Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Deodatus Philip Mwanyika (12 total)

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa mradi huu kama alivyosema yeye mwenyewe utachukua miezi 24, miaka miwili na wananchi wa Njombe wakati huo wataendelea kupata tabu na kuteseka hasa wakati wa kiangazi maji yanapopotea kabisa. Je, Serikali itakuwa tayari kutekeleza miradi mingine midogo midogo ambayo baadhi imekwishabuniwa na inafahamika na mingine inaweza kubuniwa, kwa vile Njombe tumezungukwa na mito kila upande?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali ilishatekeleza mradi mdogo katika Mji wa Kibena pale Njombe, kwa kupeleka maji mpaka Hospitali ya Wilaya ya Njombe na kuna tanki kubwa sana wamelijenga pale na tanki hilo lina maji mengi na saa nyingine yanabubujika na kumwagika. Kwa bahati mbaya wananchi wa eneo la Kibena ambao wanaishi maeneo yale bado hawana. Je, Serikali haioni kama itakuwa ni busara na jambo jema badala ya maji yale kuwa yanabubujika na kumwagika sasa wakatoa pesa na kuweka mradi mdogo wa kutawanya maji ili wananchi wa Kibena wapate kuwa na maji ya uhakika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nijibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwanyika kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala la hofu kwa sababu mradi utaanza mwezi Aprili na yeye anapenda visima ama miradi midogo midogo, nipende tu kumwambia kwamba tayari Wizara inafanya mchakato huo na hili linashughulikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na mradi ambao unapeleka maji kwenye hospitali ya Kibena pale kwa kuhitaji distribution tayari Wizara imetoa maelekezo kwa mameneja walioko pale wanafanyia upembuzi yakinifu ili kuona namna gani kama distribution itawezekana. Naomba kukupa amani Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi huu ambao tunauanza mwezi Aprili, tutaenda kuufanya kwa kasi nzuri na tutaweza kutawanya maji kadri mradi unavyokamilika hatutasubiri mradi ukamilike mpaka mwisho, ukifika hata asilimia 40 wale ambao wanapitiwa na lile eneo ambalo miundombinu imekamilika maji yataweza kutoka. (Makofi)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ambayo inaongelewa ya kwenda Kishapu ni sawasawa kabisa na barabara ya kilometa 60 ndani ya Mji wa Njombe yaani Ntoni na kwenda mpaka Lusitu. Barabara hii tunaambiwa ilishafanyiwa upembuzi yakinifu, imeshafanyiwa usanifu wa kina lakini sio tu hivyo, barabara hii vilevile imekuwa kwenye ahadi za Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2015 - 2020 na mwaka 2020 – 2025.

Swali, ni lini sasa Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara hii ambayo ni muhimu sana kiuchumi na inapita katika maeneo ya Njombe Mji, Uwemba, Luponde na Matola? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Mwanyika, Mbunge wa Njombe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayoisema atakubaliana na mimi kwamba iko sehemu ambayo ndiyo inakwenda mpaka huko Ludewa tayari imeshaanza kufanyiwa kazi na mimi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge awe na subira, kipindi hiki ni cha bajeti tunatambua umuhimu wa hii barabara na nadhani baada ya bajeti ataamini kwamba Serikali kweli ina mpango wa kuhakikisha kwamba barabara hii ya Njombe – Itoni – Lusitu inajengwa. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii iko kwenye mipango ya Wizara kwa maana ya Serikali kwamba itaendelea kujengwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi lakini niulize swali la kwanza. Kwanza tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa maamuzi aliyoyatoa siku ya Jumatatu ya kuruhusu kuajiriwa kwa walimu 6,000 kwa haraka, tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni ukweli kwamba walimu 6,000 wanaokwenda kuajiriwa bado wanakwenda kufanya replacement; mahitaji ya walimu katika shule bado ni makubwa sana. Maamuzi ya Serikali ya kutoa elimu bure kwa nia njema yamefanya kuwe na uhaba mkubwa sana wa walimu katika maeneo hasa ya vijijini. Kwa hiyo, pamoja na mipango ambayo imeelezewa lakini bado kuna tatizo kubwa na ninapenda kujua, je, Serikali inaweza bado ikatoa commitment kwamba itaajiri walimu wa kutosha? Kwasababu hii namba iliyotajwa hapa bado haitoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; naelewa kuna vigezo ambavyo vinatumika kwenye ugawaji wa walimu kwenye maeneo mbalimbali. Ni ukweli usiopingika kwamba kwa yale maeneo ambayo ni miji ambayo iko ndani ya halmashauri vigezo ambavyo vinatumika kwa kweli havina uhalisia kwasababu maeneo hayo unakuta yanaangaliwa sana kwasababu yana miji lakini vilevile yana maeneo mengi sana yenye shule nyingi sana ambayo wananchi wamejitoa wakajenga shule ambazo zipo katika maeneo ya vijijini. Wanapoangalia vigezo vya reallocation unakuta kwamba hawaangalii hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali; je, Wizara itakuwa tayari kupitia upya vigezo vya ku-allocate walimu ili maeneo ya halmashauri za miji ambayo yana maeneo makubwa ya zaidi ya kilometa 25 yaweze kupata walimu ili elimu yetu iwe na tija? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri wazi kabisa kwamba alichozungumza Mheshimiwa Mbunge ya uhaba wa walimu nchini pamoja na replacement ya walimu 6,000 ambayo tunakwenda kuifanya hivi karibuni bado upo. Na Serikali imeji-commit hapa katika statement yangu ya awali kwamba tutaendelea kuajiri kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Na mpango huo upo na ni endelevu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge ondoa wasiwasi kwenye hilo kwa sababu Serikali iko makini, na Serikali ya Rais wa Sita, mama Samia Hassan Suluhu, imejipanga kuhakikisha tunaondoa kabisa tatizo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, amezungumzia kuhusu Wizara kama tutakuwa tayari kupitia vigezo vya ugawaji wa walimu upya. Nikubali kabisa hilo tumelipokea, moja, ni kama ushauri, lakini pili, tutaendelea kulizingatia kuhakikisha kabisa ugawanyaji wa walimu wote nchini unafuata usawa na haki katika maeneo yote. Ahsante sana.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa Njombe Mjini na sisi tuna Kituo cha Afya ambacho kina uhitaji wa wodi ya kibaba na wazazi na huduma ya upasuaji na Serikali ilishaonesha nia ya kutusaidia.

Swali, je, ni lini sasa shughuli ya ujenzi na ukarabati wa kituo cha afya cha muda mrefu sana Njombe Mjini utaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Mwanyika, Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika Jimbo la Njombe Mjini kuna Kituo cha Afya cha Mji Mwema na cha siku nyingi ambacho kina uhitaji mkubwa wa miundombinu ya wodi ya akina baba akina mama lakini na wodi ya watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti ya mwaka huu wa fedha tumetenga fedha kwa ajili ya kwenda pia kuongeza miundombinu katika Vituo vya Afya na nimuhakikishie kwamba Kituo cha Afya cha Mji Mwema katika Jimbo la Njombe Mjini nacho kitapewa kipaumbele.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Moja, baada ya ufuatiliaji wa karibu sana kwenye suala hili imedhihirika wazi kwamba kwa Jimbo la Njombe ni vijiji vinne tu, Mgala, Ngalanga, Mtila na Mbega ndivyo vilivyoingizwa kwenye Mpango ambao Mheshimiwa Naibu Waziri anauongelea. Kuna vijiji takriban 20 ambavyo vimesahaulika, vijiji hivyo ni Hungilo, Uliwa, Utengule, Diani, Makolo, Lugenge, Mpeto n.k. Naomba Serikali itoe kauli kuhusiana na suala hili na iwadhihirishie wananchi wa Njombe kama sasa baada ya maongezi kati yangu, Waziri na REA vijiji vilivyobaki vyote vimeingizwa katika Mpango huo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Pamoja na vijiji vingi kuunganishwa na hasa kwenye Jimbo letu la Njombe Mjini bado tuna ukatikaji wa umeme mkubwa sana ambao unaashiria kwamba pamoja na kuunganishwa, tatizo hili litaendelea kuwa kubwa. Tunaomba maelezo ya Wizara kuhusiana na ukatikaji wa umeme katika Mji wa Njombe ambao ni endelevu na hauishi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ni kweli mara ya kwanza vilichukuliwa vijiji vinne lakini baada ya Mheshimiwa Mwanyika kuwasiliana na ofisi na tunamshukuru na kumpongeza kwa ufuatiliaji wake mkubwa, Wizara imeamua iongeze scope ya kazi ya awali na kuongeza vijiji hivyo.

Mheshimiwa Spika, kimsingi vilikuwa havikuachwa lakini vilikuwa vimebaki kwasababu viko katika eneo linalokaribiana na mji. Kwa hiyo, vilikuwa havikuingia kwenye mradi wa REA lakini tumevichukua tukivi-treat kama peri- urban area. Kwa hiyo, vijiji hivyo 20, nimhakikishie Mheshimiwa Deo Mwanyika kwamba vimeingia na vitafanyiwa kazi katika awamu hii ya kupeleka umeme vijijini.

Mheshimiwa Spika, katika swali la pili, ni kweli. Maeneo ya Njombe yana tatizo kubwa sana la ukatikaji wa umeme. Naomba nitumie muda kidogo tu kukueleza tatizo kubwa tulilokuwa nalo Njombe na hatua taunazozichukua. Njombe inapata umeme kutoka katika kituo chetu cha kupooza umeme cha Makambako na kuna kilometa 60 kutoka pale Makambako mpaka Njombe, Njombe Mji na eneo kubwa la Mkoa. Sasa Njombe tunayo matatizo makubwa matatu.

Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa la kwanza ni baraka ambazo Njombe imezipata ya kuwa na miti mingi sana. Ile miti, pamoja na sisi kufyeka ile line ya kupitisha umeme, lakini miti inayokuwa nje ya line yetu ya umeme baadaye inaangukia ndani ya line yetu kwa sababu inakuwa ni mirefu sana. Kwa hiyo, tumeendelea kufyeka na kuhamasisha wananchi basi hata watuongezee line ambayo iko nje zaidi ya line yetu sisi ili tunapofyeka basi miti inayotokea nje ya line
yao isije ikaleta shida kwenye eneo letu.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo linatupa shida sana kwa Mkoa wa Njombe ni radi. Maeneo ya Njombe, kama nilivyowahi kusema hapa, Mkoa wa Kagera lakini pia Mbeya, tunayo matatizo makubwa sana ya radi ambazo zimekuwa zikileta shida kwenye miundombinu yetu ya umeme.

Mheshimiwa Spika, tunachokifanya kwa Mkoa wa Njombe kwa mfano kila tunapofunga transformer tunaifanyia earthing system. Ile earthing system inatakiwa uzamishe chini, lakini unapima udongo kuona resistance value ya udongo ni kiasi gani. Kama iko 0 - 60 inakuwa haina shida, kama iko zaidi ya 60 inabidi kutumia zile njia za kienyeji na za kitaalam za ku--treat udongo ili radi ikienda iweze kumezwa kule, tunatumia mbolea na vitu vingine kama hivyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, pengine tukifunga transformer tunachelewa kuiwasha kwa sababu tukipima resistance value ya udongo tunaona bado ina-resist sana radi, kwa hiyo, tunaamua kuiacha kwanza ili ipoe kidogo.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri.

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie. Naomba niruhusiwe kutoa nondo kama alizozitoa mwenzangu Ndaisaba jana kwa ajili ya uelewa mzuri.

Mheshimiwa Spika, lakini eneo la pili tunafunga vifaa vya muhimu sana vinavyoitwa surge arrester and combi unit kuhakikisha kwamba transformer haiharibiki mara kwa mara. Kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Deo kwamba tutaendelea kuhakikisha kwamba…

SPIKA: Nakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameyatoa, naomba niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Njombe ni moja katika mikoa mitano bora ambayo imefikia kiwango cha uchumi wa kati kwa watu wake, mkoa huu ni moja kati ya Halmshauri 10 bora kwa makusanyo zinazizidi hata Manispaa zaidi ya 10 katika nchi hii. Mkoa wa Njombe ni mkoa ambao una miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo parachichi pamoja na Liganga.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu; hivi ni kigezo gani kinachotumika maana wasiwasi wetu hata katika viwanja 11 tunaweza tukawa wa mwisho kwa sababu sioni ni vigezo gani, ukienda kwa niliyoyasema Mkoa wa Njombe unatakiwa uwe mkoa wa mwanzo kupata uwanja wa ndege? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deodatus Phillip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tunatambua mchango mkubwa wa kiuchumi kutoka Mkoa wa Njombe kwa ujumla wake pamoja na Njombe Mjini. Lakini vilevile uwezo wa Serikali siyo mkubwa kiasi hicho kujenga viwanja hivi vyote 11 kwa wakati mmoja. Safari ni atua upembuzi yakinifu umefanyika sasa tunajua gharama ya kujenga uwanja wa ndege wa Njombe ni gharama kiasi gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukweli ni kwamba unaangalia, ameuliza vigezo kwa mfano, pale Iringa mjini kuelekea Mkoa wa Iringa karibu kabisa na Makambako na Mkoa wa Njombe, sasa hivi tunazungumza mkandarasi yuko site anaendelea kufanya kazi ya kumaliza runway ili ndege aina zote ziweze kutua eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wakati ambao Serikali inaendelea kupata fedha kutoka mapato ya ndani na washirika wengine wa kimaendeleo, watu wanaotaka kwenda Njombe wanaweza kutumia alternative kutumia uwanja Iringa baada ya kuwa umekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali yake ni njema tungependa kila Mkoa uwe na uwanja wa ndege na Waheshimiwa Wabunge wakitoka hapa baada ya Bunge kuahirishwa wangependa kutoa katika mikoa yao, lakini kwa kuwa fedha nyingi kiasi hicho tuvumiliane tupeane muda kazi hii itakamilika, ahsante sana.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Njombe tunapitiwa na gridi inayotoka Makambako kwenda Songea, lakini bado tumekuwa na tatizo kubwa sana la ukatikaji wa umeme ambao sisi tunaamini pamoja na maelezo ambayo Waziri ameyatoa siku ya nyuma, tunaamini kutokana na grid stability, ni lini sasa suala la ukatikaji wa umeme usioisha wa Mkoa wa Njombe na Mji ya Njombe utafikia tamati? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwanyika, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hasa katika eneo la Njombe pamoja na Ludewa umeme unakatika kwa kiasi kikubwa kwa sababu kuna matengenezo ya kufunga auto recloser ambayo inaimarika ndani ya siku 28. Pia katika maeneo ya Njombe na Ludewa ipo line ambayo tunaongezea, tumetenga shilingi bilioni 270 katika mikoa miwili na bilioni 100 kila mkoa kwa ajili ya shughuli za ukarabati wa mitambo na kuimarisha umeme katika Mkoa wa Makambako, Njombe pamoja na Ludewa. Kwa hiyo niwahakikishie wananchi wa Ludewa pamoja na Njombe kwamba ndani ya muda unaokuja ambao nimeutaja hali ya umeme itaimarika kwa kiasi kikubwa.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara ya Mtila - Lugenge mpaka Usalule ni barabara ya muhimu sana nani barabara inayounga wilaya tatu ikiunga pamoja na Hospitali kubwa ya Mkoa wa Njombe. Je, Serikali haioni kwamba ni muhimu sana hii barabara na yenyewe ikaingizwa katika mpango wa TANROADS kwa sababu mchakato umeshaanza na umekwama mahali Fulani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwanyika, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba hoja hii Mheshimiwa Mbunge amefikisha ofisini katika Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Kama alivyosema mwenyewe kwamba mchakato unaendelea, naomba a-speed up process hiyo na sisi tutatoa ushirikiano, itakapokidhi vigezo tutaipokea kama TANROADS, tutaitengeneza na wananchi wake watapata huduma muhimu katika eneo hilo. Ahsante.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mkoa wa Njombe mpaka miaka michache iliyopita ulionekana kama ni mkoa mpya. Katika maeneo yaliyosahaulika kwa Mkoa wa Njombe ni Vituo vya Polisi. Je, Serikali ni lini sasa itaanza kukarabati Kituo cha Polisi cha Mkoa wa Njombe ili kiendane na hadhi ya Mkoa wa Njombe? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo ameliuliza, linalozungumzia suala la ukarabati wa Kituo cha Polisi Njombe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba azma yetu ni kuhakikisha kwamba vituo vyote vinajengwa ipo pale pale. Lakini kikubwa nimwambie tu kwamba tutajitahidi pia katika mwaka wa fedha ujao tuhakikishe kwamba kituo hiki nacho tunakijenga kikawa katika hadhi ile ya kuhakikisha kwamba wananchi wanaweza kupata huduma hizi za ulinzi na usalama. Nakushukuru pia.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu yaliyotolewa lakini bado kuna sintofahamu kuhusiana na status ya hiki Kituo. Nitaomba Mheshimiwa Waziri alifuatilie kwa karibu kwa sababu, wananchi wale wenye Bima wanashindwa kupata huduma kwa sababu wanasema officially hakijawa registered kwa hiyo kuna sintofahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili, pamoja na Kituo hiki lakini Njombe tuna vituo vingine viwili vya Afya ambavyo havina vifaa ambavyo tumeahidiwa kwa muda mrefu, Kituo cha Makoo pamoja na Kituo cha Kifanya. Mawaziri wametembelea pale lakini tumepewa ahadi na hatuelewi. Sasa je, Serikali inaweza ikatoa kauli kuhusiana na hivyo vituo viwili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Deodatus Phillip Mwanyika, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Zahanati ya Ihalula imekwisha pandishwa hadhi kuwa Kituo cha Afya na imekwishapewa namba ya usajili kama Kituo cha Afya. Kwa hivyo, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hiyo sintofahamu ilikuwa kwa sababu hatukuwa tumepata namba rasmi ya usajili kuwa kituo cha Afya ili National Health Insurance Fund waanze kuilipa moja kwa moja. Kwa hiyo, sasa limeshafanyika, lakini kama kuna changamoto nyingine zote tutakwenda kuzifuatilia kuhakikisha wananchi wetu wanapata huduma za ngazi ya Kituo cha Afya.

Mheshimiwa Spika, lakini pili, tumekuwa na ujenzi wa Vituo vingi vya Afya, vikiwemo Kituo cha Afya cha Makoo na Kifanya; na mpango wa Serikali ni kuendelea kutenga fedha za ununuzi wa Vifaa Tiba na Makoo ni moja ya vituo ambavyo Mheshimiwa Waziri wa Nchi alitembelea, aliahidi Vifaa Tiba na utaratibu unaendelea kuhakikisha Vifaa Tiba vinafika pale. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili linafanyiwa kazi. Ahsante. (Makofi)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa kumtua mama ndoo kichwani mradi mkubwa ambao utasababisha hili litokee ni mradi wa Miji 26 ambao unafadhiliwa na Serikali ya India. Tunaomba kuuliza Mheshimiwa Waziri.

Ni lini mradi huu utaanza na umefikia wapi? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge lakini kama unavyotambua program ya kumtua mwana mama ndoo kichwani ni programu ya Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan. Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maji kupitia bajeti ya Serikali lakini kupitia wadau mbalimbali wa maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Serikali ya India tunatarajia kutekeleza miradi ya Miji 28 zaidi ya dola milioni 500 na mpaka sasa hatua ambayo tumefikia taratibu zote za kimanunuzi kama Wizara ya Maji tumeshazikamilisha. Tunasubiri kibali (no objection) kutoka Exim Bank na hivi karibuni tutapata, katika kuhakikisha tunatekeleza miradi hiyo na wananchi waendelee kupata huduma ya maji safi na salama.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Jimbo la Njombe Mjini tuna vituo viwili vya afya ambavyo vimejengwa kwa nguvu za wananchi na mapato ya ndani. Vituo hivi vimetembelewa na Mawaziri karibu wote wa TAMISEMI. Nipende kuuliza; ni lini sasa vituo hivi ambavyo viko tayari kwa asilimia 100 vitapata vifaa na watumishi ili viweze kuanza kutoa huduma kwa wananchi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Mwanyika, Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mwanyika kwa kuwasemea kwa ufasaha sana wananchi wa Jimbo la Njombe Mjini na kwa kweli hoja hii ameizungumza hapa zaidi ya mara mbili na sisi kama Serikali tumhakikishie tulishachukua hoja hii kwa ajili ya kupeleka vifaatiba kwenye vituo vile viwili vya afya, lakini pia kufanya mpango wa kupata watumishi pale na fedha tayari ziko MSD.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachosubiri ni manunuzi ya vifaatiba hivyo ili viweze kupelekwa kwenye Jimbo la Njombe Mjini. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili linafanyiwa kazi. Ahsante.