo katika kituo hiki na aliona hali halisi ya kituo hiki ambacho Serikali iliwekeza fedha nyingi huko nyuma lakini kilitelekezwa.

Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza; kwa kuwa Serikali pia ilikiri kwamba kituo kile kina umuhimu wa pekee, hasa kutokana na ikolojia yake, ni kituo pekee kwa Kanda ile ya Nyanda za Juu Kusini. Sasa je, Serikali kwa kuona umuhimu huo, kuanzia sasa inaweza katika mipango yake kuweka fedha za kutosha lakini pia kupeleka wataalam wa kutosha – siyo wanne – wa kutosha, au kushirikiana na mashirika kwa mfumo wa PPP ili kuweza kuzalisha mbegu kwa wingi katika eneo lile?

Mheshimiwa Spika, la pili; kwa kuwa iliyokuwa Taasisi ya Uyole ya Kuzalisha Mbegu wakati ule ilimaliza mgogoro wa ardhi pale kwa kuwaandikia na kuwapatia barua Kijiji cha Suluti kuwakabidhi hekta zao 100. Sasa je, Serikali inaweza kukamilisha taratibu hizo ili wananchi wale pia waweze kulitumia kiuhalali eneo lile kama out growers lakini pia kufanya shughuli zao za maendeleo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Vita Kawawa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu kumaliza mgogoro wa hekta 100, mimi na yeye tulikuwa pamoja na niliagiza watu wa TARI na watu wa ASA pamoja na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao na halmashauri yake wapime zile hekta 100 ambazo tayari zina makazi ya wananchi na hatuna sababu ya ku-hold eneo ambalo tayari watu wameshajenga hadi nyumba, ni kuichonganisha Serikali. Na nimhakikishie tu kwamba hizo hekta 100 utaratibu utakamilika kama tulivyokubaliana na wananchi watakabidhiwa hizo hekta 100.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la kupeleka wataalam na kukifufua, nilihakikishie Bunge lako mwaka huu tunaanza kazi hiyo na tuta-repair majengo na hao watumishi wanne watakuwa ni watumishi watakaoishi palepale, lakini siyo watakaofanya kazi; watashirikiana na Kituo cha Uyole kwa ajili ya kutatua changamoto. Hao ndiyo watakuwa stationed pale mnapopaita SQU kwa umaarufu kule kwenu. Nashukuru. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii niwaulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wakulima wa tumbaku wanalipwa District SES pia wanalipa tozo ile ya Vyama Vikuu vya Ushirika na Chama cha Msingi. Lakini imesikika mwaka huu pia kwamba wakulima wa tumbaku watakatwa na TRA kodi katika mauzo yao ya tumbaku. Nataka kujua Serikali suala hili ni kweli au siyo kweli?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa. Ni kweli Bunge lako tukufu lilipitisha utekelezaji wa Sheria ya Withholding Tax ya 2% kwenye mazao ya kilimo. Lakini kama wizara hatua tuliyochukua kwamba mjengeko wa bei ya tumbaku huamuliwa kati ya mwezi wa pili, tatu na wa nne.

Mheshimiwa Spika, wakati mjengeko wa bei ya mauzo ya mwaka huu yamepitishwa suala la withholding tax halikuwepo. Kama Wizara tumeshawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Fedha tumewaandikia ili tuone namna gani utekelezaji wa sheria hii uweze kuwa withhold kwa sababu mjengeko wa bei haukuhusisha withholding tax ya 2%. Jambo hili liko katika mazungumzo na wenzetu wa Wizara ya Fedha niwahakikishie tu kwamba tutafikia muafaka na kuweza kulinda maslahi ya wakulima katika eneo hili.