Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Vita Rashid Kawawa (3 total)

MHE. VITA R. KAWAWA Aliuliza:-

Kumekuwa na ongezeko la wanyamapori katika Hifadhi ya Mbuga ya Selous na sasa tembo na nyati wanavamia mashamba pamoja na makazi ya wanavijiji na kuleta taharuki:-

Je, Serikali inaweza kuwarudisha wanyama hao porini mbali zaidi na wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mali asili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara imeandaa na inatekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kusimamia Utatuzi wa Migongano baina ya binadamu na wanyamapori.

Aidha, Wizara inaendelea kukamilisha utaratibu wa kuweka alama katika shoroba na mapito ya wanyamapori ili kuimarisha uhifadhi wake na kuendelea kufanya utafiti na kueneza matumizi ya mbinu mbadala za kujikinga na wanyamapori waharibifu hasa tembo. Baadhi ya mbinu hizo ni: Matumizi ya pilipili, mafuta machafu (oil) na mizinga ya nyuki; na kutoa mafunzo kwa askari wa wanyamapori wa vijiji. Katika Wilaya ya Namtumbo, jumla ya askari wa wanyamapori wa vijiji 198 wamepewa mafunzo.

Mheshimiwa Spika, Wizara imekuwa ikiendelea kufanya doria za msako kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu ambapo katika kipindi cha Julai hadi Disemba, 2020 zilifanyika doria za msako zenye jumla ya sikuwatu 133 katika vijiji vya Wilaya ya Namtumbo; kutoa elimu kwa wananchi juu ya mbinu za kujikinga na wanyamapori wakali na waharibifu ambapo jumla ya wananchi 2,303 walipata elimu katika vijiji 42 vya Wilaya za Namtumbo na Tunduru; kuimarisha vituo maalum vya doria za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu katika Kanda za Kalulu na Likuyu- Sekamaganga.
MHE. VITA R. KAWAWA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kusambaza umeme wa REA kwenye baadhi ya vitongoji vya vijiji vya Namtumbo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Namtumbo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Shirika la Umeme nchini (TANESCO) pamoja na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kupeleka umeme katika vijiji na vitongoji nchini. Vijiji vyote 14 vilivyobaki katika Wilaya ya Namtumnbo vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili unaotarajiwa kuanza mwezi Februari, 2021 na kukamilika mwezi Septemba, 2022. Mradi huu utahusisha pia kupelekea umeme vitongoji vya vijiji vitakavyopelekewa umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa vitongoji vyote nchini vikiwemo vya Wilaya ya Namtumbo vitaendelea kupelekewa umeme kupitia miradi ya umeme vijijini kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. VITA R. KAWAWA Aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukifufua Kituo cha Utafiti na Uzalishaji Mbegu cha SKU – Suluti cha Shirika la Kilimo Uyole kilichopo Wilayani Namtumbo ambacho kwa sasa hakifanyi kazi na majengo yake yameharibika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Suluti chenye jumla ya hekta 378 ni miongoni mwa vituo vidogo vilivyo chini ya Taasisi ya Utafiti Tanzania (TARI – Uyole) vinavyofanya utafiti na uzalishaji wa mbegu kwa kufuata ikolojia. Kwa muda mrefu kituo hiki kimekuwa kikizalisha chini ya uwezo na hivyo kusababisha maeneo ya mashamba kutotumika kikamilifu na miundombinu mingine ikiwemo nyumba, maghala na baadhi ya mashine kuharibika kwa uchakavu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia ikolojia ya Suluti, TARI, Serikali katika Mwaka wa Fedha wa 2021/2022 ina mpango wa kumaliza mgogoro wa ardhi katika eneo la hekta 100 zilizovamiwa, kupeleka kiasi cha fedha shilingi milioni 200 kwa ajili ya kulima mbegu za alizeti, mahindi na soya. Kati ya hizo, milioni 70 zitatumika katika kilimo cha alizeti, milioni 100 zitatumika katika kilimo cha mahindi na milioni 30 zitatumika kwa kilimo cha soya.

Mheshimiwa Spika, vilevile Wizara ina mpango wa kukarabati majengo na kuongeza watumishi kutoka watumishi wawili kwenye kituo hicho na kufikia watumishi wanne. Mpango wa Wizara katika msimu wa Fedha 2021/ 2022 ni kuiwezesha TARI kuongeza uzalishaji wa mbegu mama za mahindi na soya. Vilevile TARI inatarajia kulima hekta 200 za alizeti ambapo mbegu hizo zitawafikia wakulima ili kuzalisha alizeti na kupunguza uhaba wa mafuta ya kula nchini.