Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Deodatus Philip Mwanyika (5 total)

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA Aliuliza:-

Je, ni lini mradi wa kusambaza maji Mji wa Njombe kutoka Mto Hagafilo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, Mbunge wa Njombe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ilipata mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim India jumla ya Dola za Marekani millioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika miji 28 Tanzania Bara na Zanzibar. Moja ya miji itakayonufaika na mkopo huo ni Mji wa Njombe, kwa sasa mradi upo katika hatua za manunuzi na tunatarajia Wakandarasi watakuwepo eneo la mradi kwa ajili ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi ifikapo mwezi Aprili, 2021 na ujenzi wa mradi utachukua miezi 24.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA Aliuliza:-

Je, Serikali inachukua hatua gani kumaliza tatizo la upungufu wa Walimu nchini, hasa shule zilizopo maeneo ya vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Phillip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa walimu katika shule za msingi na sekondari, kuanzia Disemba 2015 hadi Septemba 2020, Serikali imeajiri walimu 10,666 wa shule za msingi na walimu 7,515 wa shule za sekondari na kuwapanga kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa. Aidha, kuanzia mwezi Desemba 2015 hadi Septemba 2020, Halmashauri ya Mji Njombe imeajiri walimu 21 wa shule za msingi na walimu 111 wa shule za sekondari. Vilevile Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itaajiri walimu wapya 6,000 wa shule za msingi na sekondari ifikapo Juni 2021 ili kujaza nafasi zilizoachwa na walimu waliofariki ama kustaafu kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, kupitia ofisi za wakuu wa mikoa imekuwa ikifanya uhamisho wa ndani kwa kuwahamisha walimu waliozidi hasa kwenye maeneo ya mijini na kuwapanga kwenye shule zenye uhaba mkubwa wa walimu ambazo nyingi zipo maeneo ya vijijini. Serikali itaendelea kuajiri na kuwapanga walimu kwenye shule za msingi na sekondari hasa zenye mahitaji makubwa kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -

Je, ni lini Vijiji na Vitongoji nchini ambavyo havijapatiwa umeme vitapatiwa huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) inaendelea kutekeleza mradi wa kusambaza umeme vijijini Awamu ya III mzunguko wa pili. Mradi huu unatarajiwa kufikisha miundombinu ya umeme katika vijiji vyote 1,974 ambavyo havijapata umeme kati ya vijiji 12,268 vya Tanzania Bara.

Mheshimiwa Spika, mradi huu pia utafikisha umeme katika vitongoji 1,474 ambavyo havijafikiwa na umeme. Mradi ulianza mwezi Machi, 2021 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba, 2022. Gharama ya mradi ni takriban bilioni 1,176.

Mheshimiwa Spika, kazi ya kupeleka umeme katika vitongoji ni endelevu. Serikali kupitia REA na TANESCO itaendelea kupeleka umeme katika vitongoji vyote mwaka hadi mwaka kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi wa uwanja mpya wa ndege katika Mji wa Njombe utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): alijibu

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimwa Deodatus Phillip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanja cha ndege cha Njombe ni miongoni mwa viwanja 11 vya ndege vilivyofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Transport Sector Support Project (TSSP). Viwanja hivyo 11 ni pamoja na Lake Manyara, Musoma, Songea, Kilwa Masoko, Tanga, Iringa, Lindi, Moshi, Singida, Njombe na Simiyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hatua ya awali ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika, Serikali imejipanga kuanza ujenzi kwa hatua mbalimbali kwa awamu kwa kutumia fedha za ndani, lakini kutokana na ukweli kwamba gharama za ujenzi wa viwanja hivyo ni kubwa ukilinganisha na bajeti inayotolewa kila mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia bajeti, Serikali kupitia TANROADS imejipanga kuanza na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Iringa na Songea. Ujenzi wa viwanja vilivyobaki kikiwemo cha Njombe utaanza mara Serikali itakapopata fedha. Aidha, kwa sasa Serikali inaendelea kuwasiliana na washirika wa maendeleo ili kuweza kupata fedha za kujenga viwanja hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maelezo hayo hapo juu, namuomba Mheshimiwa Deodatus Phillip Mwanyika pamoja na wananchi wa Njombe Mjini waendelee kuvuta subira kwani Serikali ina nia ya dhati ya kujenga kiwanja hicho.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi Zahanati ya Ihalula kuwa Kituo cha Afya baada ya kukidhi vigezo vyote kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali iliipandisha hadhi zahanati ya Ihalula kuwa Kituo cha Afya mwaka 2018/2019 na kupewa namba ya utambulisho 101604-7. Aidha, Serikali katika mwaka wa fedha 2017/2018 ilipeleka Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ukarabati wa majengo mengine likiwemo jengo la upasuaji ambalo sasa linatoa huduma.

Mheshimiwa Spika, Kituo hiki kimekuwa kikilipwa fedha za Mfuko wa Bima ya afya kama zahanati kutokana na baadhi ya taratibu ambazo zilikuwa hazijakamilika.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto zimekwishalifanyia kazi na barua rasmi itapelekwa ndani ya mwezi huu. Ahsante.